Tangazo

May 19, 2017

MUHAS WATAKIWA KUWEKA MAKAZI YA KUDUMU OLOLOSOKWAN

Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimetakiwa kuhakikisha kwamba wanatumia vyema kijiji cha kidigitali cha Ololosokwan katika kuhakikisha kwamba taifa linakuwa na uwezo mkubwa katika tiba mtandao. Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya wakati akifunga warsha ya siku 2 ya tiba mtandao iliyofanyika chuoni hapo. Warsha hiyo ilikuwa inakokotoa tiba mtandao ili kuwezesha mradi wa majaribio wa Tiba mtandao unaohusisha wadau mbalimbali kutekelezwa. Kitovu cha mradi huo ni kijiji cha Ololosokwan kilichopo Waso wilayani Ngorongoro. Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya akizungumza na wataalamu kutoka KCMC, MUHAS wadau kutoka The Africa Foundation, Aga Khan Foundation, Ubalozi wa Uswisi, Bill & Melinda Gates Foundation, XPRIZE pamoja na Maafisa wa afya wa mikoa na wilaya za Arusha na Ngorongoro walioshiriki kwenye warsha ya siku mbili ya tiba mtandao iliyofanyika MUHAS jijini Dar es Salaam.(Picha zote na Thebeauty.co.tz)

 Katibu huyo alisema kutumia kikamilifu kwa kijiji hicho hakumaanishi kuwa na majengo bali kutumia kufunza wataalamu mbalimbali kutokana na ukweli kuwa kijiji hicho sasa kitakuwa mfano wa utendaji katika kusaidia wananchi wa Tanzania. “Uwapo wa kijiji hiki ni tukio kubwa kwetu kwani ni kijiji cha kujifunzia, namna ya kutibu, namna ya kukusanya takwimu namna ya kubaini mahitaji na … ni mfano wa namna gani teknolojia inaweza kufanya mambo makubwa” alisema Ulisubisya . Alisema yeye anaamini kwamba si lazima wataalamu watiba wafundishwe eneo moja, kama ilivyo sasa, lakini wanaweza kufundishwa katika eneo kama Ololosokwan na hivyo kuwajenga pia kisaikolojia kwamba wanaweza kufanyakazi pembezoni bila ya tatizo. Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO), Zulmira Rodrigues (kushoto) akichangia jambo wakati wa kuhitimisha warsha ya siku 2 ya tiba mtandao iliyofanyika chuoni hapo. Wa pili kushoto ni mgeni rasmi Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Prof Ephata Kaaya (wa pili kulia) na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Prof Eligius Lyamuya (kulia).

Alisema mafanikio ya dhana ya tiba mtandao yatasaidia sana kuboresha hali ya watanzania kwa kuwa mahitaji yao yatajulikana mapema na kutokana na ukweli kuwa mradi wenyewe unahusisha pia ukusanyaji wa data wa uhakika kwa kuzingatia mahudhurio ya watu na magonjwa yao. Pia alisema kwa utekelezaji thabiti utaonesha namna ambavyo Watanzania tuko mbele na kusema kwamba mradi huo wa tiba mtandao anauelewa na ameupigania sana nje ya nchi ambako amekwenda kuzungumza. “Mwaka jana mwezi Desemba nilienda kwenye mkutano Washington unaohusu Tiba mtandao na tumeuza sana hili wazo la tiba mtandao kwa wenzetu, kwa hiyo watakuja kujifunza tunafanyaje” alisema Dk. Ulisubisya na kuongeza kwamba Wizara yake itatoa ushirikiano wa kutosha kuona dhana hiyo inatekelezeka tena kwa ufanisi. Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi - Muhimbili (MUHAS), Prof Eligius Lyamuya (kulia) akitoa maoni wakati wa kufunga warsha ya siku 2 ya tiba mtandao iliyofanyika chuoni hapo.


Kwa mujibu wa mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) Zulmira Rodrigues utoaji huo wa tiba mtandao kwa majaribio utaanza mapema zaidi kabla ya mwezi Oktoba mwaka huu na kutanuka kwa jinsi inavyowezekana kwa kuangalia ufanisi wa kijiji. “Dhana hii itawezesha kuendelea na utoaji wa huduma bora za afya, zenye ufanisi wa kitaalamu zaidi katika maeneo ya vijijini, ambayo mara nyingi huachwa nyuma katika utoaji wa huduma hizo,” alisema Zulmira Tiba mtandao katika kijiji hicho itahusisha upasuaji mdogo ambao utafanywa na watendaji waliopo katika kliniki za kijiji hicho wakielekezwa na mtaalamu bingwa. Mhadhiri na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Tehama wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi - Muhimbili (MUHAS), Felix Sukums akiwasilisha mapendekezo ya mpango wa utekelezaji wa mradi wa tiba mtandao kwa mgeni rasmi (hayupo pichani), Kushoto ni Meneja Mradi wa Kijiji cha Kidigitali kutoka UNESCO, Tiina Neuvonen.

Aidha akizungumza katika ufungaji wa warsha hiyo Zulmira alitaka kuwapo kwa matumizi ya maabara ya kisasa iliyopo hapo ili iweze kusaidia taifa. Hata hivyo mwakilishi huyo wa UNESCO alisema kwamba Daktari wa wilaya ambako kijiji cha Ololosokwan kipo anahitaji kiasi cha dola elfu 70 kukamilisha baadhi ya mambo ili kuwa na uhakika pamoja na kuleta madaktari wa Afrika mabingwa kuja kufanya kazi kwa muda. 

 Akizungumzia suala hilo, Dk Ulisubisya alisema kwamba anajua shida iliyopo, lakini akamwagiza DMO kukaa na DAS (Katibu Tawala Ngorongoro) kuona namna ya kufanikisha haja ya sasa ya nyumba za makazi kwa gharama nafuu na kusema anaamini wanaofaidika wako tayari kusaidia kidogo. Alisema bajeti hiyo naamini inaweza kupungua kwa kutumia mali ghafi rahisi yenye kudumu zaidi. Majadiliano yakiendelea katika kuboresha mpango wa utekelezaji wa mradi wa tiba mtandao wa kijiji cha Ololosokwan, wilayani Ngorongoro mkoani Arusha wakati wa kuhitimisha warsha hiyo ya siku 2 iliyofanyika MUHAS.

Pia aliwashukuru UNESCO kwa kuwezesha Ololosokwan kuwa sehemu ya kujifunza na kutanua mradi wa tiba mtandao ambao amesema kwa kuzingatia teknolojia iliyopo sasa Watanzania na dunia kwa ujumla wanapata nafasi ya tiba bila kuwa karibu na bingwa. 

 Katika utekelezaji wa mradi huo hatua ya pili mifumo yote (maunganisho ya kisetelaiti) inatarajiwa kuwa tayari ifikapo Julai na hivyo kuwa na nafasi ya kuanza matibabu ifikapo Oktoba mwaka huu au mapema zaidi. 

 Mradi huo unoanza kwa majaribio unahusisha zaidi wagonjwa wanaoweza kufika kupata matibabu katika kijiji cha kidigitali cha Ololosokwani na kwa kuanzia huduma hiyo itatolewa kwa mama na mtoto na afya ya kinywa, masikio, pua na koo (ENT), ambapo mabingwa kutoka KCMC na MUHAS wanaweza kufanya tiba kwa kutumia mtandao.
  Mratibu wa E-Medicine kutoka Idara ya Tiba Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dr. Liggy Vumilia akifafanua jambo kwa mgeni rasmi wakati wa kuhitimisha warsha hiyo.

Kliniki ya Digitali ilizinduliwa katika kijiji cha Ololosokwan Ngorororo, Arusha mwezi Novemba mwaka 2016. Kijiji hicho tayari kina uwezo wa kupata huduma hizo. Warsha hiyo iliyokutanisha wataalamu mbalimbali wa tehama na madaktari kutoka Arusha , Manyara , Kilimanjaro na Dar es salaam ilichambua dhana ya tiba mtandao na kuidadavua dhana ya utekelezaji kamilifu wa jaribio la utoaji wa huduma za afya kwa kutumia teknolojia ya kisasa, na na namna ya kuirasimisha kama mfumo wa kuboresha afya maeneo yaliyo pembezoni ya miji na vijijini.
Mmoja wa washiriki akiwalisha maoni kwenye warsha ya siku 1 ya kujadili mapendekezo ya mpango wa utekelezaji wa mradi wa tiba mtandao iliyomalizika MUHAS jijini Dar es Salaam.
Picha juu na chini wataalamu kutoka KCMC, MUHAS, UNESCO, wadau kutoka The Africa Foundation, Aga Khan Foundation, Ubalozi wa Uswisi, Bill & Melinda Gates Foundation, XPRIZE pamoja na Maafisa wa afya wa mikoa na wilaya za Arusha na Ngorongoro walioshiriki kwenye warsha ya siku mbili ya kuandaa mpango wa utekelezaji wa mradi wa tiba mtandao iliyofanyika MUHAS jijini Dar es Salaam. Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO), Zulmira Rodrigues akimshukuru mgeni rasmi Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya mara baada ya kufunga warsha hiyo ya siku 2 iliyofanyika katika kumbi za MUHAS, jijini Dar es Salaam. Mkurugenzi Mwandamizi wa Uendeshaji kutoka Taasisi ya XPRIZE, Matt Keller (kushoto) akibadilishana mawazo na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO), Zulmira Rodrigues (katikati) pamoja na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Prof Eligius Lyamuya (kulia) baada ya kuhitimisha warsha ya siku 2 ya mradi wa tiba mtandao iliyofanyika jijini Dar es Salaa., MUHAS. Mgeni rasmi Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya katika picha ya pamoja na washiriki wa warsha hiyo. Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya akimpongeza Meneja Mradi wa Kijiji cha Kidigitali kutoka UNESCO, Tiina Neuvonen mara baada ya kufunga warsha ya siku 2 iliyofanyika katika kumbi za MUHAS, jijini Dar es Salaam.

No comments: