Baada ya kupokea maombi zaidi ya 250 ya wanafunzi wa kidato cha sita, kampuni ya bia ya Serengeti kupitia mpango wa ufadhili wa elimu ya juu unaoendeshwa na kampuni ya bia ya EABL imewachagua wanafunzi bora wanne ambao wamefanikiwa kupewa ufadhili wa elimu ya juu. Wanafunzi wote wanne walifanya vizuri sana kwenye mtihani wa kidato cha sita, wote walipata daraja 1.
Wanafunzi hao ni, BERTHER HYERA (21), DICKSON TUMSIIME (20), FREDRICK MWABAFULA (20), na WALTER KWEKA (19).
Bertha Hyera, msichana anayeongea kwa utaratibu sana, kutoka shule ya sekondari Igowole ambaye anakwenda kusomea shahada ya usimamizi wa biashara na masoko katika chuo kikuu cha Mzumbe alikaririwa akisema, “mimi singeweza kuendelea na masomo yangu, kulikuwa hamna jinsi, kwasababu wazazi wangu hawana uwezo wa kuniendeleza kielimu”. “Ufadhili huu umerejesha nuru iliyopotea mbele ya maisha yangu,” alikaririwa msichana huyo anayetokea mkoani Iringa wakati wa mahojiano.
Akiungana na Bertha katika masomo hayo hayo DICKSON TUSIIME(22) ambaye hadi alipopata ufahili huu alikuwa hajakata tamaa.
Aliamini siku moja atasoma masomo ya elimu ya juu pamoja na ukweli kwamba hali halisi ya kiuchumi kwa wazazi wake isingemwezesha kuendelea. Baada ya kufaulu kuna wakati mwingine alijaribu kuwakusanya ndugu jamaa na marafiki wa karibu ili kumchangia fedha za kujiunga na chuo kikuu lakini jitihada zake ziligonga mwamba.
.Hatimaye ameweza kupatiwa ufadhili na kampuni ya bia ya Serengeti na kujipatia nafasi ya kusomea shahada ya usimamizi wa bishara na masoko katika chuo kikuu cha Mzumbe.
Mwanafunzi wa tatu aliye bahatika kupata ufadhili huu wa EABL ni FREDRICK MWAMBAFULA(20) kutoka Morogoro .
“Tatizo la umeme hapa nchini limenijengea msukumo mkubwa sana wa kutamani siku moja niwe mhandisi wa masuala ya umeme ili nipate nafasi ya kuwa mmoja wapo wa kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili.” alisema Mwambafula.
“Mbali na historia ya hali duni ya maisha niliokuwa nayo nilikuwa na matumaini. Ufadhili huu umekuwa ndoto ya kweli kwangu na kwamba sasa nitasoma kwa amani na niweze kufikia malengo yangu”aliongeza Mwambafula ambaye anakwenda kusomea uhandisi wa maswala ya umeme katika chuo kikuu cha Mlimani Dar es salaam.
Mwanafunzi wa nne na wa mwisho aliyenufaika na ufadhili huu ni WALTER KWEKA (19) kutoka moshi ambaye tangu shuleni amevutiwa sana na utendaji kazi wa mhasibu mkuu wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Walter ambaye ametokea shule ya sekondari majengo anakwenda kusomea shahada ya uhasibu na fedha katika chuo kikuu cha Mzumbe.
“Nilipopata ufadhili huu, nililia, machozi ya furaha yalinitiririka, nilikimbia kuwajulisha familia yangu na watu wangu wa karibu!”, alisema Walter.
Wanafunzi wote waliochaguliwa hawakua na mengi ya kusema, isipokuwa furaha isiyo na kifani. Walielezea kwa ujumla jinsi maisha yao yamebadilika na kuahidi kusoma kwa bidii.
Akiongea na waandishi wa habari katika ofisi za kampuni ya bia ya Serengeti zilizopo Oysterbay jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa mahusiano wa kampuni hiyo Bi. Teddy Mapunda amesema kuwa baada ya matangazo yaliyotolewa katikati ya mwaka huu kuhusu ufadhili wa elimu ya juu katika mwaka wa masomo 2011/ 2012,ilipokelewa idadi kubwa ya maombi.
Wote walioomba wamefanya vizuri sana katika masomo yao laikini hali mbaya ya kiuchumi inaonekana kuwa ni changamoto kubwa kwa wanafunzi ambao wamekua na nia ya kuendelea mbele kielimu.
“ Uteuzi ulifanywa kwa umakini mkubwa.Tuliweza kupata kuona kuwa hauna mashaka ya yoyote na kwamba wanafunzi bora wameweza kupewa zawadi inayostahili” alikaririwa Bi: Mapunda.
Mpaka saa wanafunzi waliofadhiliwa katika eneo hili kupitia mpango huu wa ufadhili wa elimu ya juu ya kampuni ya bia ya Afrika Mashriki wamefikia zaidi ya 160 ambapo wanafunzi 20 kati yao wanatokea Tanzania.Wanafunzi waliosailiwa kupitia ufadhili huu kwa kipindi cha miaka sita iliyopita walijiunga na chuo kikuu cha Mzumbe na chuo kikuu Mlimani.
No comments:
Post a Comment