Tangazo

September 22, 2014

Zaidi ya wasichana milioni 58 Duniani wameolewa wakiwa na umri wa chini ya miaka 18

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akihutubia mkutano wa masuala ya elimu kwa vijana wa bara la Afrika ili waweze kufanya maamuzi sahihi ya kiafya. Mkutano huo  umeandaliwa na serikali ya Ujerumani na ulifanyika huko New York tarehe 22.9.2014. PICHA/JOHN LUKUWI
Na Anna Nkinda – Maelezo, New York

ZAIDI ya wasichana milioni 58 Duniani wameolewa wakiwa na  umri wa chini ya  miaka 18  kati ya hao milioni 15 wana umri wa kati ya miaka 10 hadi 14 jambo linalowasababisha kupata maambukizi ya Ugonjwa wa Ukimwi na kufanyiwa ukatili wa kijinsia.

Kwa upande wa Tanzania takwimu zinaonyesha kuwa wasichana wanajihusisha mapema zaidi katika mapenzi ukilinganisha na watoto wa kiume kwani asilimia 13 ya wasichana wanaanza kufanya mapenzi wakiwa na umri wa chini ya miaka 15 wakati kwa upande wa wavulana ni asilimia saba.

Hayo yamesemwa leo na Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Mama Salma Kikwete wakati akifungua mkutano uliojadili elimu ya afya ya uzazi na jinsia kwa vijana ulioandaliwa na Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Ujerumani Gerd Mueller na kufanyika katika ofisi za ubalozi wa nchi hiyo uliopo mjini New York nchini Marekani.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kutokana na kitendo cha wasichana kujihusisha na mapenzi wakiwa na umri mdogo wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la mimba za utotoni na hivyo wengi wao kushindwa kupata elimu.

“Nchini Tanzania kati ya msichana mmoja hadi wanne wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 19 wana mimba  au watoto , takwimu hizi ni kubwa zaidi katika nchi zingine za kanda ya Afrika ya Mashariki na Kusini”.

Idadi hii inaonyesha wasichana wataendelea kuwa kundi lililoathirika kwa kukosa haki zao za kupata afya, watakabiliana na unyanyasaji na maisha yao yataisha mapema. Tukichukua hatua ya kuwasaidia sasa tutaokoa  wasichana wengi na kuwasaidia kuwa na maisha mazuri hapo baadaye”, alisema Mama Kikwete.

Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema vijana wa Afrika wanatakiwa kupewa elimu ya maisha, afya ya uzazi na usawa wa jinsia ambayo itaendana na mila na desturi zao ili waweze kuwa na uchaguzi mzuri wa maisha yao kwani theluthi ya idadi ya watu wanaoishi nchi zilizopo Kusini mwa jangwa la Sahara ni vijana wa kati ya miaka 20 na 24.

Mama Kikwete alisema, “Afrika ya baadaye na ukubwa wa Dunia inategemea na jinsi tutakavyowaandaa vijana kujenga maisha yao ya baadaye. Hii itawezekana kama tutawasaidia kuchagua njia nzuri kuhusu afya yao na kuwaokoa kutoka katika tabia hatarishi”. 

Kutimiza hili tunahitaji kuwa na elimu bora ili mambo ya afya ya uzazi na stadi za maisha yapewe kipaumbele na uangalizi mkubwa unatakiwa kwa watoto wa kike”.

Akiwakaribisha wadau wa elimu na afya waliohudhuria mkutano huo Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Ujerumani Gerd Mueller alisema kwa zaidi ya miaka 20 Serikali yake imekuwa ikifanya kazi ya kuhakikisha vifo vya kina mama wajawazito na watoto vinapungua na upatikanaji wa huduma ya uzazi wa mpango inaimarika.

“Jambo la ziada linatakiwa kufanyika hasa katika Bara la Afrika lenye matumaini tutaongeza ushirikiano tukilenga zaidi katika elimu hasa elimu ya ufundi kwa wasichana na wavulana”.

Tunahitaji kufanya jambo la ziada kama tunataka kufanikiwa katika afya na elimu kwa vijana hasa wasichana. Wasichana wengi wenye umri wa chini ya miaka 18 katika nchi zinazoendelea wanapata mimba zinazowaletea matatizo yanayopelekea vifo vyao”, alisema Mueller.

Alisema Serikali ya Ujerumani itatoa fedha zingine Euro milioni 3 kwa ajili ya na kuandaa programu za pamoja ambazo zitaongeza elimu ya afya ya  ujinsia na huduma za afya ya uzazi kwa vijana katika nchi za ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kusini.

Akichangia mada katika mkutano huo Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupamba na Ukimwi (UNAIDS)  Prof. Sheila Tlou alisema vijana wanahitaji kupata elimu ya afya ya uzazi na jinsia ili waweze kujikinga na ndoa za utotoni na Ugonjwa wa Ukimwi.

Takwimu zinaonyesha kwa kila saa moja kuna maambukizi mapya 50 ya HIV kwa vijana hii ina maana kuwa kwa mwaka kuna maambukizi mapya 430000. Kwa sasa kuna vijana milioni 2.6 wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Prof. Tlou alisema mwaka mmoja umepita tangu  Mawaziri wa Afya na Elimu kutoka nchi 21 za Mashariki na Kusini mwa Afrika wakubaliane maazimio ya kuongoza juhudi za kuandaa mazingira salama na wezeshi kwa makuzi ya vijana katika nchi zao.

“Ni muhimu kuyafanyia kazi maazimio hayo ambayo yatawasaidia  vijana kupata elimu kuhusiana na afya ya uzazi na jinsia jambo ambalo litawasaidia  kufahamu zaidi ugonjwa Ukimwi”, alisema Prof. Tlou.

Mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na Mke wa Rais wa Malawi Gertrude Mutharika ni moja ya maandalizi ya Mkutano wa  69 wa Umoja wa Mataifa (UN) utaofanyika hivi karibuni mjini humo.

Mwisho.

No comments: