Tangazo

March 5, 2015

‘Harakati za IMETOSHA’ yaanzishwa kwa ajili ya kupambana na mauaji ya Albino


Balozi wa kujitolea wa harakati za kukomesha mauaji dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi maarufu kama Albino, Mwanahabari na Bloga Henry Mdimu (katikati), akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kuzindua  kampeni ijulikanayo kama ‘Harakati za IMETOSHA’, jijini Dar es Salaam Machi 05.2015. Kushoto ni Mwenyekiti wa Muda wa Mtandao wa Mabloga Tanzania (TBN) wadau wa harakati hizo, Joachim Mushi, Mjumbe wa Kamati, Monica Joseph (wa pili kushoto), Masoud Kipanya ambaye ni Mwanakamati (wa pili kulia) na Kelvina John. PICHA/JOHN BADI wa Daily Mitikasi Blog

Mwenyekiti wa Muda wa Mtandao wa Mabloga Tanzania (TBN) wadau wa kampeni hiyo, Joachim Mushi akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusu ushiriki wa bloggers katika harakati hizo. Kushoto ni Mratibu wa Habari wa Harakati za IMETOSHA, Salome Gregory.
XXXXXXXXXXXXXXXXXX

Na Mwandishi Wetu

MMOJA wa watu wenye ulemavu wa ngozi, albino na mwanahabari shupavu kutoka kampuni ya Mwananchi Communication, Henry Mdimu amejitolea kuwa balozi wa hiyari kupinga mauaji ya kikatili ya watu wenye albino yanaoendelea nchini.

Bw. Mdimu ambaye ameungwa mkono na baadhi ya marafiki na watu wanaokerwa na vitendo hivyo, ikiwemo Mtandao wa Mabloga nchini, Tanzania Bloggers Network (TBN) amesema ameamua kufanya hivyo baada ya kushuhudia ndugu zake wakiteseka kwa muda mrefu dhidi ya mauaji hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Balozi Mdimu amesema lengo lake kuu ni kuhakikisha anazunguka pamoja na marafiki watakao muunga mkono na kutoa elimu kwa kuanzia Kanda ya Ziwa ili tatizo hilo lisiendelee kuenea nchi nzima.

Akifafanua zaidi alisema mauaji ya watu wenye albino yanaichafua Tanzania hivyo atahakikisha anaisaidia Serikali kupambana na watu wenye imani hizo za kipuuzi ili kuondoa doa linaloichafua nchi yetu ambayo imekuwa na sifa ya amani dunia nzima.

"...Nimeamua kufanya hivi baada ya kushuhudia ndugu zangu wakiteseka kwa muda mrefu. Awali nilishindwa kuanzisha harakati hizi nikiamini kuna vyombo vinavyohusika na utetezi wa watu wenye ulemavu wa ngozi."

"...Hivyo nimeamua niweke jitihada zangu binafsi niisaidie Serikali yangu katika kuondoa doa hili linaloichafua Nchi yetu yenye sifa ya Amani duninia nzima. Hivyo nawaomba Watanzania wenzangu mniunge mkono tukishirikiana na Serikali ili mauaji haya yakome," alisema Mdimu.

"Kutokana na ushawishi nilionao kama Mwandishi, Mtangazaji wa redio na Blogger naamini nitaleta mabadiliko makubwa katika kuhakikisha haki ya kusihi kwa ndugu zangu inaheshimiwa na kubaki historia. Salamu zangu ziwafikie wanyanyasaji, wauaji na wenye kufanya dhihaka kwa watu wenye ulemavu wa ngozi kuwa IMETOSHA."

Akifafanua zaidi alisema kwa uchunguzi wake wa awali umebaini ukosefu wa elimu juu ya watu wenye ulemavu wa ngozi ndio chanzo cha tatizo hilo kukua na hatimaye kuuana kwa imani za kishirikina. "...Hivyo basi, silaha ya Elimu ni sehemu kubwa ya haraki hizi," alisisitiza Balozi huyo wa kujitolea.

Aidha alisema kuendesha harakati hizo alizozipa jina la 'IMETOSHA' elimu itatolewa kwa njia ya sanaa, na washauri nasaha pamoja na kundi la wanamuziki ambao pia wataandaa nyimbo mbalimbali za kutoa mafunzo ya kutokomeza ukatili huu.

Alisema wasanii ambao hadi sasa wamejitokeza kuunga mkono kampeni hizo ni paoma na Jhikoman, Kassim Mganga, Profesa J, Ray C, Fid Q, Roma Mkatoliki na Dami Msimamo.

Hata hivyo alisema bado pia anaamini nguvu ya vyombo vya habari ikiungana na kampeni hizo wanaweza kufanikiwa zaidi hivyo kuomba ushirikiano katika kuhakikisha vinapaza sauti kutokomeza mauaji hayo ya kikatili.


No comments: