Tangazo

October 13, 2011

"WAHUDUMU WA AFYA FUATENI MAADILI YA KAZI": MAMA SALMA KIKWETE

Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete
Na Anna Nkinda – Butiama
Wahudumu wa Afya nchini wametakiwa  kufuata maadili yao ya  kazi na kutoa kauli  nzuri kwa wagonjwa  ili kupunguza malalamiko yanayotolewa dhidi yao kutokana na  utendaji wao mbaya wa kazi.

Wito huo umetolewajana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wafanyakazi wa kituo cha Afya cha Butiama kilichopo wilayani Musoma katika Mkoa wa Mara.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisisitiza kwamba pamoja na mazingira ya kazi ya uhudumu wa Afya kuwa ni magumu wafanyakazi hao wanatakiwa kuipenda na kuiheshimu kazi yao  kwani kupanga ni kuchagua , wao walichagua kufanya kazi hiyo hivyo basi wanatakiwa kuipenda kazi yao.

“Baadhi ya wahudumu wa afya kila siku wanalalamikiwa  na wagonjwa wanaowahudumia  kutokana na kauli zao mbaya  wanazozitoa jambo ambalo si zuri matokeo yake  wanawachafua wauguzi wengine ambao wanatoa huduma nzuri kwa jamii na kuonekana kuwa wote ni wabaya”, alisema Mama Kikwete.

Mwenyekiti huyo wa WAMA aliendelea kusema kuwa  hivi sasa wanawake wanatakiwa kujikomboa wenyewe kimaisha hata kama wafanyakazi hao watakuwa wamechoka  kutokana na kazi nyingi walizonazo ni  lazima wawasaidie  wanawake wenzao hasa wajawazito ili waweze kujifungua salama.

Akisoma taarifa ya kituo hicho Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya ya Musoma Dk. Genchwele Makenge alisema kuwa kituo hicho kilifunguliwa mwaka 1972 kwa kusudi la kuweza kumhudumia Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, familia yake na wananchi kwa ujumla.

Huduma zinazotolewa katika kituo hicho ni Kliniki ya mama na mtoto, wagonjwa wa nje  (OPD) na wa ndani (IPD), huduma ya upasuaji mdogo na mkubwa, huduma ya majumbani kwa wenye magonjwa ya kusendeka (HBC) na kliniki maalum ya ushauri nasaha na upimajiwa hiari wa virusi vya Ukimwi, kliniki ya macho, Afya ya Akili na huduma rafiki kwa vijana.

Dk. Makenge alisema, “Mafanikio tuliyoyapata hadi sasa ni kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa wanaohudumiwa na kituo hiki hasa wagonjwa wa nje hadi kufikia wagonjwa 2800 kwa mwezi, kuongezeka kwa huduma ya upasuaji mdogo na mkubwa na kuongezeka kwa uvunaji wa maji na mvua”.

Aliyataja matatizo yanayowakabili kuwa ni kutopatikana kwa  maji muda wote, ukosefu wa vifa tiba vya kisasa kama vile X-ray mashine na utra sound mashine na kukosekana kwa watumishi wa kada mbalimbali na wenye ujuzi unaohitajika.

Mama Kikwete yuko mkoani Mara kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru na kilele cha wiki ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT)  ambayo kilele chake kinafanyika  kesho (leo) katika wilaya ya Tarime mkoani humo.

UWT ulitoa msaada wa pampu ya kuvutia maji na matanki manne kila moja likiwa na ujazo wa lita 5000 ili yaweze kukabiliana na tatizo la maji katika Hosiptali hiyo, uliandaa  dua ya kumuombea hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere    iliyosomwa na vijana wa madrasa wa msikiti wa Butiama, uliandaa ibada ya misa ya kumkumbuka Mwalimu Nyerere  iliyofanyika katika kanisa Katoliki Butiama pia  ulitoa tuzo kwa muasisi wa Umoja huo Mama Mariam Nyerere.

No comments: