Tangazo

October 19, 2017

HAKUNA MATATA’ YA TUMAINI MSOWOYA KUACHIWA ALBAMU YAKE OCTOBA 29


Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesera anatarajia kuwa mgeni rasmi katikauzinduzi wa albamu ya mwimbaji wa nyimbo za Injili Tumaini Msowoya, katika ukumbi wa Highland Hall mjini Iringa.

Wageni wengine wa heshima kwenye uzinduzi huo ni  Mbunge wa Jimbo la Iringa mjini, Mchungaji Peter Msigwa, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Asia Abdalah, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Ruaha Baby Baraka Chuma, wachungaji kutoka makanisa mbalimbali.

Akizungumza na Mwanaspoti, Msowoya alisema tayari albamu hiyo yenye nyimbo nane imeshakamilika.

“Naenda Iringa kurudisha shukrani zangu kwao, nataka wajue nipo huku sio tu kwa sababu ya kazi bali huduma ya kuimba niliyoanza ”

Alizitaja nyimbo zilizo kwenye albamu hiyo kuwa ni Hakuna Matata, Mwamba, Amenitengeneza, Furaha, Mungu Mkuu, Wanawake Jeshi Kubwa, Samehe na Mungu wa Rehema.

“Kazi hii nimeifanya chini ya usimamizi wa JB Production ikisimamiwa na Producer Smart Bilionea Baraka. Ndiye meneja anayesimamia kazi zangu kwa sasa,’ alisema Msowoya.

Wasanii watakaomsindikiza

Meneja wa Msowoya, Smart Bilionea Producer Baraka alisema tayari waimbaji na kwaya  mbalimbali kutoka Iringa na Dar es Salaam watamsindikiza kwenye uzinduzihuo.

Alizitaja kwaya zizothibitisha kumsindikiza kuwa ni Wakorinto wa Pili kutoka Mufindi, Muhimidini na kwaya ya Vijana kutoka Iringa mjini.

Baadhi ya waimbaji ni  Christopher Mwahangila anayetamba na wimbo wa ‘Mungu ni Mungu tu’, Mchekeshaji na mwanamuziki mpya wa Injili Tumaini Martine maarufu kwa jina la Matumaini wa Kiwewe, Christine Mbilinyi, Moses Simkoko, Ritha Komba na Witness Mbise kutoka Dar es Salaam.

Wengine ni Rebecca Baraka, Jesca Msigwa, Ester Mgunda, Rebecca Mwalingo, Dennis Lukosi,  Wadi Mbelwa, Peter Mgaya, Rehema Chawe, Twaibu Mgogo, Emma Sanga na Victoria Mwenda kutoka Iringa.

“Waimbaji watakaomsindikiza ni wengi nab ado tunaendelea kuwasajili wengine. Bado tupo kwenye mazungumzo na Bahati Bukiku ambaye anaangalia ratiba yake, ikiwa sawa tutakuwa pamoja,”alisema.

Aliwatanzania kupokea kazi ya Msowoya kutokana na ubora wake wa nyimbo zilizobeba ujumbe unaoweza kuisaidia jamii.

Historia

Hakuna Matata ni albamu ya pili ya Msowoya baada ya ile ya kwanza ya Natembea kwa Imani kutofanya vizuri sokoni.

“Bahati mbaya niliitengeneza kutokana na kiwango kidogo hivyo iliishia kabatini, namshukuru Mungu kwa sababu kazi hii ni nzuri na wakazi wa Iringa wameipokea. Naamini itapokelewa kote,”alisema.

No comments: