Tangazo

October 9, 2017

MFUMUKO WA BEI WA TAIFA WA MWEZI SEPTEMBA, 2017 UMEONGEZEKA

Na: Veronica Kazimoto
Dar es Salaam
09 Oktoba, 2017.

Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Septemba, 2017 umeongezeka hadi kufikia asilimia 5.3 kutoka asilimia 5.0 mwezi Agosti, 2017.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii Ephraim Kwesigabo kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) amesema kuongezeka kwa Mfumuko huo wa Bei kumechangiwa na kupanda kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula.  

Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei ni pamoja na mtama asiliamia 19.8, nazi asilimia 14.8, nyanya asilimia 10.5, mihogo asilimia 11.5, na Mchele asilimia 9.7.

Aidha, baadhi ya bidha zisizo za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko wa Bei ni pamoja na mkaa asilia 13.9, kodi za nyumba na makazi binafsi asilimia 6.3 na mabegi ya shule asilimia 9.4.

Akizungumzia thamani ya shilingi ya Tanzania, Kwesigabo amesema kuwa, uwezo wa Shilingi 100 katika kununua bidhaa na huduma umefikia Shilingi 92 na senti 18 mwezi Septemba 2017 ikilinganishwa na Shilingi 92 na senti 20 ilivyokuwa mwezi Agosti, 2017.

Mfumuko wa Bei nchini una mwelekeo unaofanana na nchi nyingine za Afrika Mashariki ambapo Mfumuko wa Bei wa mwezi Septemba, 2017 nchini Uganda umeongezeka hadi asilimia 5.3 kutoka asilimia 5.2 mwezi Agosti, 2017 wakati nchini Kenya umepungua hadi asilimia 7.06 mwezi Septemba, 2017 kutoka asilimia 8.04 mwezi Agosti, 2017.

No comments: