Na Mwandishi Wetu
MWILI wa mwimbaji mahiri
nchini aliyefariki dunia wiki iliyopita nchini Thailand, Amina Ngaluma
‘Japanese’ (pichani), unatarajiwa kuwasili Dar es Salaam Ijumaa wiki hii.
Kwa mujibu wa mume wa
marehemu, Rashid Sumuni tayari taratibu muhimu kuhusiana na kuuleta mwili huo
nyumbani zimefanyika na wana amini mambo yataenda kama wanavyotarajia.
“Naomba niwajulishe kuwa
mwili wa mke wangu utaondoka Thailand Alhamisi wiki hii kwa ndege ya KLM na
utawasili Dar es Salaam siku inayofuata saa tatu usiku.
“Tunaamini kama mambo
yataenda kama tulivyopanga baada ya mwili kuwasili basi Jumamosi tutamhifadhi
mwenzetu. Msiba upo kwa wazazi wa marehemu Kitunda, Machimbo, Dar es Salaam
ambako ndiko maziko yatafanyika.
“Kimsingi imekuwa ngumu
kusema tutazika lini, kwa sababu bado mwili haujaletwa, lakini tayari familia
kwa kushirikiana na sehemu alikokuwa anafanya kazi na Watanzania wengine
waishio kule tumeshamaliza taratibu zote zilizokuwa zikihitajika ili kuuleta
mwili nchini,” alisema Sumuni kwa masikitiko.
Pia alivishukuru vyombo
vya habari kwa kuwa karibu na familia yao wakati wa kipindi hiki kigumu, lakini
akiomba wanapotaka kutoa habari kuhusiana na msiba huo wawasiliane na wahusika
wa familia ili kupata taarifa sahihi zaidi.
Ngaluma aliyepata
kung’ara na bendi mbalimbali nchini, alifariki dunia Alhamisi iliyopita kwa
shinikizo la damu akiwa Thailand alikokuwa akifanya shughuli za muziki katika
bendi ya Jambo Survivor.
Wakati wa uhai wake
alitamba na bendi mbalimbali zikiwemo African Revolution ‘Tamtam’, Double
M Sound ‘Mshikemshike’ na TOT Plus zote za Dar es Salaam.
Pia alipigia makundi ya
Arusha Sangoma, Sayari Band na Less Mwenge yote ya Arusha na Mangelepa na Sky
Sound za Kenya. Pia amepata kufanya shughuli za muziki kwa miezi sita nchini
Uganda.
Baadhi ya nyimbo
alizotunga wakati wa uhai wake ni Manyanyaso Kazini na Mapendo alizotunga akiwa
Tamtam, wakati Double M Sound alitunga nyimbo za Wajane na Ukewenza.
Pia alitoa albamu yake
binafsi iitwayo Jitulize yenye nyimbo kama Vidonge, Pete ya Uchumba, Good
Night, Uombalo Hutopata, Jitulize na Mzigo wa Moto.
Baadhi ya nyimbo alizopata
kuimba na kumpatia umaarufu mkubwa ni Mgumba, Maisha Kitendawili, Ndugu
Lawama, Zawadi ya Watanzania, Ugumu wa Maisha na Call Box zote zikitungwa na
Muumin Mwinjuma ‘Kocha wa Dunia’. Mungu amuweke mahali pema peponi. Amin.
No comments:
Post a Comment