Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya serikali za Mitaa na Mbunge wa jimbo la Nzega Dr. Khamis Kigwangallah akimtambulisha mke wake Dr Bayoum Awadh wakati wa mkutano huo. |
..............................................................................
Ndugu viongozi mlioko hapa, wageni waalikwa, wanahabari na
watanzania wenzangu mnaonisikiliza;
Ni heshima kubwa sana kwangu kupata fursa hii. Ni katika nchi
chache sana duniani, mtoto wa maskini kama mimi, aliyewahi kutembea mitaani
akiuza karanga, Big G, maandazi, jerebi na samaki ili kusaidia wazazi kupata
chochote kwa ajili ya kulisha familia anaweza kuota kuwa Rais wa nchi yake.
Kwamba, mtoto aliyeenda shule bila viatu anaweza kuwa Daktari. Hii inamaanisha
misingi ya haki na usawa kwa wote iliyowekwa na waasisi wa Taifa hili haikuwa
ndoto za alinacha, bali ukweli na uhalisia, na inafanya kazi. Kwamba, siyo
lazima uwe mtoto wa tajiri ndiyo uoneshe kipaji chako.
Hili peke yake linanipa sababu ya ziada ya kwa nini nitamani
kuota kuwa Rais – nataka niwe mfano hai wa mafanikio ya Ndoto ya waasisi wa
Taifa letu, kuwa sote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tuna haki na
fursa sawa bila kujali nani anatokea familia ipi. Hii ni Tanzania ya ndoto za
waliotutangulia.
Ni lazima atokee kiongozi wa kizazi hiki anayetamani kuiongoza
Tanzania itakayodumu kwenye misingi hii: kwamba sisi sote ni ndugu, na tuna
fursa sawa. Kwamba, kuendelea kimaisha na kibinafsi ni haki ya binadamu na si
hisani. Kwamba, mtoto wa mama ntilie kama nilivyokuwa mimi hapa, ana haki na
fursa ya kuwa mbunge ama Rais wa nchi, sawa kabisa na mtoto wa Mbunge.
Kwa namna ya kipekee nichukue fursa hii kuwashukuru na
kuwapongeza waasisi wa Taifa letu kwa kusimamia tunu hizi. Niwashukuru pia
viongozi wote walionitangulia kwa kuzilinda, na niahidi nitakuwa wa mwisho
kuisaliti nchi yangu kwenye mambo haya.
Leo nimefika hapa kwa sababu chama change kina mfumo mzuri
ulioasisiwa na Mwl. Nyerere na umelindwa na Wenyeviti waliomfuatia mpaka na
sisi tumeukuta. Leo nimefika hapa kwa sababu Rais Jakaya Kikwete na wajumbe
wenzake wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu walitumia misingi imara iliyowekwa na
waasisi wa Chama changu kuamua kuwa nami nina haki ya kuwa Mbunge. Leo
nazungumza hapa nikiamini kuwa ni misingi hiyo hiyo itatoa uongozi wa Taifa
letu katika awamu ijayo.
Babu yangu Kizaa Baba aliishi Kijijini Goweko, Mlimani, na
alikuwa mfugaji mkubwa wa ng’ombe na mrina asali mashuhuri. Yeye na mkewe
waliishi maisha ya heshima sana pale kijijini. Hawakuwahi kusoma wala kuajiriwa
japokuwa Babu yangu aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya Chama Cha TANU
na baadaye CCM katika ngazi ya Kata.
Babu yangu na Bibi yangu kizaa mama waliishi Nzega, na ndiyo
walionilea baada ya ndoa ya mama yangu na baba yangu kuvunjika. Walinifundisha
mambo mengi, kubwa likiwa ni kujiamini, pia kufanya mambo yangu kwa bidii,
uadilifu, umakini na kwa nidhamu ya hali ya juu. Bibi yangu huyu hakusoma shule
ya kizungu japokuwa alijifunza kusoma na kuandika.
Babu yangu alikuwa mjukuu wa Chifu na hivyo alipata fursa ya
kusoma Tabora School miaka miwili mbele ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Nyerere. Alifanya kazi mbalimbali chini ya serikali ya wakoloni, na alishiriki
harakati za kuanzishwa na kusambaa kwa chama cha TAA na baadaye TANU. Babu
yangu aliamini kuwa “binadamu wote ni sawa na kwamba kila mtu anastahili
kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake”, na kwamba ukoloni haukuwa kitu cha sawa,
na hivyo kujitawala wenyewe dhidi ya wazungu ilikuwa ni haki yetu; pia aliamini
katika elimu, na hivyo alifanya juhudi kusomesha mabinti zake watatu, mama
yangu aliishia kwenye ualimu kabla ya kuingia kwenye ndoa. Babu aliamini kuwa
Tanzania ya mabinti zake itahitaji wasomi, ndoto ambayo ninaishi kuitekeleza
kwa ajili ya mabinti zangu wawili na Kaka yao, HK Jr.
Japokuwa bibi na babu yangu wameishatangulia mbele ya haki,
naamini wananitazama na kutabasamu huko waliko.
Ninaishi nikiamini kuwa hadithi ya maisha yangu ni mfano hai kwa
maisha ya watanzania wengi. Na kwamba, nina deni la kulipa kwa vizazi vijavyo
kwa kuwa mimi ninafaidi matunda ya mti uliopandwa na vizazi vilivyonitangulia.
Naliona jukumu la kuhakikisha vizazi vijavyo vinafaidi urithi wa Tanzania kuwa
ni la kwangu na wenzangu wa kizazi hiki.
Kazi yangu imenifikisha sehemu nyingi sana za nchi yetu –
vijijini na kwenye majiji, imenikutanisha na watu wa kila aina – matajiri kwa
maskini, wazee kwa vijana – hakuna hata mmoja kati ya watu hawa anayetegemea
Serikali itamtatulia kero zake zote. Wanajua wanapaswa kufanya kazi kwa bidii
ili wasonge mbele – na wana nia ya kufanya hivyo.
Nenda kwa wafanyabiashara wakubwa kule Pugu Road viwandani, kwa
watumishi pale hospitali ya Taifa Muhimbili, ama pale sokoni Kariakoo kwa
wafanyabiashara, wote watakuambia hawapendi kuona kodi zao zikitafunwa na
wachache pale TRA, ama kulipa posho za bure kwa wabunge na mawaziri kule
Bungeni, kulipia mashangingi ya viongozi na watendaji, kulipia tiketi za ndege
daraja la kwanza kwa ajili ya safari za viongozi na wataalamu wetu kwenda
kujifunza kupambana na umaskini wakati wakirudi wanauacha uzoefu uwanja wa
ndege, ama kulipia semina, warsha na makongamano ya wataalamu ya kuandika sera
za MKUKUTA, MKURABITA na kuandaa bajeti zisizotekelezwa kila mwaka.
Watanzania wanataka kupata huduma bora za afya, elimu, maji,
miundombinu.
Nenda kule kwa watani zangu, Nanyumbu, ama Tandahimba, ama kwa
ndugu zangu kule Nduli, Kyela, wazee kule watakuambia hawategemei Serikali
itawaletea ubwabwa kwenye sahani za fedha, wanajua Serikali haitowafanyia kila
kitu, lakini wanajua kabisa kuwa wanapaswa kufanya kazi kwa bidii na wamekuwa
wakifanya hivyo siku zote.
Wanachohitaji wao ni kujengewa mazingira wezeshi kushiriki
shughuli zao za kilimo ama biashara, waelekezwe namna ya kuongeza uzalishaji
kwa kutumia njia za kisasa za kilimo chenye tija na ufanisi, waelekezwe
wanapataje pembejeo, wanapataje mikopo yenye riba nafuu, wanahitaji, mwisho wa
siku, wajue wapi watauza mazao yao kwa uhakika na bila kudhulumiwa wala
kucheleweshewa malipo.
Watu hawatarajii serikali itabeba mizigo yao yote. Lakini
wanaamini kabisa, kwamba tukibadili kidogo tu vipaumbele vyetu, tukibadili
namna tunavyoendesha serikali, tukibadili kidogo namna tunavyoendesha uchumi
wetu, tutaweza, kwa kiasi kikubwa, kubadili muelekeo mzima wa maisha ya baadaye
ya watoto na wajukuu zetu. Tutatoa uhakika wa kuiondoa nchi yetu kutoka
miongoni mwa nchi maskini kabisa duniani.
Na mimi, kama watanzania wenzangu wengi, nina imani kubwa
kabisa, kwamba tunaweza kubadili mustakabali wa Taifa letu. Tunaweza kufungua
milango ya maisha bora zaidi kwa watanzania. Tutatoa fursa sawa kwa kila
mtanzania kuishi kwa matumaini, kwamba atabadili maisha yake wakati wowote ule
kuanzia leo. Tutaweza kuamsha ari ya kila mtanzania kuongeza bidii kwenye kazi
akitumaini na kuamini kuwa kesho yake itakuwa bora kuliko jana yake, kuwa naye
ataishi kwa heshima, raha na starehe ndani ya nyumba yake.
Ninaamini, kutokea ndani kabisa ya mifupa yangu, kuwa tukifanya
uchaguzi sahihi wa vipaumbele vyetu, tukibadili namna tunavyoendesha serikali
yetu, haya ninayoyasema si ndoto za mchana. Ni mambo yanayowezekana.
Watanzania wengi wanaamini, kuwa tukifanya uchaguzi sahihi wa
vipaumbele vyetu, mabadiliko makubwa, na ya haraka yatatokea kwenye uchumi
wetu. Wanaamini tukichagua kiongozi sahihi mwakani, anayejua mahitaji ya nchi
yetu kwa sasa na baadaye, tutafanikiwa.
Nyote mliopo hapa na wanaotusikiliza kutokea nje ya hapa mna
jukumu la kututazama kwa ukaribu sana, kututathmini na kutupima sote;
tuliojitokeza hadharani, walioanza safari za matumaini, wanaotajwa tajwa, na
wale wanaosubiri kuoteshwa ili wakati muafaka ukifika muwape taarifa sahihi
watanzania, kuwa kati yetu sote, ni nani anafaa kutuongoza kuelekea Tanzania ya
ndoto zetu!
Kuwa, ni nani kati yetu ataweza kuwa Amiri-jeshi-mkuu, siyo kwa
uanajeshi wake bali kwa uwezo na utayari wake wa kuwashirikisha wataalamu wa
majeshi na kuamua kwa busara kutumia nguvu za kijeshi pale inapolazimika baada
ya kupima na kuchambua aina nyingine zote za kutafuta suluhu za migogoro kabla
ya kuamua vita.
Kuwa, ni nani kati yetu anayeamini katika uhuru, haki na usawa
na wajibu wa watu wote, kama unavyolindwa na Katiba, anayeamini katika haki ya
kuabudu lakini asiyekuwa tayari kuitumia haki hiyo kuwagawa watanzania kutokana
na dini zao.
Kuwa, ni nani kati yetu anayeamini katika Haki ya kupata huduma
bora za afya, elimu, maji, kama wanavyopata wabunge na mawaziri wetu, kama
wanavyopata mahakimu na majaji wetu, kama wanavyopata wafanyabiashara na
wakurugenzi wetu.
Kuwa, ni nani kati yetu ataweza kuhakikisha kuwa watanzania wote
wanapata haki hizi bila kutazama hali zao kiuchumi ama daraja zao kijamii.
Kuwa, ni nani kati yetu anaamini zaidi katika uhuru na
kujitegemea kwenye masoko na malighafi ili kudhibiti uchumi wetu mpana wa
ndani, kujitegemea kwenye masoko ya pamba na nguo, kwenye mafuta ya kula,
kwenye chakula cha uhakika kwa ajili ya watu wetu, kwenye mafuta na gesi ili
tukwepe mtego wa kuwa sehemu ya uchumi, masoko na biashara za hasara na faida
za makampuni makubwa ya kimataifa nje ya mipaka yetu. Ili tulinde thamani ya
fedha yetu, ili tuwe na uhakika wa ustawi wa maisha ya watu wetu ndani ya nchi
bila athari kubwa kutoka nje ya nchi yetu.
Kuwa, ni nani miongoni mwetu anaakisi taswira sahihi zaidi ya watanzania
walio wengi, historia yake, rekodi yake, wajihi wake, mtazamo wake, ndoto zake,
zinaakisi ‘utanzania’ halisi. Kuwa, yeye ni hitaji sahihi la watanzania.
Wakati ukifika, muwaeleze watanzania ukweli, wafanye uamuzi
unaotokana na taarifa sahihi, wachague mtu sahihi.
Mimi, Ndugu zangu, natangaza rasmi sasa, kuwa ninatia nia ya
kugombea Urais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015.
Na nimefikia uamuzi huu bila kuelekezwa, kusukumwa,
kushawishiwa, kupangiwa ama kupanga na mtu ama na kikundi cha watu, bali kwa
utashi na utayari wangu.
Na ninayasema haya, haswa baada ya kutafakari mambo mengi kwa
kina: mahitaji ya sasa na baadaye ya Tanzania ya ndoto zangu, uwepo wa fursa ya
kugombea na kushinda uchaguzi ujao, uwezo wangu wa kuchambua mambo, kutafakari,
kufanya maamuzi sahihi, kuchukua hatua za utekelezaji na kusimamia utekelezaji,
uadilifu na uzalendo wangu, na zaidi nia yangu ya kuwa sehemu ya watanzania
wengi tunaotaka kuona mapinduzi ya kifikra katika nchi yetu – mapinduzi ambayo
yatatia chachu ya mabadiliko ya namna tunavyochagua vipaumbele vyetu kama Taifa
na namna tunavyosimamia utekelezaji wa mambo mazuri tunayojipangia kama Taifa.
Ninatangaza nia ya kugombea Urais nikiwapa fursa watanzania
wanipime na kunitazama mwenendo na uwezo wangu, nikiamini kabisa nitapimwa na
kuungwa mkono ama kutoungwa mkono si kwa rangi ya ngozi yangu, si kwa jinsi
yangu, si kwa umri wangu, na wala si kwa daraja langu kwenye jamii, dini yangu,
ama kabila langu. Ninaamini nitapimwa kwa sifa na uwezo wangu, kama mtanzania.
Watanzania tuna sifa moja kubwa; kwenye mambo ya msingi ya
kitaifa, tunakubaliana kuwa maslahi ya Tanzania hupanda juu ya maslahi yetu
binafsi. Tudumishe utanzania wetu.
Ninaamini katika Ndoto ya Tanzania. Kuwa leo miaka 50 ya kuwa
Jamhuri ya Tanzania tuna kila sababu ya kuwa Taifa la dunia ya kwanza, viongozi
waliotutangulia wameandaa misingi ya kuifikisha Tanzania kwenye matamanio yetu.
Kizazi chetu cha kina jukumu na wajibu wa kuikimbiza Tanzania kufikia kwenye
ahadi inayotokana na ndoto za wazee na waasisi wa Taifa letu. Binafsi, niko
tayari kulibeba jukumu hilo bila woga wala wasiwasi, maana naamini
tusipojitokeza watu kama mimi, tutajikuta tunaongozwa na watu wasiostahili.
Nina suluhu ya changamoto kubwa za leo na kesho: kupigana na
njaa na kuhakikisha usalama wa chakula kwa watu wetu, tatizo la ajira kwa
vijana na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi ni miongoni mwa mambo ambayo
kizazi chetu kitapaswa kuyafanyia kazi kwa haraka na umakini wa hali ya juu.
Mimi ninaamini kwamba, kama hata mimi nimefika hapa, basi kila
mtanzania anaweza, na ana haki ya kufika hapa na kwenda mbele zaidi yangu.
Mafanikio siyo haki ya wachache, ni tunu ya Mwenyezimungu kwa kila mtu.
Ninaamini ni haki ya kila mtanzania kuota ndoto yake, kuifanyia kazi na
kuifikia. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina wajibu wa kutoa fursa kwa watu
wake kuota ndoto zao na kufikia mafanikio bila kukwama.
Na ndugu watanzania wenzangu, amini nawaambia, kuwa, mbele yetu
tuna kazi ya ziada ya kufanya. Kazi ambayo ninaamini tunaiweza tukiamua; uwezo
tunao, sababu tunazo na nia tunayo – sema tuna mapungufu makubwa kwenye
kuchukua hatua za kutenda.
Mimi naamini kwamba; E Pluribus unum. Baina ya wengi,
mmoja!
Kwamba; Mimi ni mmoja kati ya uwingi wetu. Siwezi kuwa salama
kama wengine hawako salama, siwezi kuwa na raha kama wengine wanateseka.
Ninaongozwa na ile dhana kwamba, matatizo ya mwenzangu, ni ya kwangu, na si
yangu peke yangu, ni yetu sote kama jamii moja.
Hivyo:
- kitisho cha njaa ya familia fulani maskini kule Sakasaka,
wilayani Meatu, ni kitisho changu na familia yangu, hata kama siyo familia
yangu.
- Kucheleweshewa haki ya kuhukumiwa kwa mtuhumiwa wa mauaji ya
kule Sombetini, ni kitisho kwangu pia, hata kama kesi siyo yangu.
- Mzee Makame wa kule Wete, Pemba, aliyefiwa na watoto wake
akakosa msaada na yeye hana nguvu za kuzalisha tena, anavyokula mlo mmoja kwa
siku ili asukume siku, inaniumiza na kunigusa moyoni, hata kama yeye siyo babu
yangu.
- Mama John ni mpishi mzuri wa wali nazi kwa maharage, na ana
wateja wengi mtaani kwake maeneo ya Mtaa wa Sikukuu, Sokoni Kariakoo;
akifukuzwa, akapigwa virungu, akanyang’anywa pesa zake, akadhalilishwa na
kumwagiwa chakula chake na mgambo wa jiji la Dar es salaam kwa kuwa anafanya
biashara mahala pasiporuhusiwa, inaniumiza na kunigusa moyoni, hata kama yeye
si mama yangu.
- Kama kuna mtoto asiyejua kusoma na kuandika kule Mrijo Chini
kwa watani zangu warangi, hiyo inaniuma na kunigusa sana moyoni, hata kama yeye
si mwanangu.
- Bwana Kalumanzila ni mmachinga nguo za mitumba mitaani. Yeye
huchukua nguo zake kumi kwa kuaminiwa na mwenye belo kutokea soko la Karume,
akiuza anachukua kifaida kidogo cha juu kinachozidi hapo juu na kurudisha pesa
ya mwenye mali Karume jioni ya siku hiyo. Elfu mbili ama tatu anayopata
inamfanya aishi yeye na mkewe na watoto wake. Akifukuzwa barabarani na
akanyang’anywa mali, anakosa kazi ya kufanya na analazimika kumtumikia bosi
mwenye mali mpaka atakapofidia mali iliyopotea bila kupata cha juu. Shida na
madhila anayoyapata bwana Kalumanzila zinaniumiza na kunigusa sana moyoni, hata
kama yeye si mjomba wangu.
Tarehe 4, Agosti 2014, Rais Kikwete akihutubia kwenye Kituo cha
kimataifa cha maendeleo (Center for Global Development) alisema: “…Nataka na
natamani kuwa Rais wa mwisho wa Tanzania kuongoza nchi masikini. Raslimali ya
gesi inatoa nafasi na fursa kubwa kwa nchi yetu kuondokana na umasikini. Mimi
nimeongoza nchi masikini, lakini nataka mrithi wangu kuongoza nchi yenye ustawi
na utajiri…” Mimi nasema hivi: nataka na natamani kuwa Rais wa kwanza wa
Tanzania kuongoza nchi Tajiri. Kama nitafanikiwa kuwa Rais, nitatumia miaka ya
awali ya uongozi wangu kuikimbiza Tanzania kuelekea kwenye ndoto hii.
Mungu awabariki. Mungu ibariki Tanzania. Mungu ibariki Afrika.
No comments:
Post a Comment