Tangazo

October 20, 2011

MWANDISHI WA ITV/RADIO ONE, MAULID HAMAD MAULID AZIKWA ZANZIBAR

Maelfu ya wananchi washiriki katika kusindikiza jeneza lenye mwili wa Mwandishi wa Habari wa ITV/Radio One Marehemu Maulid Hamad Maulid  kuelekea kuzikwa Bumbwini Wilaya Kaskazini 'B' Unguja jana Oktoba 19, 2011.
Waumini wa Dini ya kiislamu wakimsomea hitma  marehemu Maulid Hamad Maulid, katika msikiti wa Mombasa kwa Mchina,ambae alifariki juzi katika Hospitali ya Mnazi Mmoja Mjini Unguja jana Oktoba 19, 2011. Picha zote na Ramadhan Othman
MWANDISHI mahiri wa habari za michezo nchini, Maulid Hamad Maulid amezikwa jana kijijini kwake Bumbwini Mkoa wa Kaskazini Unguja saa tano asubuhi.

Maziko hayo yaliongozwa na na Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi, Ali Abdallah Ali na wawakilishi wa majimbo mbalimbali ya Zanzibar.

Mamia ya wanamichezo walikuwepo kwenye maziko ya Maulid ambaye hadi mauti yanamkuta alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) Zanzibar huku akifanya kazi vituo vya Redio One na ITV.

Maulid alifariki dunia juzi nyumbani kwake Jang’ombe mjini hapa kutokana na matatizo ya moyo yaliyokuwa yakimsumbua kwa muda mrefu.

Ibada ya kumsalia ilifanyika saa 3:30 asubuhi msikiti wa Noor Mohammad Kwa Mchina, Zanzibar na kuhudhuriwa na watu mbalimbali akiwemo Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho na kisha ndipo msafara ukaelekea Bumbwini Mkoa Kaskazini Unguja, ambako alizikwa saa tano asubuhi.

Katika maziko hayo TASWA Taifa, iliwakilishwa na Katibu Mkuu, Amir Mhando aliyeuelezea msiba huo kama pigo kubwa kwa waandishi wa habari za michezo na jamii kwa ujumla na kwamba ya njia ya kumuenzi ni kufuata misingi aliyokuwa ameisimamia wakati wa uhai wake.

Naye Katibu wa Taswa Zanzibar, Donisya Thomas alieleza kuwa waandishi wa michezo wamepoteza mtu muhimu katika maendeleo yao na kwamba pengo lake litachukua muda kuliziba.

Maulid wakati wa uhai wake amepata kuwa msemaji wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kabla ya kujiweka pembeni wakati wa uchaguzi uliofanyika mwaka jana.

Pia aliwahi kuwa Rais wa timu ya Taifa Jang’ombe iliyopata kushiriki Ligi Kuu Zanzibar. Marehemu ameacha mjane, Jamillah Nassor na watoto nane. 
Imetolewa na:
George John
Katibu Msaidizi TASWA

No comments: