Tangazo

March 18, 2016

UAMUZI WA RAIS MAGUFULI KUTOA ELIMU BURE UTACHOCHEA USAWA WA KIJINSIA NCHINI – UMMY MWALIMU

Hayo yalisemwa na Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu (Mb.)wakati akitoa taarifa ya nchi katika Mkutano wa 60 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Hali ya Wanawake Duniani (CSW).

Mhe Ummy alieleza kuwa Adhma ya Mheshimiwa Dkt John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kutoa Elimu bure kwa shule za Msingi na Sekondari itakuwa na matokeo makubwa ya kuongeza udahili wa wanafunzi katika Elimu ya msingi, Sekondari na Elimu ya juu.

Akaongeza kwamba uimarishwaji wa upatikananaji wa elimu kwa wanawake ni msingi mkubwa wa kuwezesha wanawake kiuchumi, kwakuwa elimu hutoa ujuzi, maarifa na hali ya kujiamini kwa wanawake kuendea fursa za kiuchumi.
Ummy Mwalimu -CSW
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ( Mb) akizungumza wakati wa majadiliano kuhusu dhima ya uwezeshwaji wa wanawake na uhusiano wake na utekelezaji wa Agenda 2030. katika mchango wake Waziri anayeongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huu wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Wanawake amesema Serikali inatambua umuhimu wa mwanamke katika utekelezaji wa ajenda mpya ya maendeleo endelevu ( Agenda 2030) na kwamba itaendelea kumwezesha.

Katika Taarifa hiyo, Mheshimiwa Waziri, alieleza kuwa Serikali ya Tanzania inatambua kuwa uwezeshaji wa wanawake na Usawa wa jinsia unachangia kwa kiasi kikubwa kufikiwa kwa wepesi kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu ( Sustainable Development Goals).

 Kwa kutambua hilo Tanzania imejipanga kuhuisha Ajenda 2030 katika Sera, Sheria na Mipango ya nchi kwa kuhakikisha kunakuwa wa sheria zinazolenga kuleta Usawa wa Jinsia na uwezeshaji wa wanawake, ambapo pamoja na mambo mengine utekelezaji wa Mikakati, Sera na Sheria utaendelea kuzingatia haki ya kielimu kwa Wanawake na Wasichana.

Mheshimiwa Ummy, aliongelea pia umuhimu wa Afya kwa wanawake na Wasichana (ikiwa ni pamoja kupunguza vifo vya wajawazito na watoto) kama njia ya kumuwezesha mwanamke kushiriki kikamilifu katika uzalishaji mali.

Mkutano huo wa wiki mbili unafanyika NewYork, Marekani kuanzia tarehe 14-24 Machi 2016, ukihusisha wawakilishi kutoka serikali mbalimbali duniani na Asasi za Kiraia ambapo hujadiliana na kubadilishana uzoefu na kuelimishana kuhusu hatua mbalimbali ambazo Serikali zao zinachukua katika kuboresha maisha ya mwanamke na mtoto wa kike.
Ummy Mwalimu - CSW
Mheshimiwa Ummy Mwalimu akiwa pamoja na Mhe. Balozi Tuvako Manongi na Mhe Peter Serukamba (Mb.), mara baada ya kuwasilisha taarifa ya Tanzania kuhusu Masuala ya Maendeleo ya Wanawake.

No comments: