Tangazo

December 22, 2013

Aoa Wanafunzi Mtu na Dada Yake

JESHI la Polisi Wilaya ya Nkasi kupitia dawati la Jinsia na Watoto, linamshikilia Pius Jacob Mkazi wa Kijiji cha Chala kwa kosa la kuoa mtu na dada yake, ambapo mdogo mtu alikuwa ni mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Kabwe wilayani Nkasi.

Jacob alikamatwa na Polisi wa Dawati la Jinsia na watoto Kituo cha Nkasi ikiwa ni wiki moja tangu amchukue kwa nguvu binti huyo wa darasa la tano (umri miaka 12) na kuja kuishi naye kama mke na mume huku akiwa tayari amemuoa binti mwingine wa kwanza mwenye umri wa miaka 16 ambaye pia ni dada wa binti wa pili.

Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Dawati la Jinsia Nkasi, CPL-Anna Kisimba alisema walimfuatilia Jacob na kumkamata baada ya wao kupewa taarifa na mmoja wa majirani wa mtuhumiwa kuwa alikuwa akiishi kinyumba na wanafunzi hao.

“…Tulikuwa katika ziara zetu za kawaida zilizoambatana na siku 16 za kupinga ukatili tukizunguka baadhi ya vijiji vya wilaya yetu, ndipo raia wema walituarifu kuwepo kwa tukio hilo na kuanza kufuatilia hatimaye kumkamata mtuhumiwa,” alisema Kisimba.

Tayari mtuhumiwa huyo amefikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Desenba 10, 2013 kwa kosa la kumuoa mwanafunzi na kubaka katika Mahakama ya Wilaya ya Nkasi, Mkoa wa Rukwa kujibu mashtaka ya tuhuma zake.

Akizungumzia tukio hilo, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri wa Wilaya ya Nkasi, Oscar Mdenye alisema baada ya kufuatilia zaidi wamebaini hata binti (16) aliyemuoa wa kwanza alikuwa ni mwanafunzi haijulikani alitumia mbinu gani za kumpata na kuanza kuishi naye kama mke na mume.

Aidha ameongeza kuwa kwa mujibu wa tarifa ambazo walizipata kutoka kwa majirani inadaiwa binti wa pili alimpata kwa kutumia nguvu na vitisho, kwani alimfuata nyumbani kwao na kudai anakuja kuwasalimia lakini baada ya kufika kwake alimjulisha binti huyo kuanzia sasa wewe ni mke wangu na kuanza kuishi naye.

“…Hadi Polisi na Ofisi ya Ustawi wa Jamii tunafikiwa na taarifa hizo inadaiwa mtuhumiwa huyu alikuwa tayari ameishi na binti huyu wa pili kwa wiki nzima nyumbani kwake, na majirani walijua baada ya binti wa pili (12) kuanza kulalamika kwao kuwa alikuwa amechukuliwa kwa nguvu na kulazimishwa kuolewa,” alisema Mdenye.

Juhudi za kumpata mtuhumiwa kuzungumzia tuhuma zake hazikuweza kuzaa matunda baada ya kuwa mahabusu akisubiri mwenendo wa kesi yake inayomkabili.

Hata hivyo matukio ya ukatili yanayoripotiwa polisi kupitia Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Nkasi yamekuwa yakipungua kutoka mwaka hadi mwaka, kwani kwa mujibu wa takwimu za dawati hilo kwa mwaka 2012 kulikuwa na kesi 224 za ukatili zilizoripotiwa, ilhali kwa mwaka 2013 jumla ya kesi 143 zimeripotiwa wilayani hapo.

*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa ushirikiano na TAMWA

No comments: