Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na Sensa ya Watu na Makazi wa Ofisi
ya Taifa ya Takwimu Bw. Ephraimu Kwesigabo akitoa taarifa ya mfumuko wa bei kwa
mwezi Julai 2014 kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na. Aron Msigwa-MAELEZO.
Dar es salaam.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu imeeleza kuwa ongezeko dogo la mfumuko wa bei nchini kutoka asilimia 6.4
za mwezi June hadi asilimia 6.5 za mwezi Julai 2014 linatokana na kupanda kwa
bei za baadhi ya bidhaa na huduma katika maeneo mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa
habari leo jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na sensa ya Watu
na Makazi Bw. Ephraim Kwesigabo amesema kuwa bidhaa zisizo za vyakula zikiwemo
Bia, Sigara, mavazi kwa wanaume na yale ya watoto zimechangia ongezeko hilo.
Aidha, huduma na bidhaa nyingine zilizochangia ongezeko hilo ni
gharama za udobi, kodi za pango, mazulia na mkaa wa kupikia
Bw. Kwesigabo amefafanua
kuwa hali ya mfumuko wa bei za bidhaa za vyakula na migahawa kwa mwezi Julai
umepungua hadi 7.9 kutoka asilimia 8.5 kutoka asilimia 8.7 za mwezi Juni huku
badiliko la fahirisi za bidhaa zisizo za vyakula likiongezeka hadi asilimia 4.9
kwa mwezi Julai 2014 kutoka asilimia 4.8 iliyokuwepo mwezi uliopita.
Kuhusu mfumuko wa bei
unaopimwa kwa kipimo cha mwezi amesema kuwa umeongezeka kwa asilimia 0.1
ikilinganishwa na kupungua kwa asilimia 0.6 kama ilivyokuwa kwa mwezi Juni
mwaka huu, huku fahirisi za bei za taifa zikiongezeka hadi kufikia 149.16
kutoka 148.98 za mwezi Juni 2014.
Kwa upande wa uwezo wa
shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma za jamii kutoka mwezi
Septemba 2010 hadi Julai 2014 umefikia shilingi 67 na senti 04 kutoka shilingi
67 na senti 12 za mwezi Juni mwaka huu.
“Kuongezeka kwa bei ya baadhi ya bidhaa na huduma kwa mwezi uliopita kunamaanisha kwamba, uwezo wa fedha yetu katika kununua huduma na bidhaa hizo unaupungua hii inamaanisha mfumuko wa bei unapopanda thamani ya shilingi nayo inashuka” Amebainisha.
Kuhusu ulinganifu mfumuko wa bei wa Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki amesema kuwa una mwelekeo unaofanana na kueleza kuwa mfumuko wa bei nchini Kenya umeongezeka na kufikia asilimia 7.67 kwa mwezi Julai 2014 ikilinganishwa na asilimia 7.39 za mwezi Juni huku Uganda ikiwa na mfumuko wa bei wa asilimia 4.3 mwezi huu ikilinganishwa na asilimia 5.0 za mwezi Juni.
No comments:
Post a Comment