Tangazo

January 17, 2014

Mtibwa Sugar na Sinba SC kuvaana kesho katika Uwanja wa Taifa

 Na Asha Said

MABINGWA wa michuano ya mtani Jembe, timu ya Simba, kesho inashuka katika Uwanja wa Taifa kuvaana na timu ya Mtibwa Sugar, huku kiingilio cha chini kikiwa sh.5000.

Mchezo huo utakaoanza saa 10 jioni, ukiwa wa kirafiki, kwa ajili ya kuziweka timu hizo sawa kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu tanzania Bara, inayoanza kutimua vumbi wiki ijayo.

Simba inaingia dimbani ikiwa inatoka kwenye mashindano ya Mapinduzi, ambapo Simba ilichukua ushindi wa pili.

Katika mchezo huo Simba iliyopo chini ya kocha Zdravko Logarusic akisaidiana na Suleiman Matola, imepanga kutumia wachezaji wake, wote ili kiwe kipimo tosha kabla ya Ligi Kuu.

Timu hiyo inayoshika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi, imejipanga kuhakikisha inavuka mpaka nafasi ya kwanza huku kocha wao Logarusic, akisema ana uhakika kikosi chake kitaibuka na ushindi.

Logarusic, alisema kuwa mchezo huo ni moja ya mtihani wake wa kutambua kikosi chake, kabla ya kuanza kwa ligi kuu. Alisema ameambiwa kuwa Mtibwa Sugar, ni moja ya timu nzuri hivyo anajua kwake ni kipimo kizuri.

"Nina amini mchezo wetu na Mtibwa Sugar, utakuwa mzuri , kutokana na ubora wa timu hiyo, ninajua itasaidia timu yangu kupata mazoezi mazuri"alisema Logarusic.

Nae kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime, alisema ana amini mchezo huo utakuwa mzuri kwake kutokana na wapinzani wao kutoka katika mashindano.
Mexime alisema kuwa amepata nafasi ya kucheza na timu kubwa, ambayo itampa mazoezi mazuri.

"Nina amini mchezo huo utakuwa mzuri kwangu kwa kuwa nacheza na timu kubwa ambayo imetoka kwenye mashindano"alisema Mexime.

Katika mchezo huo viingilio vitakuwa shilingi 20,000 VIP A, shilingi 10,000 katika VIP B, wakati VIP C itakuwa shilingi  7,000 na sehemu ya viti vya orange na bluu itakuwa shilingi 5000.

No comments: