Nkasi-Rukwa
SAKATA la
ndoa iliyovunjwa na mahakama ya Mwanzo Wilaya ya Nkasi, Mkoa wa Rukwa limeingia
katika sura mpya baada ya uchunguzi zaidi kubainika kuwa mume aliyeiomba
mahakama ivunje ndoa yake, Ndebile Kazuri alimkatisha mke masomo ya elimu ya
msingi mkewe baada ya kumtia ujauzito akiwa darasa la sita.
Kwa mujibu
wa vyanzo vya habari ambazo mwandishi wa habari hii amevipata vinaeleza kuwa
Kazuri ambaye hivi karibuni ameiomba mahakama hiyo kuvunja ndoa yake na Bi.
Maria Tarafa kwa madai mke wake anakiburi na mdokozi wa vitu ndani ya nyumba
yao, alimkatisha masomo na baadaye kumuoa mwaka 2004.
Taarifa
zinaeleza kuwa Kazuri alimkatisha masomo Bi. Tarafa, mwezi Machi akiwa Shule ya
Msingi Isale iliyopo Wilayani Nkasi huku akiwa na umri wa miaka 15 na
alijifungua mtoto akiwa na umri wa miaka 16.
Taarifa
zinasema baada ya kutiwa ujauzito Bi. Tarafa wazazi wa mumewe walizungumza
kifamilia na kukubaliana wasimshtaki kwa kuwa atafungwa na mama na mtoto kukosa
huduma za baba. Baada ya hapo walikubaliana amuoe hivyo mume huyo alilipa
mahari na kumuoa binti huyo wa darasa la sita akiwa na umri wa miaka 16.
Akizungumza
na Thehabari.com, kuzungumzia madai hayo Bi. Tarafa amekiri kuwa ni kweli
kwamba alikatishwa masomo na Kazuri mwaka 2003 akiwa darasa la saba, lakini kwa
kuwa baba yake mzazi na baba mzazi wa Kazuri walikuwa marafiki sana
waliyamaliza wenyewe na kukubaliana watoto wao waoane.
Alisema
aliunganishwa na mumewe Kazuri mwaka 2004 akiwa na umri wa miaka 16 baada ya
mumewe huyo kulipa mahari (ng’ombe) kwa familia ya mzee Tarafa.
“…Inaniuma
sana kwa kitendo ambacho ananifanyia kwa sasa kwani alinikatisha masomo,
kanipotezea muda wangu na kaniongezea mzigo wa watoto wane na anataka niende
kuishi nao peke yangu baada ya kwenda kuongopa mahakamani,” alisema Bi. Tarafa.
Alisema
sababu alizozitoa mahakamani si za kweli kwani amekuwa akimpiga na kumnyanyasa
ndani ya ndoa yake na kumtaka aondoke kwake na kwenda kuishi kwao. Alisema kuna
kipindi mtalaka wake huyo aliwahi kumfukuza akiwa na watoto wawili na kurudi
nyumbani kwao lakini baadaye alikuja kuomba radhi na kutaka apewe mke wake
aende kuishi naye.
Kazuri
alifungua kesi katika Mahakama ya Mwanzo, Namanyere Wilaya ya Nkasi Oktoba 28,
2013, kesi namba 26/2013 iliyosikilizwa na Hakimu aliyetajwa kwa jina la B.
Stanley; na Novemba 18, 2013 hakimu huyo baada ya kuisikiliza kesi aliamuru
ndoa ivunjwe.
Mahakama
ilivunja ndoa hiyo na kuamuru Bi. Tarafa aondoke na watoto wawili kati ya wanne
waliozaa na mumewe kipindi wakiishi kama mke na mume bila kueleza namna watoto
hao watakavyo pata huduma toka kwa baba yao.
Katika
hukumu yake mahakama iliamuru watoto wa miaka 7 na 9 watabaki kwa baba yao na
wenye miaka chini ya saba kubaki na mama yao. Mahakama hiyo ya mwanzo pia iliamuru
mke apewe magunia 9 ya mahindi kati ya 10 ambayo walizalisha wote na bati 7
zilizokuwa nyumbani kwao.
Hata hivyo
alipotafutwa Kazuri kuzungumzia madai hayo kwa njia ya simu hakuweza kupatikana
kwani taarifa ambazo zimetufikia ni kwamba, kwa sasa anashikiliwa na Jeshi la
Polisi Wilaya ya Nkasi kwa kitendo cha kuvunja nyumba ya mtalaka wake na
kumtishia kumdhuru huku akimtaka aondoke kwake ilhali mvutano ukiendelea.
*Imeandaliwa
na www.thehabari.com kwa kushirikiana na
TAMWA.
No comments:
Post a Comment