Na Anna Nkinda – Maelezo, Dubai
Serikali ,
Asasi za kiraia, Sekta binafsi na watu mbalimbali wametakiwa kusaidia kuinua elimu ya wanawake kwakuwa faida yake ni pana
na endelevu na kwa kufanya hivyo watakuwa wameotesha mbegu ambayo matunda yake
yatanufaisha ulimwengu kwa kuufanya uwe na ustawi zaidi, amani na utengamano.
Wito huo umetolewa leo na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea
kwenye mkutano wa siku tatu wa wanawake kutoka nchi za Afrika, Asia na Mashariki ya Kati unaofanyika katika Hoteli ya
Atlantis The Palm iliyopo Dubai , Umoja
wa Falme za Kiarabu (UAE).
Mama Kikwete ambaye pia
ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema elimu pekee
ndiyo mkombozi wa mwanamke kwa kuwa husaidia kuboresha afya, uchumi, usalama na hupunguza
kwa kiasi kikubwa vifo vya watoto. Husaidia watoto kuwa na lishe bora na
kuboresha afya ya uzazi na kupunguza kusambaa kwa maambukizi ya Ugonjwa wa
Ukimwi.
“Umuhimu wa elimu kwa
wasichana na wanawake unafahamika kwetu sote kwa sababu elimu ni mlango kwa ajili ya fursa
na inafaida zaidi katika familia, jamii, nchi na bara zima kwani wanawake walio
na elimu ya msingi wanafursa kubwa ya kuepuka umaskini, kuwapatia watoto elimu na
kuongeza kipato chao kwa asilimia 10
hadi 20.
Mtoto aliyezaliwa na
mama aliye na elimu ana nafasi zaidi ya kuishi ukilinganisha na aliyezaliwa na
mama asiye na elimu, watoto walio na mama mwenye elimu ya msingi walau kwa
miaka mitano wananafasi ya asilimia 40 ya kuishi zaidi ya miaka mitano salama
pia mwanamke aliyeelimika anauwezekano zaidi kwa asilimia 50 ya watoto wake
kupata chanjo dhidi ya maradhi ya utotoni”, alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wa Tanzania Mwenyekiti
huyo wa WAMA alisema idadi ya watu ni
asilimia 44.9 kati ya hao wanawake ni asilimia 51.3 Serikali imepiga hatua
kubwa za maendeleo za kuwaendeleza wanawake na tayari imeridhia na kusaini maazimio
ya kitaifa na kimataifa yanayukusudia kuendeleza haki za wanawake.
Alisema Serikali imeanzisha sera, mikakati, sheria na
kanuni madhubuti zinazoboresha mazingira wezeshi kwa ajili ya usawa wa kijinsia
na kuwekeza rasilimali na nguvu kubwa kuimarisha haki za wanawake, kuboresha
majukumu na fursa katika siasa, kijamii na kiuchumi.
Mama Kikwete alisema, “Pamoja
na mafanikio makubwa tuliyoyapata katika kutoa elimu ya msingi kwa watu wote,
kufuta ujinga na kupunguza tofauti za kijinsia bado idadi ya wasichana katika
vyuo vya elimu ya juu ni ndogo ukilinganisha na wavulana hii inasababishwa na
utoro mashuleni ambao unatokana na tatizo la ujauzito, ndoa za utotoni na mila
hatarishi”.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Maendeleo ya kiuchumi na Uongozi (CELD) chenye
makao yake makuu nchini Nigeria ambao ndiyo waandaaji wa mkutano huo Mama Furo
Giami alisema huu si muda wa kujadili mambo ya usawa wa kijinsia bali ni wakati
wa kuchukua hatua ili kuona kwamba usawa wa kijinsia unatekelezeka katika jamii.
Alisema takwimu zinaonyesha
ifikapo mwaka 2028 asilimia 75 ya wanawake watajihusisha katika biashara Dunia
nzima ingawa hivi sasa wanawake wanamiliki robo ya biashara
na nusu ya biashara hizo ni katika kuendeleza masoko na kukua kwa kazi za
kiuchumi wanazozifanya.
“Ingawa takwimu hizi
zinaonyesha uchumi wa mwanamke utakuwa umekuwa lakini hakuna usawa wa kijinsia
kwa mfano idadi ya wanawake ambao ni wakurugenzi watendaji katika makampuni 500
ni chache kwa mwaka 2012 ilikuwa ni
asilimia 4, katika viwanda vya uchumi asilimia
11.1 na katika masoko idadi ilishuka
hadi kufikia asilimia 7.2”, alisema Mama Giami.
Mkurugenzi huyo Mtendaji
alisema wanawake wanatakiwa kupewa nafasi ya uongozi ili waweze kupata
maendeleo ya kiuchumi kwa kuwawezesha kiuchumi
siyo tu kuwapatia haki zao katika sekta
za afya na elimu.
Mama Giami alisema, “Viongozi
wa nchi zetu wanatakiwa kuwapa wanawake teknolojia, mitaji, kuunga mkono miradi
ya kijamii na kudhibiti biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu kwa kufanya
hivyo maendeleo yatapatikana . Pia wahakikishe wanawake siyo kwamba wanapata nafasi pekee ya uongozi bali wanapata
nafasi ya kuchangia katika uchumi wao.
Mada kuu katika mkutano
huo ni Uongozi ni Elimu: Ufunguo wa mustakabali wa wanawake katika nchi zenye
uchumi unaoibuka ambapo washirikiki kutoka nchi za Afrika, Asia na Mashariki ya
Kati walipata nafasi za kujadili mafanikio na changamoto za kuwaendeleza
wasichana na wanawake kielimu.
No comments:
Post a Comment