Tangazo

November 21, 2011

Watoto Yatima 537 wafaidika na Ufadhili wa Masomo wa WAMA

Mwenyekiti wa WAMA, Mama salma Kikwete
Na Anna Nkinda – Maelezo

Jumla ya watoto yatima 537 wamefaidika na ufadhili wa masomo ya elimu ya Sekondari wa miaka minne unaotolewa na Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) inayoongozwa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete.


Hayo yamesemwa hivi karibuni na Katibu Mtendaji wa Taasisi hiyo Daud Nasibu wakati akiongea na wawakilishi  wa Sekta binafsi katika mkutano uliojadili  umuhimu mradi wa jinsi ya  kuwasaidia watoto yatima na wanaishi katika mazingira hatarishi ujulikanao kama FHI Pamoja Tuwalee.

Nasibu alisema kuwa watoto walionufaika na ufadhili huo ni kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani huku wengi wao wakiwa ni watoto wa kike wanaoishi katika mazingira magumu kwani moja ya malengo ya Taasisi hiyo ni kuwasaidia watoto yatima hasa wa kike ili waweze kupata elimu sawa na watoto wengine walio na wazazi.

“Watoto hawa wako katika shule za Bweni hii ni kuwafanya waweze kupata huduma zote muhimu ambazo ni chakula, malazi na muda wa kujisomea kwani watoto wengi wa kike wakisoma shule za kutwa  wanatumia muda mwingi kufanya kazi za nyumbani na hivyo kukosa muda wa kujisomea” alisema Nasibu.

Aliendelea kusema kuwa kutokana na umuhimu wa watoto wa kike kupata elimu Taasisi ya WAMA iliamua kujenga shule ya Sekondari ya mfano ya wasichana wanaotoka katika mazingira magumu ijulikanayo kama WAMA-NAKAYAMA iliyoko Nyamisati  wilaya ya Rufiji mkoani Pwani ambayo  ina wanafunzi 167 wa kidato cha kwanza hadi cha pili na itapofikia kuwa na  kidato cha sita itakuwa na  wanafunzi 510.

Taasisi ya WAMA ilianzishwa mwaka 2006 huku moja ya malengo yake ikiwa ni kumsaidia mtoto wa kike ambaye ni yatima na anayetoka katika mazingira magumu ili aweze kupata elimu sawa na watoto wengine walio na wazazi.

No comments: