Msimamizi wa Mnara
wa Airtel Tabora, Bw. Phidelis Lugangila (wa pili kushoto), akimwonyesha sehemu
za mnara, aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua, John Kadutu (kushoto),
baada ya uzinduzi wa mnara huo wa mawasiliano wa Airtel, utakaowawezesha wakazi
wa kijiji cha Kingwang’oko wilayani Uyankulu mkoani Tabora kupata mawasiliano
bora. Anayeshuhudia ni Diwani wa Kata ya Kona Nne, Bw. Japhael Lufungija na
Afisa Masoko wa Airtel Tabora, Godfrey Kigata.
XXXXXXXXXXXXXXXXXX
XXXXXXXXXXXXXXXXXX
TABORA
WAKAZI wa Kijiji cha Kigwang’oko Wilaya ya Ulyankulu,wameipongeza kampuni ya Airtel kwa kuwajengea mnara wa mawasiliano na hivyo kuondokana na tatizo sugu la mawasiliano lililokuwa likiwakabili.
Wakazi hao wamekuwa wakifanya shughuli zao bila ya mawasiliano ya uhakika kwa muda mrefu jambo linalotajwa kukwamisha shughuli nyingi za maendeleo kijijini hapo.
Wanakijiji hao wameeleza kuwa, wamekuwa wakipata tabu ya kufanya mawasiliano wakati mwingine wakilazimika kupanda kwenye miti au vichuguu kupata mawasliano kabla ya kujengwa kwa mnara huo.
“Tunawashukuru sana Airtel kwa kutukumbuka na kutuleta mnara huu ambao hapa kijijini kwetu ni mkombozi mkubwa katika sekta ya mawasiliano” walisema wananchi hao.
Akiongea na waandishi wa habari mkazi wa Kigwang’oko, Juma Magema alisema “Kabla ya Airtel kuweka mnara hapa kijiji kwetu tulikuwa tunapanda katika miti na hata vichuguu ili kupata mawasiliano, lakini sasa hatupati tena shida hiyo”.
Akiuzindua mnara huo,aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua, John Kadutu, amewataka wananchi kuutumia mnara kuboresha shughuli zao za kijamii na kiuchumi na kuboresha maendeleo ya kijijini hapo na jamii kwa ujumla.
“Muutumie mnara huu kujiletea maendeleo kwani hivi sasa mnaweza kutumia mawasiliano ya Airtel na huduma zote zinazoenda sambamba na uwepo wa mnara huo kijijini hapo” alisema Kadutu.
Awali meneja wa Airtel Mkoa wa Tabora,Fidelis Lugangira,alisema wamepeleka mnara huo ili kuboresha za kiuchumi ,lengo likiwa ni kuzidi kuwafanya wanufaike kwa kutumia mawasiliano.
“Mnara huu umejengwa kijijini hapa ikiwa ni hatua ya Kampuni yetu kusogeza karibu huduma za mawasiliano hivyo ni fursa ya kipekee kwenye kujiletea maendeleo” alisema Lugakingira.
Airtel imezindua huduma ya mawasiliano katika Kijiji cha Kigwang’oko Wilayani Ulyankulu mikoani Tabora mara baada ya kuzindua huduma kama hizo katika wilaya ya Ikungi mkoani Singida na katika kijiji cha Nduruma wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Mpango mkakati ni kufikia maeneo mengi zaidi husasani
yaliyoko pembezoni mwa nchi.
No comments:
Post a Comment