Tangazo

April 2, 2015

KURA YA MAONI YA KATIBA INAYOPENDEKEZWA YAOTA 'MBAWA'

Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva
DAR ES SALAAM

Kama inavyofahamika, chini ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1997 na Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 ya mwaka 2010, jukumu la Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni kusimamia na kuendesha Uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani kwa Tanzania Bara. 

Aidha, Sheria ya Kura ya Maoni imezipa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Tume ya Uchaguzi Zanzibar jukumu la kuendesha Kura ya Maoni kwa ajili ya kuhalalisha Katiba Inayopendekezwa. Kwa mujibu wa Katiba na Sheria, Tume hizi huendesha shughuli zake kwa uhuru bila kuingiliwa na mamlaka nyingine yeyote. 

Ni jambo linaloeleweka kwamba, zoezi lolote la Uchaguzi huanzia na Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Wapiga Kura wote wenye sifa za Kikatiba na Kisheria ya Kupiga Kura ni lazima kwanza waandikishwe katika Daftari na kupata Kadi kama Kitambulisho kinacho thibitisha kuwa ameandikishwa na ndicho atakachotumia kujitambulisha siku ya kupiga kura. 

Hivyo, ni muhimu sana kuwa na Daftari la Wapiga Kura linaloaminika ili kuhakikisha kuwa wote wanaopiga kura kweli ni wale tu walioandikishwa. 

Kutokana na chaguzi zilizopita, za mwaka 2010, Chaguzi Ndogo za Igunga, Arumeru Mashariki, Kalenga na Chalinze, Daftari lililokuwa linatumika limekuwa lilalamikiwa Tume imelalamikiwa sana hivyo, linahitaji kuboreshwa. 

Hivyo, Tume ilifanya tafiti za kutosha katika nchi mbalimbali ikiwemo wenzetu wa Zanzibar na tuliridhika kwa dhati kuwa, Kuboresha Daftari kwa mfumo wa BVR unafaa. Hata hivyo, kwa Tanzania mfumo huo utatumika kwa Kuandikisha Wapiga Kura tu na siyo kwa shughuli nyingine za Mchakato wa Kupiga Kura. 

Kwa kuwa kazi ya kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni ya msingi kabla ya zoezi la Kupiga Kura, Tume wakati wote imesisitiza kuwa jukumu lake la kwanza ni kukamilisha kazi ya Kuboresha Daftari. Mengine yatafuata baada ya hapo.

Kama inavyofahamika, zoezi la Kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lilizinduliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu tarehe 24 Februari, 2015 katika Halmashauri ya Mji wa Makambako, Mkoani Njombe. Zoezi lilianza kwa kutumia vifaa 250 vya BVR vilivyokuwa vimefika nchini na ndivyo pia vilitumika wakati wa Zoezi la Majaribio katika maeneo ya Kawe Dar es Salaam, Kilombero Morogoro na Mlele Mkoani Katavi. 

Pamoja na changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika matumizi ya mfumo huu, kwa ujumla zoezi limeendelea vizuri. Mwitikio wa wananchi ni mkubwa sana. Kwa mfano katika maeneo fulani ya Kata mbili tumeongeza muda ili kumaliza Uandikishaji kwa wananchi waliojitokeza. 

Inatarajiwa kwamba, zoezi litakamilika Mkoani Njombe tarehe 18/04/2015. Hadi kipindi hiki kwa Kata ambazo Tume imeishapita, hakuna hata mtu mmoja aliyejitokeza Kituoni ambaye aliachwa kuandikishwa. 

Tume inawahakikishia wananchi kuwa wakati ambapo vifaa vingine vya BVR vinaendelea kupokelewa na Tume wanachi wote watakaojitokeza katika Mikoa mingine nchini wenye sifa wataandikishwa. Baada ya zoezi kukamilika Mkoani Njombe, kwa tarehe zitakazo ainishwa, Tume itaendelea na Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura katika Mikoa ya Ruvuma, iringa, Mtwara, na Lindi. 

Kama ilivyofanyika Mkoani Njombe ni tegemeo la Tume kuwa Mikoa inayofuata itawahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi katika maeneo yao na kujiandikisha kwa tarehe zitakazotangazwa kwenye Mikoa husika. Ni upotoshaji kwa wananchi kwamba mistari/foleni ni dalili ya ubovu wa mfumo wa BVR badala ya kuonyesha kwamba ndiyo kukolea kwa demokrasia nchini. 

Mara kwa mara, Tume imeulizwa itakuwaje kama tarehe 30 April, 2015 inakaribia na Tume haijakamilisha Uboreshaji wa Daftari. Wakati wote Tume imesema, ikitokea hivyo itawaarifu wananchi haijakamilisha Uboreshaji wa Daftari. Wakati wote Tume imesema, ikitokea hivyo itawaarifu wananchi kwa jumla hali itakavyokuwa.

Kwa muktadha huo leo tarehe 02/04/2015, Tume inapenda kuwaarifu wananchi kama ifuatavyo;

i. Kwa vile kazi ya Uboreshaji Daftari la Kudumu la Mpiga Kura ni ya msingi kabla ya Zoezi la Kupiga Kura na kutokana na uzoefu tuliopata Mkoani Njombe, Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura bado halijakamilika Mkoani Njombe na katika Mikoa mingine. 

ii. Kwa vile zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura halijakamilika, Tume haitaweza kuendelea na zoezi la upigaji wa kura ya maoni. 

Hivyo, kwa heshima na taadhima Tume inawaarifu kuwa Zoezi lililotangazwa awali la Kura ya Maoni kufanyika tarehe 30 Aprili, 2015 limeahirishwa hadi tarehe itakapotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi baada ya kushauriana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar.

No comments: