Naibu Waziri wa Katiba na Sheria
Mhe. Angellah Jasmine Kairuki akiagana na Naibu Mkurugenzi Mkazi wa Shirika
la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo (UNDP) Bi. Mandisa
Mashologu (kulia) alipomtembelea Naibu Waziri ofisini kwake, Mtaa wa
Mkwepu, jijini Dar es Salaam leo (Jumatatu, Mei 19, 2014). Katikati ni
Mkurugenzi Mkazi wa UNDP Bw. Philippe Poinsot.
----------------------
Na
Mwandishi Wetu
Serikali
kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo
(UNDP) inatarajia kutoa mafunzo kwa Waandishi wa Sheria kwa lengo la
kuwaongezea uwezo wa kuandaa miswada katika lugha ya kiswahili – lugha ambayo
inatumiwa na watanzania wengi.
Naibu
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Angellah Jasmine Kairuki amemwambia Mkurugenzi
Mkazi wa UNDP Bw. Philippe Poinsot kuwa kwa sasa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali inatekeleza mkakati wa kuandaa miswada yote inayosilishwa Bungeni
katika lugha mbili, Kiingereza na Kiswahili ili kuwawezesha wananchi wengi
kuisoma.
Hata
hivyo, kwa mujibu wa Naibu Waziri Kairuki, katika kutekeleza kazi hiyo, Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Uandishi wa Sheria inakabiliwa
na changamoto kadhaa zikiwemo uhaba wa watumishi na uwezo na hivyo kuhitaji
msaada wa mafunzo.
“Kwa
sasa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ina kazi ya kuandaa miswada katika lugha mbili
ikiwemo Kiswahili ambayo ndiyo lugha ya taifa ambayo wananchi wengi
wanaifahamu,” alisema Bi. Kairuki katika mkutano wake na Bw. Poinsot leo
(Jumatatu, Mei 19, 2014) jijini Dar es Salaam.
Mkutano
huo ulifanyika katika ofisi ya Naibu Waziri Kairuki jijini Dar es Salaam na
kuhudhuriwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. George Masaju, Mkurugenzi
wa Mashtaka Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, Naibu Mwakilishi Mkazi wa UNDP Bi. Mandisa
Mashologu na maafisa wengine waandamizi wa serikali.
Akizungumza
katika mkutano huo, Bw. Masaju alisema kwa sasa Ofisi yake ina Waandishi wa
Sheria 18 tu na kuwa idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na majukumu ya Idara ya
Uandishi wa Sheria.
“Serikali
imeanzisha utaratibu huu wa kuandaa miswada katika lugha mbili lakini tuna
changamoto ya uhaba wa watumishi na hata hao waliopo, walifundishwa kuandaa
miswada katika lugha ya kiingereza na hivyo kuhitaji mafunzo,” alisema Bw.
Masaju.
Akiongea
katika mkutano huo, Bw. Poinsot alisema Shirika lake limepokea maombi ya
Serikali na kuwa litayafanyia kazi kwa kushirikiana na Serikali ili hatimaye
miradi hiyo itekelezwe.
“Kwetu
sisi UNDP, sekta ya sheria ni muhimu sana hususan katika miradi inayolenga
kuwasaidia masikini na kujenga uwezo … ndiyo maana tupo tayari kuisadia,”
alisema kiongozi huyo wa UNDP hapa nchini.
Kwa
mujibu wa Bw. Poinsot, Shirika lake limepanga kuisaidia Serikali kupitia mradi
wake unaolenga kuimarisha usimamizi wa utoaji haki (Strengthening
Administartion of Justice Project). Miradi ya awali inatarajiwa kuanza
kutekelezewa hivi karibuni kabla ya kuanza kutekelezwa kwa awamu ya pili ya
Mpango Maalum wa Shirika hilo (UNDAP II) unaotarajia kuanza kutekelezwa mwezi
Januari 2015.
Maeneo
mengine ambayo Serikali na UNDP zinatarajia kushirikiana ni katika utoaji wa
huduma za msaada wa kisheria; kuimarisha uwezo wa waendesha mashtaka na
watumishi wa mahakama; na kuboresha mifumo ya uendeshaji ili kupunguza
mlundikano wa kesi mahakamani.
No comments:
Post a Comment