Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe akiongea na katika ubalozi wa Tanzania nchini Marekani mjini Washington DC, Marekani, ambako atapokea tuzo ya Africa’s
Most Impactful Leader of the Year kwa niaba ya Mhe. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania mjini humo leo.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amechaguliwa kuwa Kiongozi Mwenye Mchango Mkubwa Zaidi katika Maendeleo Barani
Afrika kwa mwaka 2013 .
Heshima
hiyo kwa Rais Kikwete imetolewa na jarida maarufu la kimataifa la African
Leadership Magazine Group na Tuzo la heshima hiyo itatolewa jioni ya kesho,
Jumatano, Aprili 9, 2014, katika sherehe iliyopangwa kufanyika Hoteli ya St.
Regis mjini Washington, D.C ikiwa ni pamoja na chakula cha jioni.
Tuzo
hiyo itapokelewa kwa niaba ya Rais Kikwete na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe, ambaye tayari amewasili
mjini Washington kwa sherehe hiyo kubwa.
Tuzo
hiyo ya heshima kubwa hutolewa kwa viongozi wa Afrika ambao hutoa mchango
mkubwa zaidi wa kiuchumi na kijamii kila mwaka kwa watu wao na limetolewa kwa
Rais Kikwete kwa mwelekeo wake usiokuwa wa kawaida na wenye mafanikio makubwa
kwa masuala ya utawala bora.
Jarida
hilo linasema kuwa ukweli wa hali hiyo bora ya utawala bora chini ya uongozi wa Rais Kikwete umeendelea kumiminiwa
sifa kimataifa na leo umeifanya Tanzania kuwa nchi ya kuigwa mfano kama kituo
cha uhakika cha uwezeshaji kutokana na mageuzi makubwa yaliyofanywa katika sera
na mifumo ya uchumi.
Jarida
hilo linasema kuwa Rais Kikwete alikuwa chaguo kubwa na la kwanza la wasomaji
wa Jarida hilo ambao walipiga kura kupitia njia mbali mbali za mawasiliano za
jarida hilo.
Linasema
Jarida hilo, “Kuhusu maoni ya wasomaji wetu juu ya kiongozi yupi wa Afrika ambaye ni
hodari zaidi kwa maendeleo ya kiuchumi na maendeleo, matokeo ya majibu ya swali
hilo yamedhihirisha bila shaka yoyote kuhusu nafasi ya Rais Kikwete katika
uongozi wa nchi yake. Na ushahidi uko kila mahali – ameweza kusimamia uchumi
ambao umekuwa kwa wastani wa asili mia saba kwa miaka yote ya uongozi wake.”
Sherehe za kesho, miongoni mwa mambo mengine,
zitaliwezesha Jarida hilo kutangaza mafanikio ya Tanzania chini ya uongozi wa
Rais Kikwete kwa Jumuia ya Kimataifa, ikiwa ni pamoja na Jumuia ya Kimataifa ya
Kibiashara, wanadiplomasia na taasisi nyingine zenye ushawishi mkubwa katika
medani za kimataifa na zenye makao yake katika Jiji la Washington na maeneo ya
jirani.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR
ES SALAAM.
No comments:
Post a Comment