Tangazo

October 13, 2011

JAMII YATAKIWA KUWAENZI WAZEE

Mama Fatma Karume
Na Anna Nkinda – Maelezo, Butiama

Jamii nchini imetakiwa kutowadharau, kuwanyanyasa  na kuwasahau wazee bali  wawaenzi  na kuwathamini kwani kupitia kwao itafaidika kwa kujifunza mambo mengi zaidi ambayo haikuwa inayafahamu.

Wito huo umetolewa jana na Mke wa Rais wa kwanza na Muasisi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Hayati Abeid Aman Karume Mama Fatma Karume wakati akiongea na wakazi wa Butiama  wilayani Musoma katika Mkoa wa Mara.

Mama Fatma ambaye ni mmoja wa waasisi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT)  alisema kuwa baadhi ya watu katika jamii wamekuwa na tabia ya kuwadharau wazee jambo ambalo linawafanya wasifahamu mambo mengi ya zamani na hivyo kutokutambua historia ya taifa lao.

“Vijana mmejaliwa kuwa na nguvu za kutosha nawasihi mtumie vizuri akili mliyonayo kufanya kazi kwa bidii kwani wazee wenu tunaona fahari kubwa pale ambapo vijana wetu mnafanikiwa kimaisha kama ilivyo  kwa wazee wenu”

Kwa upande wake Mke wa rais Mama Salma Kikwete ambaye aliambatana na Mama Karume kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru na wiki ya UWT ambayo kilele chake kinafanyika  kesho (leo) katika wilaya ya Tarime alisema kuwa mchango wa wazee ulisaidia kwa kiasi kikubwa  kupatikana kwa uhuru wa Tanzania.

Wakiwa katika kijiji cha Butiama UWT ulitoa msaada wa pampu ya kuvutia maji na matanki manne kila moja likiwa na ujazo wa lita 5000 ili yaweze kukabiliana na tatizo la maji katika kituo cha Afya, uliandaa  dua ya kumuombea hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere  iliyosomwa na vijana wa madrasa wa msikiti wa Butiama, uliandaa ibada ya misa ya kumkumbuka Mwalimu Nyerere  iliyofanyika katika kanisa Katoliki Butiama pia  ulitoa tuzo kwa muasisi wa Umoja huo Mama Mariam Nyerere.

No comments: