Na
Anna Nkinda – Maelezo
Watanzania
wengi hawana uelewa wa tatizo la usonji (Autism) kwa watoto hivyo
basi uhamasishaji na utoaji wa elimu kwa jamii unahitajika ili watu
watambue tatizo hilo na kuweza kuwasaidia watoto hao.
Hayo yamesemwa jana na Mke wa Rais Mama Salma kikwete wakati
akiongea na Prof. Andy Shih ambaye ni Makamu wa Rais Mwandamizi wa Mambo ya
kisayansi kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Autism Speaks katika ofisi za Taasisi
ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) zilizopo jijini Dar es Salaam.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi hiyo
alisema jamii ikiwa na uelewa kuhusu watoto hao kutakuwa na mabadiliko
kwa wazazi na walezi hivyo basi ni jukumu la jamii nzima kuungana na kuweza
kuwasaidia watoto hao ili waweze kupata elimu na mafunzo maalum.
Mwenyekiti
huyo wa WAMA alimpongeza Prof. Shih kwa kazi anayoifanya ya kuwasaidia watoto
wenye usonji Duniani na kwa kitendo chake cha kuamua kuwasaidia watoto wa
Tanzania.
Kwa
upande wake Prof. Shih alisema tatizo la usonji linatibika kama watoto watapewa
mafunzo mapema na jamii ikipata elimu na kulifahamu tatizo hilo itaweza
kuwasaidia watu wenye matatizo hayo kupata huduma.
Alisema
alitembelea shule ya msingi Msimbazi Mseto ambacho ni kitengo mama cha kutoa
huduma ya watoto wenye usonji na kujionea hali halisi na kuahidi kushirikiana
na wadau wengine ili waweze kutatua changamoto zilizopo.
Taasisi ya WAMA kwa kushirikiana na wadau wa Afya nchini na
Taasisi ya kimataifa ya Autism Speaks yenye makao yake mjini New York
Marekani watafanya kazi kwa pamoja ili kutumia vitendea kazi na
utaalam wao ambao wameukusanya kwa miaka mingi kuwasaidia watoto wenye matatizo
ya usonji nchini.
Kazi
watakazozifanya ni pamoja na kuunda timu ndogo ya wataalam wa mitaala na
mafunzo ambao watapitisha miongozo na mitaala iliyopo pamoja na ile ya Autism
Speaks na kupendekeza utaratibu wa mafunzo ya makundi mbalimbali wakiwemo watoa
huduma.
Timu
hiyo inaandaa utaratibu wa mafunzo ya wazazi, walezi na familia ya mtoto mwenye
matatizo ya usonji, kuandaa mwongozo unaokubalika wa kuwapima na kuwatambua
watoto wenye usonji, kuandaa mitaala na miongozo ya ufundishaji wa watoto wenye
usonji na kutumia jukwaa na program za kitaifa kuwalinda watoto.
Wakati
wa Mkutano wa 69 wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa (UN) uliofanyika
mwishoni mwa mwezi wa tisa mwaka huu mjini NewYork Marekani Mama Kikwete
alikutana na Prof. Shih ambaye aliahidi kufanya kazi na WAMA ili kuwasaidia
watoto wenye tatizo la usonji ambao wataweza kupata elimu na huduma ya afya
kama watoto wengine.
No comments:
Post a Comment