Tangazo

January 23, 2012

Wakenya Wanne kujibu Mashtaka ICC

William Ruto, Henry Kosgey na Joshua Sang'
Mahakama ya kimataifa ya jinai ya ICC imewakuta na kesi ya kujibu Wakenya wanne mashuhuri.

Wakenya hao ni aliyekuwa waziri William Ruto, mwandishi wa habari Joshua Sang', mkuu wa utumishi wa umma Francis Muthaura na naibu waziri mkuu Uhuru Kenyatta.


Ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka dhidi ya aliyekuwa waziri Henry Kosgey na mkuu wa zamani wa polisi Meja Jenerali mstaafu Mohammed Hussein Ali haukutosha kuanzisha kesi dhidi ya wawili hao.

Akitoa uamuzi huo kwa niaba ya jopo la majaji, jaji Ekaterina Trendafilova alisema kulikuwa na sababu za kuamini kwamba washukiwa William Ruto na Joshua Sang' huenda walichangia katika madai ya kuwatimua watu wa jamii ya Wakikuyu, Wakamba na Wakisii ambao walikuwa na misimamo tofauti ya kisiasa.

Katika kesi ya pili dhidi ya Uhuru Kenyatta na Francis Muthaura, mahakama ilisema huenda wakawa na mkono katika madai ya mateso dhidi ya binadamu na kuwatimua watu kwa nguvu kutoka makaazi yao.

Washukiwa hao wanne hata hivyo hawatazuiliwa katika mahakama hiyo na wako huru kwa sasa kuendelea na shughuli zao.

Kesi hizo ni kuhusiana na machafuko yaliyotokea baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 ambapo watu zaidi ya 1,200 walifariki dunia.
Source: BBC Swahili

No comments: