Na Benedict Liwenga,
Maelezo-Dodoma.
UMOJA wa Wabunge
Wanawake Tanzania (TWPG) kwa kushirikiana na Mtandao wa Wanawake na Katiba
wamezungumzia juu ya umuhimu wa uwepo wa masuala ya jinsia katika Katiba Mpya
na masuala muhimu ya jinsia ya kuzingatiwa katika katiba.
Wito huo umetolewa 30
Agosti, 2014 wakati wa Semina iliyoandaliwa na Umoja huo wakishirikiana na
Mtandao wa Wanawake na Katiba ili kutambua usawa na haki za wanawake ili kuleta
hali ya usawa kati ya wanaume na wanawake katika maamuzi, majukumu ya kazi,
umiliki wa rasilimali pamoja na haki zao kwa ujumla.
Akitoa mada wakati wa
semina hiyo, Mjumbe wa Mtandao wa Wanawake na Katiba Bi. Usu Mallya amesema
kuwa suala la msingi wa usawa wa kijinsia ni muhimu kuwekwa katika Katiba Mpya
na baadaye kuwepo na uwajibikaji wake kwani kwa kufanya hivyo kutaipatia nchi
katiba yenye mlengo wa kijinsia.
Bi. Mallya ameongeza
kuwa wanawake wengi nchini hawapati fursa ya usawa wa kijinsia katika nyanja
mbalimbali licha ya Tanzania kuwa kinara wa kutoa wanawake vinara ambao
wamewahi kushika nyazifa mbalimbali na wengine bado wakiendelea kushika nafasi
hizo za juu hapa nchini.
“Utafiti unaonyesha
kuwa, asilimia 5% ya wanawake nchini ndiyo wanaomiliki ardhi, asilimia 39% ya
wanawake hao hao hawapati elimu, pia utafiti unaonyesha kuwa asilimia 40.3% ya
wanawake walioko kwenye ajira wapo katika sekta isiyo rasmi, wakati asilimia 10%
ya Maprofesa wanawake ndiyo tunayo hapa nchini”. Alisema Bi. Mallya
Aidha, Bi. Mallya
amezitaja changamoto mbalimbali wanazokabiliana na wanawake wengi nchini
kuhusiana na usawa wa kijinsia na haki zao pamoja na haki za watoto huku akitoa
taarifa za utafiti zinazoonyesha kuwa mzigo wa kazi wa asilimia 66% ya wanawake
wanafanya kazi zisizo na kipato na asilimia 44% ya wanawake walioolewa katika
ndoa zao wamefanyiwa ukatili wa kijinsia.
Naye Mwenyekiti wa Women
Fund Tanzania ambaye pia ni Mjumbe wa Mtandao wa Wanawake na Katiba, Profesa
Ruth Meena amezungumzia juu ya masuala ya umuhimu wa jinsia ya kuzingatiwa
katika Katiba Mpya huku akisisitiza juu ya usawa wa uongozi katika ngazi zote
uwe hamsini kwa hamsini na uwepo wa chombo maalum kitakachozingatia haki za
wanawake.
Profesa Meena ameongeza
kuwa kuna umuhimu wa Katiba Mpya iweze kulinda haki za watoto kwa kutoruhusu
ndoa za utotoni, hivyo kuwekwe sheria zitakazo mlinda mtoto dhidi ya ndoa hizo
mpaka mtoto anapotimiza umri wa miaka (18) kumi na nane.
“Suala la umri wa mtoto
wa kike kuolewa iwe ni miaka kumi na nane, na mtu atakayeoa mtoto chini ya
miaka kumi na nane awe amebaka”. alishauri Profesa Meena.
Aidha, Profesa Meena
amegusia kuhusiana na suala zima la haki ya uzazi salama kwa wanawake pindi
wanapojifungua liweze kupewa kipaumbele kwa kujali usalama wa maisha ya mama na
mtoto na suala hilo, lisiwe hukumu ya kifo kwao.
“Iwe ni haki yetu ya
uhai tunapofanya kazi ya kuongeza kizazi cha Tanzania, wanawake wapewe usalama
wa uzazi wanapozaa pasipokuwa na kugugumizi, hivyo kuzaa kusiwe hukumu ya kifo
kwa watoto wetu”. alisema Profesa Meena.
Kwa upande wake Makamu
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewatia moyo
wanawake kwa kuwa na umoja wa kudai haki zao za usawa wa jinsia na amesisitiza
juu ya ushirikiano kati ya wanaume na wanawake katika jamii.
Mhe. Samia, amewaasa
wanaume wasiwe na tabia ya kuwadharau wanawake katika masuala mbalimbali
yakiwemo uongozi ama kuwapa talaka pindi wanawake wapatapo fursa ya uongozi.
Naye Waziri wa Maendeleo
ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mhe. Sophia Simba ameitaka jamii kuwekea mkazo
suala la elimu ya uzazi ianze kutolewa kuanzia elimu ya msingi ili watoto
waweze kuwa na uelewa wa kutosha pindi wanapokuwa na ametoa msisitizo juu ya
usawa kati wanawake na wanaume wa hamsini kwa hamsini katika masuala yote
katika jamii.
Shirika la UN Women
ndilo mwezeshaji wa Semina hiyo kwaajili ya Umoja wa Wabunge Wanawake Tanzania
na Mtandao wa Wanawake na Katiba kwa ajili ya Wajumbe wa Bunge Maalum kuhusu
masuala ya jinsia na Katiba, ambapo ni mara ya kwanza kwa semina kama hii
kufanyika nchini Tanzania jambo ambalo limewavutia wajumbe wengi waliohudhuria
wakiwemo wanaume na wanawake.
No comments:
Post a Comment