Tangazo

October 17, 2012

MAADHIMISHO YA MIAKA 67 YA UMOJA WA MATAIFA TANZANIA YATAKA MATAIFA DUNIANI KUJADILI CHANGAMOTO ZA UHARIBIFU WA MAZINGIRA


Pichani Juu na Chini ni Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania Dkt. Alberic Kacou akizungumza machache kuhusiana na umuhimu wa wiki ya Umoja wa Mataifa inayoanza leo, ambapo amesema mabadiliko ya hali ya hewa yanayotokea duniani ni ushahidi wa kutosha wa ongezeko la mafuriko na ukame kunakotokana na uharibifu wa mazingira mambo ambayo tunapaswa kuyachukulia kama changamoto kwa kuwa yanatukwaza katika kutimiza malengo ya Maendeleo ya Milenia.

Ameongeza kuwa Wiki ya Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2012 inaadhimishwa kwa shughuli mbalimbali zinazolenga vijana, wanafunzi, wasomi, vyombo vya habari na jamii kwa ujumla.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bw. John Haule akizungumzia maadhimisho ya miaka 67 ya Umoja wa Mataifa ambapo pamoja na mambo mengine amesema kutakuwa na maonyesho yatakayofanyika katika viwanja vya Karimjee siku ya tarehe 23 na 24 mwezi huu ambapo wananchi wataona mipango na miradi mbalimbali ambayo Umoja wa mataifa umekuwa ukiisaidia Tanzania na pia amesema kutakuwa na mjadala wa wazi katika ukumbi huo siku ya tarehe 23 ambapo wananchi wanakaribishwa kushiriki na kutoa mawazo yao.

Na Mwandishi wetu
Tanzania inaungana na nchi nyingine mbalimbali duniani kuadhimisha miaka 67 ya Umoja wa Mataifa ambapo kutakuwa na shughuli mbali mbali zinazoanza leo tarehe 17 mpaka siku ya tarehe 24 Oktoba ambayo ndio siku ya kilele cha shughuli hizo.

Kitaifa nchini Tanzania miaka 67 ya Umoja wa Mataifa itaadhimishwa kwa kauli mbiu ambazo zimekuwa zikitoka kila mwaka na kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Changing Peoples’ Lives: Greening The Environment For Sustainable Livelihoods’.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bw. John Haule amesema kauli mbiu hiyo imekuja wakati muafaka ili kutukumbusha mahusiano yetu ndani ya Jumuiya ya Umoja wa Mataifa lakini vilevile inatukumbusha changamoto ya jinsi uharibifu wa mazingira unavyofanyika hivi sasa. Ameongeza kuwa wiki ya maadhimisho ya miaka 67 ya Umoja wa Mataifa itaadhimishwa na matukio mbali mbali ikiwemo uzinduzi wa leo, na Siku ya Familia itakayohusisha michezo mbali mbali itakayofanyika kwenye viwanja wa Leaders Club tarehe 20 Oktoba 2012.
 
Michezo hiyo itawahusisha wanadiplomasia waliopo nchini Tanzania, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje.

No comments: