Tangazo

April 3, 2015

MKUTANO MKUU WA 31, TUZO ZA VIONGOZI WA SERIKALI ZA MITAA (MAYORS AWARD) NA MIAKA 30 YA ALAT KUFANYIKA APRILI 8-11, 2015JIJINI DAR


Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) ambaye pia ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi (katikati), akizungumza na waandishi wa habari jijini jana kuhusu Mkutano Mkuu wa 31 wa ALAT utakaokwenda sambamba na Tuzo za Viongozi wa Serikali za Mitaa ‘Mayors Award’ na Miaka 30 ya ALAT, utakaofanyika katika hoteli ya Kunduchi jijijni Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu Mkuu wa ALAT, Habraham Shamumoyo na (kulia) ni Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya NMB ambao ndio wadhamini wakuu wa mkutano huo, Waziri Barnabas. PICHA NA JOHN BADI WA DAILY MITIKASI BLOG

Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya NMB, Waziri Barnabas (kushoto), akikabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 200, kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) ambaye pia ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi kwa ajili ya kudhamini mkutano huo. Katikati ni Katibu Mkuu wa ALAT, Habraham Shamumoyo


XXXXXXXXXXXXXXX 

Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) itafanya Mkutano wake Mkuu wa 31 katika hoteli ya Kunduchi jijijni Dar es Salaam. Kauli mbiu ya Mkutano huo unaodhaminiwa na benki ya NMB ni “Wananchi pigia kura katiba pendekezwa kuboresha Serikali za Mitaa na maendeleo endelevu baada ya mwaka 2015”“.

Mkutano mkuu wa 31 unafanyika pamoja na mambo makubwa mawili yafuatayo; Moja ni Sherehe za Miaka 30 ya Serikali za Mitaa na ALAT ambayo itakuwa na kongamano la kutathmini tulikotoka, tulipo na kuangalia nini cha kufanya huko mbeleni ili kuziwezesha Serikali za Mitaa kutoa huduma kwa ufanisi zaidi. Pili, shaerehe za tuzo za viongozi bora wa Serikali za Mitaa (Mayors Award). Kwa mara ya kwanza ALAT itatoa tuzo kwa viongozi wa Halmashauri ambao wanafanya vizuri katika kusimamia Halmashauri zao. Katika mchakato wa kuwapata viongozi bora wananchi wameshirikishwa kwa kutuma ujumbe mfupi kwa njia ya simu kwenda namba 15440. 

Kwa mwaka wa pili mfululizo, NMB wamekuwa wakidhamini mkutano wa ALAT na kwa mwaka huu, wametudhamini kwa shilingi milioni 200 ambapo milioni 150 ni kwaajili ya matayarisho ya mkutano na milioni 50 kwaajili ya ununuzi wa trekta ambalo litakabidhiwa kwa washindi wa tuzo ya uongozi bora wa Serikali za Mitaa (Mayors Award). Trekta hili tunaimani litasaidia shughuli mbalimbali za halmashauri iliyoshinda kama shughuli za ukandarasi ikiwemo utengenezaji wa barabara na urekebishaji wa miundombinu ndani ya halmashauri.


Mkutano wa mwaka huu una umuhimu wa pekee katika historia ya Serikali za Mitaa na taifa letu kwa jumla. Mwaka huu ni mwaka wa 31 tangu kurejesha mfumo wa Serikali za Mitaa hapa nchini mwaka 1984; pili Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania inaadhimisha miaka 31 tangu kuanzishwa kwake tarehe 13 Disemba 1984. Tatu mwaka huu nchi yetu inapitia kwenye mchakato wa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakayotuwekea misingi na kanununi za uendeshaji wa nchi yetu kwa miaka 50 ijayo ikiwa ni pamoja na kuweka mifumo ya Serikali za Mitaa itakayo jikita kwenye ugatuaji wa madaraka kupeleka kwa wananchi. 

Mkutano Mkuu wa kawaida wa Jumuiya hufanyika mara moja kila mwaka na wajumbe wake ni: Wenyeviti na Mameya 168 wa Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya, Wakurugenzi 168 wa Halmashauri, Wabunge 25 mmoja toka kila mkoa. Mkutano huu utahudhuriwa pia na Wizara, Idara za Serikali Kuu, Wakala za Serikali, Taasisi shiriki katika Serikali za Mitaa, wawakilishi wa Balozi na Wabia katika Maendeleo, Mashirika ya Kimataifa na Jumuiya za Serikali za Mitaa za Afrika Mashariki na wadau wangine wa sekta ya Serikali za Mitaa. 

Aidha Mkutano huu utahudhuriwa na Asasi zisizo za Kiserikali, Mashirika na Makampuni na Wawakilishi wa Sekta Binafsi.  Inatarajiwa kwamba Mkutano huu utahudhuriwa na Washiriki takribani mia tano (550). Mkutano Mkuu wa ALAT ndiyo chombo cha juu kabisa cha maamuzi cha Jumuiya. 

Maandalizi yote kwa ajili ya Mkutanop yamekamilika kwa asilimia 95 na kwa namna ya pekee Kabisa tumemwalika Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Mgeni Rasmi wa mkutano wetu Mkuu pamoja na kutoa tuzo za kwa Mameya/wnyeviti wa Halmashauri.

Niwashukuru wadau mbalimbali amabo wamejitokeza katika kufadhili na kusaidia Mkutano huu. Kwa namna ya pekee kabisa niwashukuru benki ya NMB kwa kuendelea kuwa mwenza (partner) katika Mkutano huu na tuzo za viongozi wa serikali za Mitaa. Niwashukuru pia PSPF, MABIBO BEER & WINE, MSD, NHC, NIDA, GF TRUCKS, PPF,TBA, TAA, LAPF, TSN, UTT.

Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania ni chombo kinachoziunganisha Halmashauri zote za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji Tanzania Bara. Kwa sasa kuna Halmashauri 168 zinazounganishwa na chombo hiki.

No comments: