Tangazo

October 20, 2011

WATU WATATU WAMEFARIKI KATIKA AJALI MBAYA -MKOANI MBEYA

Majeruhi wa ajali hiyo.
Mwili wa marehemu Yuda Ambokile ukiwa umenasa kwenye gari.
Majeruhi mwingine aliyenusurika kifo.
Na Ezekiel Kamanga-Mbeya yetu.

Jinamizi la ajali mbaya limeendelea kuusakama mkoa wa Mbeya ambapo usiku wa kuamkia jana imetokea eneo la Mlima Nyoka Uyole Jijini humo na kuua watu watatu akiwemo dereva wa gari hilo dogo Yuda Ambokile Jeshi la Polisi limethibitisha.

Kaimu Kamanda wa Polisi, Anacletus Malindisa amesema Marehemu wengine ni Peter Kishimba mwenye umri wa miaka 47 mkazi wa Tazara Iyunga na Joshua Sanga mwenye umri wa miaka 2 mkazi wa Uyole jijini Mbeya na ajali hiyo ilitokea majira ya saa Moja na nusu kwa kuhusisha gari Nne ambazo zote zilijeruhi watu waliokuwemo ndani yake.

Wakizungumza na waandishi wa habari eneo la tukio, mashuhuda wa ajali hiyo walisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni kuharibika kwa gari aina ya Toyota Dyana yenye namba za usajili T 660 AUX ambayo ilikuwa imeegeshwa katika mlima huo.

Walisema kuwa kutokana na kuharibika kwa gari hiyo ndipo gari dogo aina ya Suzuki Escudo yenye namba za usajili T 425 BAZ , iliyokuwa ikitokea barabara ya Mbarali kwenda Mbeya mjini ambayo ilikuwa na abiria watano iliigonga gari hiyo na kusababisha kifo cha Dereva wake Yuda Ambokile na wengine kujeruhiwa vibaya na magari mengine Toyota Cheser T 512 BCT na Nissan T 991 BAK.

Baada ya gari hiyo kugonga gari iliyokuwa imeegeshwa na kusababisha madhara hayo ndipo gari nyingine aina ya Baloon ikagongwa na gari hiyo aina ya Escudo kisha Baloon hiyo ikatumbukia korongoni na kusababisha majeruhi wawili waliokuwemo ndani ya gari hiyo ambao wote walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya na Mmoja wao akaruhusiwa baada ya hali yake Kiafya kuimarika.

Ajali hiyo haikuishia hapo bali gari nyingine aina ya Pickup yenye namba za usajili T 991 BAK nayo ikakumbwa na dhahama hiyo ambapo iliharibika vibaya bila kusababisha majeruhi kwa watu waliokuwemo ndani yake.

Majeruhi wa ajali hiyo waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya na kutembelewa na waandishi wa habari leo, wengi wao walikutwa wakiwa na hali mbaya na kushindwa kuzungumza chochote bali baadhi yao waliokuwa na nafuu walisema kuwa walikuwa hawakumbuki chochote juu ya ajali hiyo zaidi ya kujikuta wamelazwa wakiwa na majeraha katika miili yao.

Majeruhi hao ambao baadhi yao waliweza kuzungumza na waandishi wa habari ni pamoja na Denis Untwa (24) ambaye ni dereva wa Baloon, Laina John Sanga (35), Michael Mteve (20), Anania Simbeye(35) ambaye ni dereva wa Escudo, Emmanuel Tambikeni na mmoja aliyejitaja kwa shida jina moja la Boniface..

No comments: