Tangazo

May 7, 2018

WAINGEREZA WAVUTIWA KUWEKEZA SELOUS, DK. KIGWANGALLA AAGIZA KUWEKWA MAKUBALIANO YA AWALI (MOU)

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akimuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA, Dk. James Wakibara (hayuko pichani) kushirikiana na wawekezaji kutoka nchini Uingereza kuandaa mkataba wa makubaliano ya awali (MoU) ya uwekezaji katika sekta ya utalii kwenye Pori la Akiba Selous, ofisini kwake Jijini Dodoma juzi. Wawekezaji hao pichani ni Eva Sanchez na Nicholas Negre.

Na Hamza Temba-WMU-Dodoma
..............................................................

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ameagiza uandaliwe mkataba wa makubaliano ya awali (MoU) ya utekelezaji wa mradi wa kuendeleza utalii wa picha katika Pori la Akiba Selous.

Mkataba huo wa makubaliano utahusisha wawekezaji kutoka Jiji la London nchini Uingereza na Serikali ya Tanzania kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA na  utakapokamilika utasainiwa na pande zote mbili.

Dk. Kigwangalla ametoa agizo hilo juzi ofisini kwake Jijini Dodoma kufuatia maombi yaliyowasilishwa kwake na wawekezaji hao, Eva Sanchez na Nicholas Negre.

Akiwasilisha maombi hayo, Sanchez amesema mradi huo utakuwa wa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA ambao ndio wasimamizi wakuu wa Pori la Akiba Selous utakapoanzishwa mradi huo. 

Amesema pamoja na mambo mengine mradi huo wa utalii wa picha pia utasaidia kupiga vita ujangili na kukuza uchumi wa jamii zinazozunguka pori hilo.

Dk. Kigwangalla amewataka wawekezaji hao kuwasilisha andiko la mradi huo, kufanya utafiti wa kina na tathmini ya athari za kimazingira zitakazoweza kujitokeza kutokana na uanzishwaji wa mradi huo.

Amesema kwa sasa Serikali inafanya marekebisho ya Sheria mbalimbali zitakazoiwezesha Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA  kutekelezaji majukumu yake ipasavyo ikiwemo uwekezaji wa aina hiyo kwenye sekta ya Utalii wa Picha na Uwindaji wa Kitalii.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA, Dk. James Wakibara amesema mamlaka hiyo itatoa ushirikiano wa kutosha kwa wawekezaji hao ili kutimiza azma ya Serikali ya kushirikisha wadau, watu binafsi na wawekezaji katika kukuza sekta ya utalii nchini.

Pori la akiba Selous ndio hifadhi kubwa kuliko zote nchini ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba takriban 50,000 katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara na Ruvuma. Mwaka 1982, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Uneso) lilitangaza eneo hilo kuwa moja ya eneo la Urithi wa Dunia na kuanza kuhifadhiwa.
  Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na muwekezaji kutoka Jiji la London nchini Uingereza, Eva Sanchez ofisini kwake Jijini Dodoma juzi alipowasilisha ombi lake la kuwekeza kwenye sekta ya utalii wa picha katika Pori la Akiba Selous.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA, Dk. James Wakibara (kulia) akifafanua jambo kuhusu uwekezaji huo.
 Mkurugenzi wa Utalii na Huduma za Biashara wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA, Imani Nkuwi (aliyesimama) akifafanua jambo kuhusiana na uwekezaji huo.
 Waziri Kigwangalla akisisitiza jambo katika kikao hicho.
 Waziri Kigwangalla akitoa maelekezo katika kikao hicho.
   Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiagana na muwekezaji kutoka Jiji la London nchini Uingereza, Eva Sanchez ofisini kwake Jijini Dodoma juzi baada ya kupokea ombi lake la kuwekeza kwenye sekta ya utalii wa picha katika Pori la Akiba Selous.
Picha ya pamoja ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla,  Wawekezaji wanaotaka kuwekeza kwenye utalii wa picha katika Pori la Akiba Selous Eva Sanchez na Nicholas Negre, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA, Dk. James Wakibara (kushoto) na Mkurugenzi wa Utalii na Huduma za Biashara wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA, Imani Nkuwi (kulia). 

No comments: