MAKATIBU WAKUU/ MA-RAS
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amefanya uteuzi
wa Makatibu Wakuu wa Wizara kwa kuteua Makatibu Wakuu wanne wapya na kuhamisha
mmoja.
Aidha,
Rais Kikwete amefanya uteuzi na uhamisho wa Makatibu Tawala wa Mikoa.
Taarifa
iliyotolewa mjini Dodoma jioni ya leo, Jumatano, Novemba 5, 2014 na Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue imesema kuwa walioteuliwa kuwa Makatibu Wakuu ni
Dkt. Donan Mmbando ambaye anakuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii, Dkt. Yohana Budeba ambaye anakuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Mifugo
na Uvuvi, Mhandisi Mbogo Futakamba kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Dkt.
Adelhelm James Meru ambaye anakuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Utalii na
Maliasili.
Kabla
ya uteuzi wake, Dkt Mmbando alikuwa Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Budeba
alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Uvuvi na Mifugo, Mhandisi
Futakamba alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji na Dkt. Meru alikuwa
Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA).
Aidha,
taarifa hiyo imesema kuwa Rais Kikwete amemhamisha Bibi Maimuna Tarishi kutoka
Wizara ya Maliasili na Utalii kwenda kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na
Sheria.
Kuhusu
uteuzi na uhamisho wa Makatibu Tawala wa Mikoa, Rais Kikwete amemteua Bw.
Charles Pallangyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuwa Katibu
Tawala wa Mkoa wa Geita, Bw. Adoh Steven Mapunda, Mkurugenzi Mtendaji, Manispaa
ya Bukoba kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Bw. Severine Kahitwa, Katibu
Tawala wa Mkoa wa Geita kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro na Dkt.
Faisal Issa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa
Mwanza.
Wakati
huo huo, Rais Kikwete amemteua Kanali (Mst) Joseph Simbakalia, Mkuu wa Mkoa wa
Mtwara, kuwa Mkurugenzi Mkuu wa EPZA.
Uteuzi
huo unaanza leo na Makatibu Wakuu na Makatibu Tawala wa Mikoa wataapishwa
kesho, Alhamisi, Novemba 6, 2014, Ikulu, Dar es Salaam.
Mwisho.
Imetolewa na;
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es
Salaam.
05
Novemba,2014
XXXXXXXXXXXXXXX
WAKUU WA MIKOA/WILAYA
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amefanya uteuzi
wa wakuu wapya wanne wa Mikoa, amewahamisha wengine sita na ameamua kuwa wengine
watatu watapangiwa kazi nyingine.
Taarifa
iliyotolewa mjini Dodoma jioni ya leo, Jumatano, Novemba 5, 2014 na Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue inasema kuwa, Wakuu wapya wa Mikoa ni Bi. Halima
Omari Dendego ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dkt. Ibrahim Hamisi Msengi
ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Bi. Amina Juma Masenza ambaye anakuwa
Mkuu wa Mkoa wa Iringa na Bwana John Vianney Mongella ambaye anakuwa Mkuu wa
Mkoa wa Kagera.
Taarifa
inasema kuwa kabla ya uteuzi wake Bi. Dendego alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Tanga,
Dkt. Msengi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya
Moshi, Bi. Masenza alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilemela na Bwana Mongella alikuwa
Mkuu wa Wilaya ya Arusha.
Taarifa
hiyo inasema kuwa Wakuu hao wapya wa Mikoa wataapishwa kesho, Alhamisi, Novemba
6, 2014 saa saba mchana, Ikulu, Dar es Salaam.
Aidha,
taarifa hiyo imesema kuwa Wakuu wa Mikoa ambao watapangiwa kazi nyingine ni
Kanali (Mst) Fabian Massawe wa Kagera, Dkt. Christine Ishengoma wa Iringa na
Kanali Joseph Simbakalia wa Mtwara.
Wakuu
wa Mikoa ambao wamehamishwa vituo vya kazi ni Bwana Magesa S. Mulongo ambaye
anakwenda Mkoa wa Mwanza kutoka Arusha, Dkt. Rehema Nchimbi ambaye anakwenda
Mkoa wa Njombe kutoka Dodoma, Bwana Ludovick John Mwananzila anakwenda Tabora
kutoka Lindi, Kepteni (Mst) Anseri Msangi anayekwenda Mkoa wa Mara kutoka
Njombe na Mhandisi Everist Ndikilo ambaye anakwenda Arusha kutoka Mwanza.
Wengine
waliohamishwa ni Luteni (Mst) Chiku A.S. Galawa ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma kutoka Tanga, Dkt. Rajab Rutengwe ambaye anakwenda Mkoa wa Tanga kutoka
Katavi, Bi Fatma Mwasa ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita kutoka Tabora na
Bwana Magalula S. Magalula ambaye anahamishiwa Lindi kutoka Geita.
Taarifa
hiyo imesema kuwa Wakuu wa Mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma, Kilimanjaro,
Manyara, Mbeya,Morogoro, Pwani, Rukwa, Shinyanga, Ruvuma, Singida na Simiyu
watabakia kwenye vituo vyao vya sasa.
Aidha,
Rais Kikwete amefanya uteuzi wa Wakuu wapya wa Wilaya, kuhamisha baadhi yao na
kutengua uteuzi wa baadhi. Taarifa kamili itatolewa na Waziri Mkuu baada ya
kuwa wamepangiwa vituo vya kazi.
Mwisho.
Imetolewa na;
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es
Salaam.
05
Novemba,2014
No comments:
Post a Comment