Tangazo

July 12, 2012

TATIZO LA MAJI HANDENI NI LA BANDIA

DC Handeni, Muhingo Rweyemamu
Na Mohammed Mhina, Handeni

 MKUU wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga Bw. Muhingo Rweyemamu, ameipiga marufuku Halmashauri ya Wilaya hiyo kuwauzia maji wafanyabiashara wakubwa wa maji na kuongeza uhaba wa bidhaa hiyo kwa wananchi wa kawaida katika mji wa Handeni.

Mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa wafanyabiashara hao ambao wanauziwa maji kwa bei ya shilingi 18,000 kwa boza lente ujazo wa zaidi ya lita 12,000 sawa na ndoo 600 na huwalangua wananchi kwa kuwauzia maji hayohayo kwa bei ya shilingi kati ya 300 na 500 kwa ndoo moja.

Bw. Muhingo amesema kuwa wafanyabiashara hao kwa kutumia magari hayo yenye maboza wamekuwa wakijipatia faida kubwa ya kati ya shilingi 180,000 na 300,000 kwa kila gari moja lenye boza la ujazo huo wa lita 12,000.

Hata hivyo Bw. Muhingo amesema kuwa hatua ya wafanyabiashara hao kupeleka magari yao hadi kwenye bwawa hilo kumekuwa kukiongeza uharibifu wa mazingira kwenye chanzo hicho cha maji wilayani Handeni.

Bw. Muhingo amesema amebaini kuwa, uhaba wa maji unaotangazwa kuwepo wilayani humo kwa muda mrefu sasa ni wa bandia na kwamba bwawa lililopo mjini Handeni likihudumiwa vizuri maji yake yanaweza kutosheleza kwa msimu wa mwaka mzima bila ya kuwepo kwa shida ya maji katika mji huo.

Amesema pamoja na uchakavu wa miundombinu ya maji kati mji huo, lakini maji ya bwawa hilo yanaweza kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali ya mji huo tofauti na inavyoelezwa na waliowengi kuwa Handeni kuna shida kubwa ya maji.

Mkuu huyo wa wilaya ya handeni amesema kuwa ingawa mashine ya maji iliyopo katika Bwawa hilo ina uwezo wa kufanya kazi kwa muda wa saa 22 kwa kila siku kwa kusukuma lita 45,000 za maji kwa saa moja, lakini amesema katika hali ya kushangaza, maji hayo yalikuwa yakielekezwa katika maeneo ya visiwa vya wafanyabiashara wakubwa huku wananchi waliowengi wa mji huo wakikosa maji kwa muda mrefu ama kuyanunua maji hayo kwa bei ya juu kutoka kwa wafanyabiashara hao.

Amesema baada ya kubaini hivyo, Mkuu huyo wa wilaya alitoa maelekezo kwa wafanyakazi wa Idara ya maji kuhakikisha kuwa wanasambaza maji kwa watu wote na katika mabomba ya umma ili yaweze kuwanufaisha wakazi wote wa mji huon a vitongoji vyake.

 Bw. Muhingo amesema ili kukomesha kabisa tatizo la maji wilayani humo, ofisi yake inaangalia uwezekano wa kuchimba mabwawa katika maeneo mbalimbali yakiwemo yale ya vijiji ambayo yana uhitaji mkubwa wa maji kwa wananchi pamoja na mifugo yao.

Hata hivyo, Mkuu huyo wa wilaya ya Handeni pia ameutaja mkakati mwingine wa kuipatia wilaya hiyo maji ya uhakika kuwa ni kuimarisha mradi wa HTM wa kuvuta maji kutoka katika mto Pangani kwenda mjini Handeni.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa wilaya ya Handeni wamepongeza juhudi za Mkuu huyo wa wialaya na kusema kuwa uhaba wa maji kwenye mji huo umekuwa ukisababishwa na watumishi wachache wa Idara ya maji ya mji huo wenye uroho wa kujitajirisha huku wananchi wakihangaika na kuilaumu serikali kwa ukosefu wa maji.

No comments: