Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza katika mkutano wa
maadhimisho ya miaka 50 ya nchi za G77 na China, uliofanyika jijini Santa Cruz,
Bolivia Juni 15, 2014. Picha na OMR
Xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na Mwandishi Maalum, Santa Cruz,
Bolivia
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal amezitaka nchi wanachama wa
G77+China, kuhakikisha zinaboresha kilimo ili ziwe na hifadhi ya kutosha ya
chakula kwa wananchi wake.
Akihutubia mkutano wa mwaka kwa nchi
za G77+China ambao pia ni kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya umoja wa nchi
hizi, unaofanyika jijini St Cruz De Sierra, Dkt Bilal alisema nchi za umoja huu
zina maeneo mazuri kwa kilimo na hivyo ni muhimu kuyatumia maeneo haya katika
kuzalisha chakula kwa lengo la kuhifadhi na kuwa na usalama wa chakula nyakati
zote.
Dkt. Bilal alisema, nchi hizi kwa
pamoja zinahitaji kuwa na kauli moja kuhusu masharti yanayowekwa na nchi kubwa
hasa katika kilimo na kuelezea kuwa ili mafaniio makubwa yapatikane, lazima
uwepo uwekezaji wa ndani katika kilimo sambamba na serikali za nchi hizi
kuchangia shughuli za uzalishaji ili kuwa na kilimo chenye tija kwa wakulima na
kinachoweza kuchangia usalama wa chakula.
Kuhusu suala la mazingira,
Mheshimiwa Makamu wa Rais aliwaeleza wajumbe wa G77+China kuwa, maazimio
yaliyofikiwa Rio+20 na mapendekezo kuhusu ‘Kesho tunayoitaka’ yanazihitaji nchi
hizi kupaza sauti zake kwa pamoja kuhusu kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi
kwani suala hili kwa sasa haliwezi kutatuliwa na nchi moja bali linahitaji
nguvu ya kila mtu duniani.
Makamu wa Rais alifafanua kuwa bila
kuwa na mazingira bora maendeleo endelevu yatabakia ndoto na pia kufanikisha
Malengo ya Milenia kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa itakuwa vigumu kama
suala la mazingira litaachwa kwa kila nchi kufanya inavyotaka.
“Kundi hili lina kazi kubwa iliyo
mbele yetu na hasa kuhusu malengo mapya ya maendeleo baada ya kukamilika kwa
muda wa Malengo ya Milenia mwakani. Tunahitajika kubuni njia za kuzipatia nchi
zetu maendeleo katika Nyanja za uchumi, kijamii na mazingira ili tufanikiwe
vema,” alisema Mheshimiwa Makamu wa Rais.
Katika hotuba hiyo Mheshimiwa Makamu
wa Rais pia alizungumzia kuhusu umuhimu wa nchi hizi kuweka msisitizo wa kuwapa
wananchi maji safi na salama, umuhimu wa kuwa na nishati inayotosheleza
matumizi ya uzalishaji, uwepo wa huduma bora za afya na elimu ili kupiga hatua
kwa haraka baina ya wananchi wa nchi hizi. “Nafahamu kufanikisha haya yote ni
kazi kubwa lakini hatuna muda wa kusubiri. Ni lazima tufanye kazi ili kubadili
hali iliyopo,”alifafanua.
Mkutano huo ambao umekamilika jana
kwa mwenyeji wake Rais Evo Morales kuwashukuru wanachama wa G77+China walioweza
kushiriki mkutano huo, pia ulionesha nia kwa wanachama wa nchi hizi kutafuta
majibu ya changamoto ya ukosefu wa ajira unaokabili wananchi wengi wa nchi
hizi. Viongozi wengi walisisitiza kuwa, suala la ajira hasa kwa vijana
linatakiwa kutazamwa upya na hasa ukizingatia rasilimali zilizopo katika nchi
za G77+China ili zitumike katia kutengeneza ajira mpya zitakazoweeza kusaidia
kuboresha maisha ya watu wa nchi hizi kwa miaka mingi ijayo.
No comments:
Post a Comment