Tangazo

September 15, 2011

Vodacom kudhamini Mafunzo ya Waandishi wa Habari za Michezo Morogoro Oktoba 1-2.2011

Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando
MAFUNZO kwa ajili ya waandishi wa habari za michezo yatafanyika mkoani Morogoro Oktoba 1 na 2 mwaka huu chini ya udhamini wa Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania.

Katibu Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), Amir Mhando, amesema leo wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam kuwa maandalizi ya mafunzo hayo yanaenda vizuri na wana matumaini yatakuwa na manufaa makubwa.

Aliishukuru Vodacom Tanzania kwa udhamini wake na kusema ni hatua nzuri katika kutekeleza mikakati ya TASWA kuendesha mafunzo kwa wanachama wake na waandishi wa habari za michezo kwa ujumla chini ya kauli mbiu ya chama hicho isemayo: TASWA Mafunzo Zaidi.

Alisema mafunzo hayo yatahusisha washiriki 40 kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Pwani na kuongeza kuwa mwanzoni mwa Novemba pia wataendesha mafunzo kama hayo mkoani Arusha yakihusisha washiriki kutoka Tanga, Arusha, Kilimanjaro, Manyra, pamoja na baadhi ya washiriki kutoka Dar es Salaan.

Alieleza mwishoni mwa Novemba TASWA itaendesha pia mafunzo kwa wahariri wa habari za michezo, ambayo yatakuwa nje ya Dar es Salaam na kwamba mkoa husika utatangazwa baadaye.

Alielezea kuwa mafunzo ya Morogoro na Arusha yatahusisha masuala ya maadili ya uandishi wa habari,, masuala ya sheria za mambo ya habari na sheria za michezo mbalimbali.

Alisema washiriki wataelimishwa namna ya kuripoti habari za michezo ya mpira wa wavu, kikapu na riadha na kwamba kama mambo yataenda vizuri pia utaingizwa na mchezo wa ngumi.

Alieleza kuwa wakufunzi katika mafunzo hayo ni baadhi ya walimu wa mambo ya habari, wahariri wazoefu, wanasheria na pia wakufunzi wa michezo mbalimbali nchini.

 Kwa upande wake Meneja Uhusiano na Habari za Mtandao wa Vodacom Tanzania, Matina Nkurlu, alisema kampuni yake inajisikia fahari kubwa kudhamini mafunzo hayo na kuwa itaendelea kufanya hivyo kadri watakavyoweza na kuwa mafunzo ya Morogoro yatagharimu kiasi cha sh. Milioni saba.

“Vodacom Tanzania inajisikia fahari kwa kudhamini mafunzo haya kwani hii siyo mara ya kwanza kwa Vodacom kudhamini mafunzo ya aina hii, ambapo mwaka jana tuliendesha mafunzo na wahariri wa habari za michezo.

“Mwaka huu tunadhamini mafunzo ya TASWA yote haya tukiwa na lengo la kuboresha tasnia ya habari, mafunzo ya Arusha pia tutadhamini, lakini bajeti yake itaongezeka zaidi ya hii,” alisema Nkurlu.

Naye Katibu Msaidizi wa TASWA, George John alisema katika mkutano huo kuwa, chama chake kimeamua kuendesha mafunzo hayo kwa ajili ya kuwoangezea uelewa zaidi waandishi wa habari za michezo.

“Mafunzo yatasaidia sana kwani kwenye ripotingi yetu mfano mchezo wa mpira wavu huwa wengine wanauliza wameshinda kwa mabao mangapi? Wakati kule huwa ni mambo ya seti si mabao,” alisema John ambaye pia ni Katibu Msaidizi wa Chama cha Mpira wa Wavu Tanzania (TAVA).

1 comment:

Mbota Amani said...

Thank you John for your efforts to inform people!I am very happy to say asante mkubwa