Tangazo

April 11, 2012

Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete aomboleza Kifo cha Gordon Mwakitabu

Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. Kikwete
 Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Katibu Mkuu wa CCM, Mheshimiwa Wilson Mukama kuomboleza kifo cha Katibu Myeka wake, Ndugu Gordon Mwakitabu, ambaye alifariki dunia asubuhi ya jana, Jumanne, Aprili 10, 2012 mjini Dodoma.

Katika salamu zake hizo, Rais Kikwete amesema kuwa ameshtushwa na kuhuzunishwa na taarifa ya kifo cha Ndugu Mwakitabu ambaye kwa miaka 15 iliyopita, tokea Julai mwaka 1996, amekuwa Katibu Myeka wa Katibu Mkuu wa CCM, na kufanya kazi na Makatibu Wakuu watatu wa Chama hicho.
Marehemu Gordon Mwakitabu
“Nimepokea taarifa za kifo cha ghafla cha Ndugu Mwakitabu kwa mshtuko na huzuni. Nakutumia wewe Katibu Mkuu wa CCM salamu zangu za rambirambi kuomboleza kifo hiki, na kupitia kwako naitumia familia ya ndugu Mwakitabu salamu za dhati ya moyo wangu kwa kuondokewa na mhimili mkuu wa familia. Wajulishe kuwa niko nao katika wakati huu mgumu wa msiba wa mpendwa wao,” amesema Rais Kikwete katika salamu hizo.

Ameongeza; “ Aidha, kupitia kwako natuma salamu zangu za rambirambi kwa viongozi, wanachama na wapenzi wa CCM kwa kuondokewa na mwenzi wetu. Wajulishe kuwa naungana nao katika kuomboleza kifo cha Ndugu Mwakitabu.”

Rais Kikwete amemwelezea Ndugu Mwakitabu kama mtumishi mwadilifu wa Chama cha Mapinduzi. “Katika kipindi chote cha utumishi wa Chama chetu, Ndugu Mwakitabu alikuwa mwadilifu, mwaminifu, mchapakazi aliyejituma na kujitolea kwa moyo wake wote kutumikia Chama wakati wote bila kujadili muda wa kazi. Alikuwa mchapakazi wa mfano na mchango wake katika utumishi wa chama utakumbukwa na kuenziwa daima.”

Katika salamu zake, Rais Kikwete amesema kuwa anaungana na wanafamilia na wana-CCM katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke pema peponi roho ya Marehemu Gordon Mwakitabu. Amina.
 
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
11 Aprili, 2012

No comments: