Tangazo

October 11, 2011

WATAALAM WA JINSIA KUKUTANA NA WAHARIRI WA ZANZIBAR

Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Ananilea Nkya.
Wataalamu wa  masuala ya  ukatili wa kijinsia (GBV) kesho Jumatano, (12 Oktoba, 2011)  watakutana na wahariri   wa vyombo mbalimbali vya habari  huko Zanzibar kujadili  mikakati  ya kutokomeza ukatili huo unaoongezeka kwa kasi nchini.

Mkutano huo utafanyika Mlandege katika ukumbi wa Shirika la Habari Tanzania (MCT), Zanzibar na kuhusisha wataalamu kutoka mashirika ya Shirika la Idadi ya Watu Duniani
(UNFPA), Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Wanawake na Watoto Zanzibar, Care Tanzania na Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar.

Mkutano huo utawapa fursa wahariri  kueleza uzoefu wao katika kuripoti vitendo vya ukatili wa kijinsia huko Zanzibar.

Vitendo vya ukatili  wa kijinsia vilivyoshamiri Tanzania Visiwani  ni pamoja na
ubakaji, ndoa za kulazimisha, mimba za utotoni, vipigo kwa wanawake, utelekezaji wa wanawake na watoto na wanawake kunyimwa fursa za kushiriki katika shughuli za kimaendeleo.

Tafiti zinaonesha kuwa vitendo hivyo vinaongezeka kutokana na kutokuwa na mbinu madhubuti za kukabiliana navyo miongoni mwa wadau pamoja na usiri unaoambatana na unyanyapaa dhidi ya waathirika.

Mkutano huo umeandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu (UNFPA) kama sehemu ya  shughuli za pamoja  za Umoja wa Mataifa.

Wahariri wa habari pia  wataeleza hatua watakazochukua ili kuimarisha  uandishi wa habari za ukatili wa kijinsia kwa lengo la  kushawishi mabadiliko kutoka ngazi za familia hadi taifa.

Vyombo vya habari vina umuhimu mkubwa katika kuzuia ukatili wa kijinsia kwa vile vina uhusiano wa moja kwa moja na jamii na watunga sera hivyo kujitolea kwake kunahitajika  katika kukabili tatizo hili.

Aidha TAMWA inaamini kuwa wakati umefika sasa kwa jamii nzima  kusimama kwa pamoja kuhakikisha kuwa wanaowafanyia vitendo vya ukatili wanawake, wasichana na watoto, sheria inachukua mkondo wake kwa wakati ili kudumisha  amani kwa makundi yote katika jamii.
 
Imetolewa na:
Ananilea Nkya
Mkurugenzi Mtendaji

No comments: