Tangazo

December 1, 2014

UNESCO WAANZISHA PROGRAM YA UTAMADUNI KUKABILI UKIMWI

DSC_0202
Afisa Ardhi na Mazingira wa Halmashauri ya wilaya ya Msalala (Kahama), Zablon Donge, akifungua rasmi warsha ya siku tatu ya wadau wa mapambano dhidi ya UKIMWI kwa niaba ya Mkurugenzi wa wilaya hiyo, iliyofanyika Kata ya Segese wilayani Kahama mkoani Shinyanga. Kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues pamoja na Afisa Mradi wa Elimu ya Afya na VVU/UKIMWI kutoka UNESCO, Bw. Herman Mathias.

Na Mwandishi Wetu, Kahama

MKURUGENZI Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues ametaka jamii kujumuisha suala la utamaduni katika kupambana na maambukizi mapya ya Ukimwi.

Alisema hayo kwenye warsha ya siku tatu ya wadau wa mapambano dhidi ya UKIMWI inayofanyika Kata ya Segese wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Alisema katika ufunguzi huo kwamba kwa miaka mingi pamoja na kuwepo kwa elimu ya UKIMWI, kumekosekana mabadiliko yanayotakiwa kukabili maambukizi mapya.

Alisema UNESCO iliangalia tatizo hili na kubaini kwamba kutobadilika kwa hali kumetokana na kutounganishwa kwa kipengele cha mila ambacho ndicho kinachofanya kuwepo na mazingira rafiki ya kupashana habari.
DSC_0151
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues akizungumza na washiriki wakati wa uzinduzi wa program ya utamaduni kukabili UKIMWI itakayoendeshwa na shirika lake.

Warsha hiyo ya Siku tatu imelenga katika kuhamasisha jamii, Shule, Asasi, Taasii za Dini na Serikali katika utoaji wa Elimu sahihi ya huduma rafiki za Afya ya Uzazi, VVU/UKIMWI, ujinsia na maadili ya Afya kwa vijana balehe na vijana.

Amesema mpaka sasa utoaji wa elimu ya afya, ueleweshaji wa ugonjwa haujafanya mabadilikoya kutosha kutokana na ukweli kuwa katika utekelezaji wa kampeni masuala ya utamaduni na uwasilishaji wa taarifa haukuwa umezingatiwa.

Alisema wakati Kahama (Msalala) kwa sasa kiwango cha maambukizi ni asilimia 5.9, Juhudi zinatakiwa kufanywa katika kuhakikisha kwamba elimu inayotolewa inahusishwa na masuala ya kitamaduni ili kubadilisha maisha ya wakazi.

Alisema katika mapambano ya maambukizi mapya mila na utamaduni zinaweza kabisa kusaidia kukabiliana na maambukizi ya UKIMWI.
DSC_0348
Afisa Mradi wa Elimu ya Afya na VVU/UKIMWI kutoka UNESCO, Bw. Herman Mathias akielezea madhumuni ya warsha hiyo ya siku tatu iliyojumuisha makundi mbalimbali ikiwemo Waganga wa jadi, wakunga wa jadi, viongozi wa dini, viongozi wa vijiji na kata, walimu, wataalamu wa afya na elimu na Asasi zisizokuwa za kiserikali.

Alisema program inayoangaliwa sasa ni ile iliyoleta mafanikio katika nchi kadhaa za Afrika ikiwamo Msumbiji na hivyo wanaona waijaribu Tanzania katika wilaya sita ikiwemo Kahama na hasa halmashauri ya wilaya ya Msalala.

Alisema pamoja na watu wengi kutibiwa na waganga wa kienyeji ni vyema watengeneza sera na watu wengine kutambua umuhimu wao ili kwa kupitia mila waweze kuwafunua watu akili na kujikinga na maambukizi ya UKIMWI.

Alisema anaamini kuwa mila na tamaduni zikitumika vyema na hata matibabu zitasaidia kuokoa maisha ya wengi na pia kuzuia maambukizi mapya.

Alisema maambukizi mapya ni tatizo kwa sasa hasa ikizingatiwa kwamba wananchi wengi wanajua uwapo wa UKIMWI lakini ufahamu ni mdogo kwa kuwa katika kufundisha watu hawakupewa elimu ya kutosha inayoambatana na kuangalia mila na desturi njema za afya zilizopo.
DSC_0366
Afisa afya mkuu kitengo cha elimu ya afya kwa umma-programu ya afya mashuleni kutoka Wizara ya afya na ustawi wa jamii, Avit Maro akielezea jambo kwa washiriki kuhusiana na masuala ya afya ya uzazi wakati wa warsha ya siku tatu ya wadau wa mapambano dhidi ya UKIMWI iliyofanyika Kata ya Segese wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Alisema ni vyema wananchi wakatumia mali asili waliyonayo kufundishana juu ya kukabiliana na maambukizi mapya ya UKIMWI.

Alisema UNESCO imeamua kuanzisha programu maalumu ya kutumia mila na desturi kukabili UKIMWI kama njia nyingine ya kuoanisha nguvu katika mapambano dhidi ya maambukizi mapya.
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Msalala (Kahama), Zablon Donge alishukuru UNESCO kwa kuanzisha program ya kujifunza namna ya kukabiliana na maambukizi mapya ya UKIMWI.

Alisema ukiwa na halmashauri ya wagonjwa huwezi kuwa na halmashauri kwa kuwa shughuli za kiuchumi na kijamii kushindikana kutekelezwa, na kusema kuja kwa UNESCO ni msaada mkubwa.

Warsha hiyo imejumisha makundi mbalimbali ikiwemo Waganga wa jadi, wakunga wa jadi, viongozi wa dini, viongozi wa vijiji na kata, walimu, wataalamu wa afya na elimu na Asasi zisizokuwa za kiserikali.
DSC_0384
Mkurugenzi msaidizi masuala mtambuka kutoka Wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi, Dkt. Laetitia Sayi akifafanua jambo jinsi wizara yake inavyoshirikisha jamii katika utoaji wa elimu mashuleni hususani afya ya uzazi, VVU/UKIMWI huku ikishirikiana na wadau wao wa karibu UNESCO.
DSC_0269
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues, akiendesha warsha hiyo kwa njia ya majadiliano na washiriki juu ya dhana na maana ya balehe, vijana balehe na vijana sambamba na maana ya mimba na ndoa za utotoni.
DSC_0368
Pichani juu na chini ni sehemu ya washiriki hao wakifuatilia majadiliano kwenye warsha hiyo ya siku tatu iliyofanyika Kata ya Segese wilayani Kahama mkoani Shinyanga.
DSC_0063
DSC_0257
Pichani juu na chini ni baadhi ya washiriki wakichangia maoni wakati majadiliano ya kutafuta suluhu ya kupunguza maambukizi mapya ya VVU/UKIMWI, mimba na ndoa za utotoni kwenye jamii zao.
DSC_0264
DSC_0096
Sehemu ya washiriki warsha hiyo kwenye vikundi kazi wakianisha na kubainisha matatizo yanayowakabili vijana balehe na vijana katika jamii zao huku wakiongozwa na Mkurugenzi msaidizi masuala mtambuka kutoka Wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi, Dkt Laetitia Sayi (kushoto).
DSC_0091
Mshiriki akiwasilisha kazi za vikundi baada ya majadiliano.
DSC_0061
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues akifafanua baadhi ya changamoto zilizoanishwa kwenye vikundi kazi na washiriki wakati wa warsha hiyo ya siku tatu.

No comments: