Tangazo

December 20, 2013

Sikinde yajichimbia Bagamoyo kuikabili Msondo Ngoma - X Mass



Na Mwandishi Wetu

HOMA ya pambano la watani wa jadi katika muziki wa dansi nchini kati ya Mlimani Park 'Wana Sikinde' na Msondo Ngoma 'Baba ya Muziki' litakalofanyika siku ya Krismasi imeanza kupanda kwa bendi hizo kujificha kambini na huku wakipigana vijembe.

Bendi hizo kongwe nchini zinatarajiwa kuonyeshana kazi katika onyesho litakalofanyika kwenye viwanja wa TCC Club Chang'ombe, Temeke Dar es Salaam katika kunogesha sikukuu hiyo ya Krismasi.

Katika kuonyesha wamelipania pambano hilo bendi ya Sikinde tayari imeiendea Msondo wilayani Bagamoyo kwa ajili ya kuweka kambi yao na wamewatahadharisha 'mahasimu' wao hao wasije wakatoa visingizio baada ya kugaragazwa kwenye onyesho hilo.

"Sisi tumeamua kuweka kambi yetu mjini Bagamoyo ambako tutatua viwanja vya TCC kutokea huko ili kuisambaratisha Msondo, na tunataka wajipange sawasawa ili wasije wakatoa visingizio tena kwa maana kama vyombo vipya bendi zote imepewa na Konyagi," Katibu wa Sikinde, Hamis Milambo alisema.

Milambo alisema mashabiki wa dansi wajitokeze kwa wingi kushuhudia namna gani wanavyowachachafya wapinzani wao hao, ikizingatiwa hawajakutana kwa muda tangu mwaka jana.

Upande wa Msondo kupitia Meneja wao, Said Kibiriti, alisema hawana haja ya kutaja mahali kambi yao ilipo isipokuwa wamejiandaa kuwatoa nishai wapinzani wao siku ya onyesho hilo litakaloanza saa nane mchana.

"Sisi hatuna mchecheto wowote na mpambano huo, tunaendelea kujifua kimya kimya mahali ambapo siwezi kupataja kwa sasa," alisema Kibiriti.

Naye muimbaji anayekuja juu wa bendi hiyo ya Msondo alitokea Sikinde, Athuman Kambi, alisema amejipanga kuonyesha umahiri wake katika mpambano huo baada ya kufanya hivyo wakati akiwa Sikinde dhidi ya Msondo kwenye ukumbi wa Diamond na kuwawehusha mashabiki wa muziki wa dansi nchini.

"Najua watu watataka kuona nafanya kitu gani dhidi ya bendi yangu ya zamani iliyonitangaza vyema, wasiwe na hofu waje Desemba 25 waone nini nitakachofanya TCC Club Chang'ombe," alisema Kambi.

Mpambano huo wa Sikinde na Msondo umeandaliwa na kampuni ya Bob Entertainment na Keen Arts chini ya udhamini wa Konyagi, gazeti la NIPASHE, Integrated Communications, CXC Africa na Salute5.

No comments: