Tangazo

February 21, 2013

TAMASHA LA PASAKA KUTIKISA UWANJA TAIFA DAR NA SAMORA IRINGA




Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya Tamasha la Pasaka, Alex Msama akizunguimza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo kuhusu maandalizi ya tamasha hilo. (Picha na Habari Mseto Blog)

DAR ES SALAAM, Tanzania
WARATIBU wa Tamasha la Pasaka, Kampuni ya Msama Promotions wamesema mikoa iliyoshinda nafasi ya uwenyeji wa tamasha hilo kwa mwaka huu, imefikia mitatu baada ya Dar es Salaam kuwa wa kwanza kujitwalia nafasi hiyo kwa wingi wa kura.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati inayohusika na uratibu wa tamasha hilo la kimataifa, Alex Msama, mikoa iliyoongezeka ni Mbeya na Iringa kwani wapenzi na wadau wa huko wamejitahidi kutuma maombi
kwa utaratibu ambao waliuweka.

Msama alisema mikoa hiyo mitatu ndio imepatikana kati ya saba hadi sasa kwa ajili ya tamasha hilo ambalo kwa mwaka huu litabeba ujumbe wa Amani na Upendo kwa watu wote kwani bila vitu hivyo, hakina kinachoweza kupangwa na kufanikiwa.

“Tumeamua Tamasha la safari hii libebe ujumbe huu kwani kuna kila dalili kuwa baadhi yetu tumeanza kuichoka amani, hivyo tunataka kufikisha ujumbe huu kwa Watanzania kama kuwakumbusha kwa vile ikipotea, ni vigumu kuirejesha,” alisema.

Alisema wameona ni jambo jema kwa tamasha hilo kubeba ujumbe huo kwa lenyewe pia limekuwa kielelezo cha amani na upendo sio tu kupitia ujumbe wa neno la Mungu ambao hupatikana kwenye nyimbo, pia limekuwa likiwaleta wengi pamoja bila kujali tofauti za dini.

Msama alifafanua kuwa, kwa jijini Dar es Salaam, tamasha hilo litafanyika kwenye Uwanja wa Taifa, jijini
Dar es Salaam hapo Machi 31 kabla ya kuhamia Uwanja wa Samora, Iringa hapo April mosi na Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Naye Janeth Christopher ambaye ni muimbaji wa injili chipukizi alisema fursa ya kuwapata waimbaji watakaoshiriki itawasaidia kwa sababu walikuwa hawana namna ya kuweza kupata nafasi ya kushiriki.
Janeth alisema awali walidhani kwamba, tamasha linaendeshwa kwa mfumo wa mtu mmoja ambaye ni Alex Msama kumbe linatushirikisha hata sisi wadau, jambo ambalo anaipongeza kamati ya maandalizi kwa kuwaona.
Aidha wakati taratibu za maandalizi ya tamasha hilo zikiendelea, wadau wanatakiwa kupiga kura katika mikoa yao ili kukamilisha mikoa takribani  saba ambayo inategemewa kufikiwa na tamasha hilo, wadau wanatakiwa kupiga kura kwa kuandika neno gospo halafu jina la mkoa unaotaka lifanyike na utume kupitia namba 15522.    
Wakati zoezi hilo likifanyika, litakalofuata ni zoezi la kuwapata waimbaji washiriki  ambao nao watapatikana kwa kuandika neono gospo, jina la mwimbaji, kikundi au kwaya na kuituma kwendanamba 15678.  

Tangu kuasisiwa kwa Tamasha hilo mwaka 2000 kwa lengo la kueneza neno la Mungu kwa njia ya nyimbo, pia limekuwa faraja kwa wenye mahitaji maalumu.

No comments: