Tangazo

November 11, 2011

HUKUMU YA KESI YA MEYA WA ZAMANI WA RWANDA, NDAHIMANA KUTOLEWA NOVEMBA 17

Na Nicodemus Ikonko, Hirondelle, Arusha

Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) itatoa hukumu ya kesi ya mauaji ya kimbari inayomkabili meya wa zamani wa Rwanda, Gregoire Ndahimana, Novemba 17, 2011 kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na mahakama hiyo.

 Ndahimana, meya wa zamani wa wilaya ya Kivumu mkoa wa Kibuye, Magharibi ya Rwanda, anashitakiwa kwa mauaji ya kimbari, kula njama za kufanya mauaji hayo na kuteketeza kizazi kama uhalifu dhidi ya binadamu.

 Anadaiwa alikuwa anashirikiana na wenzake kufanya mauaji dhidi ya Watutsi waliokuwa wanapata hifadhi katika kanisa la Nyange wilayani humo kati ya Aprili 14 na 16, 1994 ambapo watu wapatao 2000 waliuawa.

 Wengine walihusishwa na mauaji yaliyofanyika katika kanisa hilo ni pamoja na Padre Athanase Seromba ambaye anatumikia kifungo cha maisha jela, mfanyabiashara, Gaspar Kanyarukiga ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na Fulgence Kayishema, Inspekta wa Polisi katika wilaya ya Kivumu ambaye bado anasakwa na ICTR.

 Wakati wa kutolewa hoja za mwisho mahakamani Septemba 21, 2011, mwendesha mashitaka aliiomba mahakama aliyokuwa inaongozwa na Jaji Florence Rita Arrey kumhukumu adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa sababu ya matendo aliyofanya katika nafasi yake kama Meya na kwa kutumia vibaya uaminifu wa watu wake kama kiongozi.

 Mwendesha mashitaka pia alidai kwamba mashahidi wake wamethibitisha pasipo mashaka kwamba Ndahimana alikuwa mshiriki mkuu katika kulibomoa kanisa la Nyange; aliongoza washambaliaji kwa kuonyesha mfano, aliwapatia nyenzo na kuwasaidia katika kila hatua ya uhalifu huo.

 Hata hivyo upande wa utetezi uliomba mteja wao aachiwe, wakidai kwamba mshitakiwa hana hatia yoyote kwa kuwa mashahidi wa mwendesha mashitaka hawaaminiki kutokana na kutofautiana katika ushahidi walioutoa mahakamani na hati za ushahidi wao zilizotolewa awali juu ya mauaji hayo.

 Kwa mujibu wa upande wa utetezi, Ndahimana hakuwapo katika eneo kulikofanyika mauaji hayo na mashahidi wa utetezi walitoa vielelezo vya kuunga mkono hoja zao.

Kesi ya Ndahimana ilianza kusikilizwa  Septemba 6, 2010 ambapo upande wa mashitaka ulileta mashahidi 15 na kuhitimisha kesi yake Novemba 19, 2010. Alianza kujitetea Januari 17, 2011 na kuhitimisha utetezi wake Mei 13, 2011 baada ya kuita mashahidi 30 kuunga mkono utetezi wake.

Mtuhumiwa huyo, alitiwa mbaroni Agosti 10,2009  Mashariki mwa DRC na kuhamishiwa ICTR mijini Arusha, Agosti 21, mwaka huohuo.

No comments: