Kama mnavyofahamu Kampeni za Uchaguzi Mkuu
wa Rais, Wabunge na Madiwani zimeanza tangu tarehe 22 Agosti, 2015 na zinaendelea
hadi tarehe 24 Oktoba, 2015.
Ni jambo linaloeleweka kwamba mchakato wa
Kampeni na wa Upigaji Kura unatawaliwa au kuongozwa na Sheria, Katiba na
Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015.
Katika kipindi hiki tangu Kampeni zianze,
nafurahi kusema kwa niaba ya Tume kuwa kwa ujumla, Kampeni zimeenda
vizuri. Karibu mikutano yote imefanyika
katika hali ya utulivu na amani.
Hatujapata taarifa ya mkutano wa Kampeni ambao umevurugwa kwa fujo
zozote. Kwa hilo napongeza Vyama vyote
vya Siasa.
Hata hivyo, kutokana na mikutano hiyo
nchini ya Kampeni, ngazi ya Urais, Ubunge na Udiwani yamejitokeza mambo ambayo
ni kinyume kabisa na Mwongozo wa Maadili ya Uchaguzi wa Rais Wabunge na
Madiwani wa mwaka 2015 uliotiwa saini na Vyama vyote vya Siasa tarehe 27 Julai,
2015.
Yafuatayo ni baadhi ya mambo ambayo
yamejitokeza katika Kampeni hizo:-
(i)
Kutozingatia
muda wa kumaliza Mikutano ya Kampeni
Kuna baadhi ya Vyama ambavyo katika
mikutano yao vimekiuka Kipengele hiki kwa kufanya mikutano zaidi ya saa 12.00
jioni. Kuendelea kufanya Mkutano wa
Kampeni zaidi ya muda huo ni ukiukwaji wa Kipengele
cha 2.1 (c) cha Maadili ya Uchaguzi
wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015 kinafafanua kuwa Mikutano
yote ya Kampeni itafanyika kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 12.00 jioni.
(ii)
Kubandika
mabango ya Kampeni, matangazo au Mchoro wowote kwenye maeneo yasiyoruhusiwa au
bila idhini ya wahusika
Baadhi ya Vyama vimeanza kubandika mabango,
michoro na picha za Wagombea wao katika majengo au vyombo vya usafiri vya watu
binafsi au Taasisi mbalimbali bila idhini ya wamiliki husika.
Napenda kuwakumbusha kuwa, kwa mujibu wa Kipengele cha 2.2. (g) cha Maadili ya
Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015, hairuhusiwi kufanya hayo
bila idhini ya wamiliki husika.
(iii)
Kuchafua,
kubandua au kuharibu matangazo au picha za Kampeni za Vyama vingine
Tume imeanza kupokea malalamiko kutoka
baadhi ya Vyama kuwa, mabango au picha za Kampeni za Vyama vyao yanabanduliwa
au kuchafuliwa na wafuasi wa Vyama vingine.
Ni vema Vyama vya Siasa na Wagombea
wakumbuke kuwa Kipengele cha 2.2 (f)
cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015, kinapiga
marufuku Chama kingine kuchafua, kubandua au kuharibu matangazo au picha za
Kampeni za Vyama vingine.
(iv)
Matumizi
ya lugha zisizo za staha
Tume imepokea malalamiko kuwa, katika
Mikutano mbalimbali ya Kampeni katika ngazi zote, kumeanza kujitokeza baadhi ya
viongozi wa Vyama, Wagombea au wafuasi wao kutumia lugha zisizo za staha wakati
wa Mikutano ya Kampeni katika ngazi mbalimbali.
Lugha zisizo za staha zinajumuisha matusi,
kejeli, kashfa n.k. Kipengele cha 2.2 (b) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na
Madiwani ya mwaka 2015, kinakataza Viongozi wa Vyama vya Siasa na Wagombea wao
kutumia lugha zisizo za staha katika harakati zote za Kampeni hadi upigaji
Kura.
Wajibu
wa Vyama vya Siasa na Wagombea
Viongozi wa Vyama vya Siasa na Wagombea wana
wajibu wa Kisheria wa kuyaheshimu, kuyasimamia na kuyatekeleza Maadili hayo kwa
mujibu wa Kipengele cha 2.1. (b) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na
Madiwani ya mwaka 2015. Viongozi wa Vyama vya Siasa na Wagombea wana jukumu la kuwaelimisha,
kuwahamasisha na kuwasisitiza wanachama wao kutekeleza Sheria ya Uchaguzi
(ikumbukwe kuwa Maadili ya Uchaguzi yametungwa chini ya Kifungu cha 124A cha
Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343)
Adhabu
za ukiukwaji wa Maadili ya Uchaguzi
Napenda kuwakumbusha Vyama vya Siasa na
Wagombea kuwa, ukiukwaji wa aina yoyote wa Maadili unaweza kusababisha Chama au
mgombea kupewa adhabu kama zilivyoainishwa katika Kipengele cha 5.10 (a-f). Adhabu hizo ni pamoja na:
1.
Chama au Mgombea
aliyekiuka maadili kuelekezwa kuomba msamaha hadharani.
2.
Kupewa onyo au karipio.
3.
Kumtangaza kupitia vyombo
mbalimbali vya habari na taarifa kwa Umma mgombea au Chama kilichokiuka
Maadili.
4.
Chama au Mgombea
kusimamishwa kuendelea kufanya Kampeni.
5.
Chama au Mgombea kuzuiliwa
kutumia vyombo vya habari.
6.
Chama au Mgombea kulipa
faini kuanzia kiwango cha 100,000/- 500,000/- na 1,000,000/- kutegemea ngazi ya
Kamati husika.
Katika
kipindi hiki cha Kampeni, Chama au Mgombea akipewa mojawapo ya adhabu hiyo
kunaweza kuathiri Kampeni zake za kuelekea Uchaguzi wa Rais, Wabunge au
Madiwani.
Hitimisho.
Napenda
kunukuu Kipengele cha 1.4 cha
Maadili ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015 ili kila
Chama kione umuhimu wa kuwahimiza wagombea na wanachama wao kuzingatia Maadili
katika harakati zao za kujinadi. Nanukuu:
“[……]
kila mgombea atajaza Fomu Na. 10 kuthibitisha kuwa ataheshimu na kutekeleza
Maadili ya Uchaguzi. [….] Mgombea atakayekataa kusaini Maadili haya atakataliwa
au kuondolewa kushiriki katika Uchaguzi kama Mgombea.”
Maana yake ni kwamba kila Chama, Mgombea na
Wanachama kwa ujumla wana wajibu kuheshimu taratibu zote za Kampeni hadi kupiga
Kura.
Yote yaliyokatazwa katika Maadili
yazingatiwe na Vyama vyote. Kama
nilivyosema hapo awali Tume imepata malalamiko kuwa baadhi ya Vyama na Wagombea
wamekiuka Maadili ama kwa kuzidisha muda wa Kampeni, au kuchana na kuharibu
mabango, au kutumia lugha chafu isiyo na staha; Haya yote Tume inakemea kwa
nguvu sana na kusihi Vyama vyote na Wanachama wao wote kuheshimiana,
waeleze sera zao bila kukashifiana.
Lengo na matumaini ya Tume ni kuwa na
Kampeni za utulivu na hatimaye wananchi kuwa na hali ya utulivu na amani ili
Uchaguzi ufanyike kwa amani na utulivu.
Kwenye hali ya utulivu na amani wananchi wataweza kupiga Kura ya utulivu
ili kuamua viongozi wanaowataka. Hiyo
ndiyo Demokrasia.
Nimalizie kwa kuwakumbusha Vyama vyote
kuzingatia Maadili ya 2015. Tume
isilazimishwe kuchukua hatua za kutoaadhabu kwa Vyama na Wagombea. Busara itumike katika mikutano yote ya
Kampeni.
Inawezekana, wote
tukidhamiria, “Play your Part”.
Jaji (Mst.) Damian Z. Lubuva
MWENYEKITI
TUME YA
TAIFA YA UCHAGUZI
No comments:
Post a Comment