Tangazo

September 21, 2016

Watanzania watakiwa kutunza mazingira ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza


Na Rabi Hume, MO BLOG

Kutokana na kuwepo na shughuli nyingi za kibinadamu ambazo zinaharibu mazingira, watanzania nchini kote wametakiwa kuwa makini kwa kutunza mazingira yanayowazunguka ili kuepusha matatizo ambayo yanaweza kutokea kutokana na kushindwa kudhibiti vitendo vya uharibifu mazingira.

Rai hio imetolewa na Balozi Mwakilishi wa Mashirika ya Kimataifa Geneva, Uswisi, Modest Mero katika warsha ya kujadili kuhusu kilimo na biashara iliyoandaliwa na Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF).

Balozi Mero alisema kuwa nchi nyingi duniani zimekuwa na shughuli nyingi ambazo zinaharibu mazingira hali ambayo inatishia maisha ya vizazi vijavyo na hivyo ni vyema watanzania wakaanza kuchukua hatua kwa kutunza mazingira ili kuepeusha athari ambazo zitajitokeza kwa miaka ijayo.

"Dunia nzima watu wanakata miti, wanachoma majani mashambani lakini hawajui kama kuna vitu vya muhimu wanaua ardhini, na mimi niwambie watanzania wawe makini wasikate miti ambayo inawazunguka huo ni uharibifu wa mazingira," alisema Balozi Mero.
Balozi Mwakilishi wa Mashirika ya Kimataifa Geneva, Uswisi, Modest Mero akizungumza na washiriki wa warsha iliyoandaliwa na Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF), ikizungumza kuhusu kilimo na biashara. (Picha zote na Rabi Hume - MO BLOG)

Aidha alisema kuwa kwa sehemu kubwa watu ambao wanachangia vitendo hivyo ni wafanyabiashara na hivyo kuwataka wafanyabiashara kuacha vitendo vya kukata miti ikiwa bado haijafika katika muda sahihi ambao wanaruhusiwa kuikata.

"Wafanyabiashara wanakata sana miti, lakini wajue kuwa wakikata hovyo baadae wataikosa hiyo miti, ili mazingira yanayotuzunguka yawe mazuri inabidi kuyatunza ila tukitumia vibaya hata vyanzo vya maji vitakauka," alisema Mero.
Mtafiti Mshiriki wa ESRF, Dkt. Osward Mashindano akizungumzia malengo ya warsha hiyo.

Nae Mtafiti Mshiriki wa ESRF, Dkt. Osward Mashindano alisema warsha hiyo ina lengo la kuzungumzia jinsi gani kilimo, biashara, usalama wa chakula na mabadiliko ya hali ya nchi jinsi ambavyo vinaweza kutoa matokeo mazuri au mabaya.

Alisema kuwa pamoja na matokeo hayo, pia wanazungumzia ni hatua gani inafaa kuchukuliwa iwapo matokeo yanakuwa ni mazuri au mabaya ili kumsaidia mkulima mdogo kwa jinsi gani anaweza kufaidika na kilimo chake na kuepuka kupata hasara.

"Bidhaa kwa sasa zinatakiwa kuongezwa thamani, bidhaa kama haijaboreshwa haiwezi kuwa na soko zuri la ndani na hata nje ya nchi, tunataka kujua matokeo yake yanakuwaje maana biashara inavutia kutokana na soko lake lilivyo,

"Watu wanatakiwa kujua matokeo kama ni mazuri wafanyaje kama wengine wanaweza wanachangamkia fursa au kama ni mabaya wajue jinsi gani wanaweza kupunguza athari hizo ... tunatazama hilo maana hata sera zilizopo sasa hazisemi hatua gani ichukuliwe kama matokeo ni mabaya au mazuri," alisema Dkt. Mashindano.

Baadhi ya washiriki wa warsha hiyo wakihangia mada zilizokuwa zikijadiliwa.



Baadhi ya washiriki wa warsha ya kujadili kuhusu kilimo na biashara iliyoandaliwa na Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF).



Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja.

No comments: