Tangazo

September 28, 2011

RAIS, DK. JAKAYA KIKWETE ATUMA SALAM ZA RAMBIRAMBI KUFUTIA VIFO VYA WATU 14 KATIKA AJALI MBEYA

Rais, Dk Jakaya Mrisho Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Abbas Hussein Kandoro kufuatia vifo vya watu 14 na wengine 40 kujeruhiwa vibaya kutokana na ajali ya barabarani iliyotokea tarehe 25 Septemba, 2011 katika kijiji cha Mbuyuni, wilayani Chunya, Mkoa wa Mbeya baada ya gari aina ya Mitsubish Fuso walilokuwa wakisafiria kupinduka wakitoka kweye mnada Wilayani humo.

 “Nimeshtushwa, na kusikitishwa kwa Taifa letu kupoteza, kwa mara nyingine, roho za Watanzania wenzetu 14 waliofariki kutokana na ajali mbaya ya barabarani katika eneo la mkoa wako,” amesema Rais Kikwete katika salamu zake na kuongeza:

 “Naomba unifikishie salamu zangu za pole kwa familia zote zilizopoteza wapendwa wao katika ajali hii mbaya.  Nawahakikishia kwamba
nipo pamoja na familia hizo katika kipindi chote cha maombolezo kwani msiba huu ni wetu sote.”   Rais Kikwete amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema azilaze pema peponi roho za marehemu wote.

Aidha, amesema anawaombea kwa Mola wote waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo wapone haraka ili waweze kuungana tena na familia zao na kuendelea na maisha yao ya kawaida.

Amesema kutokana na kukithiri kwa ajali za barabarani ambazo zimeendelea kulinyang’anya taifa nguvukazi muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu, vyombo vyote vinavyohusika na usalama wa barabarani havina budi kusimamia kwa karibu mwenendo wa vyombo vya usafirishaji wa abiria ili kuepusha kutokea kwa ajali zaidi za barabarani.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

No comments: