Tangazo

October 12, 2011

Maelfu wajitokeza kupiga kura Liberia

Hali imekuwa shwari katika vituo vingi
Shughuli ya kuhesabu kura zinaendelea baada ya raia wa Liberia kujitokeza kwa wingi kuwachagua viongozi wapya kwenye uchaguzi wa pili baada ya kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
wapiga kura

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi James Fromoyan anasema matokeo yanatarajiwa baada ya siku mbili.

Rais Ellen Johnson Sirleaf anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Winston Tubman wa chama cha Democratic,ambaye mgombea mwenza wake ni mcheza kandanda maarufu Gearge Weah.

Mwandishi wa BBC mjini Monrovia Jonathan Paye-layleh anasema watu wengi walikuwepo vituoni hata baada ya muda wa kupiga kura kumalizika.

Ushindani mkali katika uchaguzi huo umechochewa na hamu ya watu ya kumpata kiongozi atakae wapa huduma bora za umeme, maji , barabara, nafasi za kazi, elimu na huduma za afya bora.

Kiongozi wa kundi la waangalizi kutoka jumuiya ya kiuchumi ya nchi za magharibi mwa Afrika Athiru Jegga ambaye pia anaongoza tume ya uchaguzi ya Nigeria, amesema kwa kiasi kikubwa shughuli hiyo imeendeshwa vyema licha ya kuwa ndio safari ya kwanza Liberia inasimamia uchaguzi wake.

Hata hivyo baadhi ya vyama vya upinzani havina imani kuwa tume hiyo itasimamia uchaguzi ulio huru na wa haki.

Umoja wa mataifa umetuma vikosi vyake kutoka Ivory Coast na jumla ya wanajeshi na polisi elfu nane watakuwa wanashika doria kote nchini Liberia.

Baadhi ya viongozi wa upinzani wamechukizwa na hatua ya kumpa Rais Ellen Johnson Sirleaf tuzo ya amani ya Nobel na wanadai kuwa hatua hiyo huenda ikawashawishi wapiga kura kumuunga mkono. Hata hivyo kamati ya Nobel imekanusha madai hayo.

No comments: