Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mheshimiwa Fabian Massawe kufuatia vifo vya watu 18 kutokana na ajali ya barabarani iliyotokea juzi, Jumamosi, Novemba 19, 2011, katika eneo la Lusahunga, Biharamulo, Kagera.
Aidha, Rais Kikwete ametuma salamu za pole kwa watu wote 17 walioumia katika ajali hiyo ambako basi la Taqwa liligongana na lori kwenye barabara la Biharamulo-Ngara.
Katika salamu zake, Rais Kikwete amemwambia Mkuu huyo wa Mkoa, “ Nimepokea kwa masikitiko na huzuni habari za vifo vya wenzetu 18 waliopoteza maisha yao katika ajali ya basi la Taqwa. Kupitia kwako nawatumia salamu zangu za pole za dhati ya moyo ndugu, jamaa na marafiki wote waliopoteza watu katika ajali hiyo,”
Ameongeza Rais Kikwete: “Wajulisheni kuwa niko nao katika uchungu mkubwa walionao katika kipindi hiki cha maombolezo. Waambie kuwa msiba wao ni msiba wangu pia. Nawaombeeni subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu kwa sababu yote ni mapenzi ya Mungu. Namwomba Mwenyezi Mungu aziweka roho za marehemu pahali pema peponi. Amen.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Kwa wenzetu walioumia katika ajali hiyo, nawatumia pole zangu nyingi. Nawatakia heri waweze kupona haraka ili warejee katika shughuli zao za kujenga taifa na za kujiletea maendeleo.”
IMETOLEWA NA:
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
NOVEMBA 21, 2011
No comments:
Post a Comment