![]() |
Mama Salma Kikwete |
Na Anna Nkinda – Maelezo,
Rufiji
Wanachama wa
vikundi vya kukopa na kuweka akiba wametakiwa kuwa na
uthubutu na kujiwekea malengo ya maendeleo kutokana na fedha wanazokopa kwa kufanya
hivyo wataweza kujikwamua kutoka maisha ya umaskini na kuongeza kipato cha
familia.
Rai hiyo imetolewa na
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati wa sherehe za kuadhimisha mwaka mmoja wa
kuanzishwa kwa vikundi vya mradi wa Mwanamke Mwezeshe unaoongozwa na Taasisi ya
Wanawake na Maendeleo (WAMA) zilizofanyika katika viwanja vya shule ya
Sekondari ya Zimbwini iliyopo Kibiti wilayani Rufiji mkoa wa Pwani.
Mama Kikwete ambaye ni
Mwenyekiti wa Taasisi hiyo alisema kupitia vikundi hivyo vya hisa wanawake wameweza
kukopa na kuweka akiba na kufanya mambo ya
maendeleo ikiwa ni pamoja na kulipa ada za watoto, kununua mashamba , viwanja,
kujenga nyumba na hivyo kuongeza thamani yao katika jamii kwani mwanamke akiwa na fedha mkononi hadhi yake inaongezeka lakini akiwa ombaomba hadhi
yake inapungua na kudharaulika na mme wake.
“Pamoja na jina la
mradi huu kuitwa mwanamke mwezeshe nawasihi wanaume msiogope kujiunga kwani
lengo la mradi ni kumkomboa mtanzania kutoka maisha ya umaskini pia vikundi
vilivyopo katika mfumo huu vimeweza kupata huduma ya bima ya afya kupitia mfuko
wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) hali kadhalika kupitia vikundi wanachama
ameweza kupewa mafunzo ya kuwaongezea ujuzi kupitia semina na maonesho”.
Muwe makini na
waaminifu kwani vikundi hivi ni nyenzo muhimu ya kuwakomboa. Msikubli
kuondolewa katika lengo lenu la msingi la kuinua hali zenu za maisha na
kutumiwa na watu wabaya kufanya mambo yaliyo kinyume, mkumbuke amani ya nchi
ikipotea waathirika wakubwa ni kina mama na watoto”, alisema Mama Kikwete.
Aidha Mwenyekiti huyo
wa Taasisi ya WAMA alisema huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu na kupiga kura ya
maoni na kuwataka wanavikundi hao
kuhakikisha wanajitokeza kujiandikisha
katika daftari la kudumu la wapiga kura ili waweze kushiriki katika zoezi la kura
za maoni na kuchagua katiba inayopendekezwa na mwishoni mwa mwaka huu kuchagua
rais, mbunge na diwani.
Mama Kikwete
alisisitiza, “Nawasihi ndugu zangu msiwasikilize watu watakaowashawishi
msijitokeze kujiandikisha au msiende kupiga kura ya maoni kuhusu katiba
inayopendekezwa. Na baya zaidi msikubali kufanya mambo yanayoweza kuvuruga
amani ya nchi, Historia inatufundisha kuwa kila palipoharibika amani
walioteseka zaidi ni wanawake na watoto”.
Kwa upande wake Mkuu wa
Mkoa wa Pwani Evarist Ndekilo aliishukuru Taasisi ya WAMA kwa kuwawezesha
wanawake katika mkoa huo kwani hivi sasa wanaweza kutoa michango mbalimbali ya
kifedha katika jamii zao bila ya kumtegemea mwanaume tofauti na ilivyokuwa miaka
ya nyuma.
Alisema kupitia
wataalam waliopo katika ofisi za Halmashauri za mkoa huo wakiwemo maafisa
maendeleo ya jamii watahakikisha wanavisaidia vikundi hivyo ili viwe endelevu.
“Wanachama wa vikundi
hivi nawaomba mshikamane na kushirikiana bila ya kufanya hivyo mradi huu hautakuwa
endelevu WAMA wamewapa nyavu nendeni mkavue samaki, ipandeni hii mbegu mliyopewa iweze kustawi zaidi na hivi vikundi viwe vya mfano ili
waliopo nje nao wajiunge”, alisema Ndekilo.
Akisoma risara ya
vikundi hivyo Arafa Ngwaya ambaye ni mwalimu wa vikundi vya hisa na Katibu wa
Umoja Ikwiriri alisema umoja huo umeanzishwa na vikundi vya hisa vipatavyo 51
venye wanachama 1643 kati ya hao wanaume 268 na wanawake 1375 ambavyo
vimemaliza mzunguko wa mwaka wa kwanza na kugawana hisa ya shilingi 492,422,947/=.
Alisema madhumuni ya
umoja huo ni kuviunganisha vikundi vya hisa wilaya ya Rufiji ili umoja uweze
kusimama na kuleta ufanisi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya ujasiriamali na ya
utunzaji wa kumbukumbu za fedha kwa wanachama wake na kutatua changamoto
mbalimbali zinazowakabili katika biashara zao.
Kutafuta vyanzo
mbalimbali vya mapato ikiwemo michango ya wanavikundi na wanahisa na mikopo
kutoka taasisi mbalimbali za kifedha ili kuweza kuvikopesha vikundi vya
wanachama.
“Changamoto
zinazotukabili ni hakuna vifa vya kutosha vya kuendesha ofisi vifaa hivyo ni
samani za ofisi na Computer, tunahitaji msaada wa kitaalam ili tuweze kufungua
benki yetu kwani tunahakika malengo yetu yakitimia na changamoto hizi kutatuliwa
tutakuwa tumepunguza suala la umaskini kwa kiasi kikubwa kama si kuondoa kabisa
katika wilaya yetu”, alisema Arafa.
Akiongea jinsi alivyoweza
kunufaika na mradi huo Fatuma Mbuzi
ambaye ni mkazi wa Ikwiriri anasema aliweka akiba na kukopa fedha za mkopo wa kwanza ambazo alizitumia
katika mradi wa kutengeneza batiki,
mkopo wa pili alinunua kiwanja na baada ya kumaliza mzunguko wa mwaka waligawana
hisa na kununua shamba.
Mradi wa Mwanamke
Mwezeshe ulianza kufanya shughuli za kijamii mwanzoni mwa mwaka jana katika wilaya
za Rufiji, Kilwa, Liwale, Lindi vijijini, Nachingwea kwa ufadhili wa Financial
Sector Deeping Trust (FSDT) unalenga kuanzisha vikundi 3000 vyenye jumla ya
wanavikundi 60,000 kwa kipindi cha miaka mitatu.
Hadi kufikia mwishoni
mwa mwaka jana mradi ulikwishaunda vikundi 1,047 na kuwafikia wanavikundi 26,710
kati ya hivyo vikundi 450 viko wilaya ya Rufiji na vina wanavikundi 10,499.
Mradi huo pia umetoa mafunzo ya kuweka akiba ambayo yatawawezesha wanavikundi
kuweka akiba za jumla ya shilingi bilioni moja na nusu, kufikia mwishoni mwa mwaka jana mradi
ulikusanya shilingi 1,518,643,430/= na hivyo kuvuka lengo la mwaka la kukusanya
akiba ya shilingi milioni 500.
No comments:
Post a Comment