Tangazo

April 30, 2015

SALAAM ZA RAMBIRAMBI ZILIZOTOLEWA NA KATIBU MKUU WA CHAMA CHA MAPINDUZI NDUGU ABUDLRAHAMAN KINANA WAKATI WA KUAGA MWILI WA BRIG. GEN. HASHIM MBITA (Mst) TAREHE 29 APRILI, 2015 – LUGALO DAR ES SALAAM

Ndugu Rais, Amiri Jeshi Mkuu na Ndugu Waombolezaji,

Maisha ni safari na kila safari huwa na mwisho wake,  Tuko hapa kwa kuwa safari ya Brig. Gen. Hashim Mbita duniani imefika ukingoni.  Tumekusanyika hapa siyo kuhuzunika bali kujivunia safari ya mafanikio makubwa ya Mwanamapinduzi, Mpiganaji, Mwanadiplomasia, Mwanahabari, Mwanasiasa na Mzalendo wa mfano.

Mwanasayansi mashuhuri Albert Enstain aliwahi kusema kuwa, thamani ya mtu itapimwa kwa mchango wake kwa jamii siyo kwa kile alichokipata kutoka kwa jamii yenyewe.  Hakuna ubishi, Brig. Gen Mbita alitoa mchango mkubwa kwa Watanzania na Waafrika.  Aliipenda na kulitumikia Taifa lake.  Alishiriki kikamilifu kulijenga na kuliimarisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania katika miaka ya awali na aliongoza Chama cha TANU kwa ufanisi.  Lakini mchango na umahiri wake ulidhihirika katika kuiongoza Kamati ya Ukombozi ya Bara la Afrika.

Kwa kumbukumbu zilizopo kila kazi na jukumu alilopewa Brig. Gen. Mbita iwe Jeshini, Serikalini, katika Chama, katika kuongoza Ukombozi na baadaye kuandika historia ya Ukombozi, aliteuliwa kwa makusudi maalum na kwa malengo maalum.  Alipelekwa Uingereza kutoka Ikulu kwa lengo la kusaidia kulijenga Jeshi la Wananchi Tanzania liwe la kizalendo baada ya maasi ya mwaka 1964. Kwa kuamini kuwa Chama imara ndicho kinachotoa uongozi bora kwa Taifa, Brig. Gen. Mbita aliteuliwa kuwa Katibu Mtendaji Mkuu wa TANU ili kuleta ufanisi na nidhamu katika Chama.

Kuna msemo maarufu jeshini usemao Kamanda aliye jasiri anaweza kuwa na bahati. Lakini hakuna Kamanda anayeweza kuwa na bahati bila ya kuwa jasiri. Ujasiri aliokuwa nao Brig. Gen. Mbita ndiyo iliyokuwa sababu ya kuteuliwa kwake kuiiongoza Kamati ya Ukombozi wa Afrika.  Alishiriki kuvijenga vikosi vya Frelimo (Msumbiji), ZANU-PF (Zimbabwe), SWAPO (Namibia), ANC (Afrika Kusini), MPLA (Angola), MOLINACO (Comoro), PAIGC (Guinea Bissau, Cape Verde)  na vyama vingine.  Aliviandaa vikosi hivi kupambana na majeshi makubwa yenye silaha nzito na za kisasa na yenye nguvu nyingi.  Lakini mwaka 1994, Brig. Gen Mbita alihitimisha kazi ya Ukombozi wa Afrika kwa ushindi mkubwa.

Chama Cha Mapinduzi kinatambua na kuthamini mchango na kazi kubwa iliyofanywa na Brig. Gen. Mbita katika kukiendeleza na kukiimarisha Chama cha TANU na baadaye Chama Cha Mapinduzi. Katika maisha yake kazini na hata baada ya kustaafu aliendelea kutoa ushauri, maoni na wakati mwingine kutoa uzoefu wake ndani ya Chama. Tutauenzi mchango wake, tutajifunza utendaji wake, tutajitahidi kuiga mwenendo wake na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu Muumba wa Mbingu na ardhi na mwenye kutupa na kutuondolea uhai, ili amuonee huruma mja wake huyu.  Brig. Gen. Mbita atabaki kuwa na nafasi muhimu katika historia ya mapambano dhidi ya ukoloni, ubeberu, ubaguzi wa rangi na uonevu.

Alikuwa kiongozi mwenye msimamo na mwenye kuelewa mambo mengi lakini msikivu. Inawezekana Watanzania wengi hatukumjua kwa kuwa hakushughulika kujulikana. Alikuwa jasiri na vile vile alikuwa na wingi wa unyenyekevu. Ujasiri wake ulidhihirika katika kufanikisha majukumu aliyokabidhiwa lakini unyenyekevu ulimzuia kujinadi.  Alitanguliza utumishi na kujiepusha na utukufu. Nafasi alizoshika zilikuwa za juu na zenye kuheshimika.  Kama angependa angeweza kupata umaarufu mkubwa katika nafasi aliyokuwa nayo lakini hiyo haikuwa hulka yake.  Maisha na Utumishi wake ni darasa kamili kwetu sote.

Tunawashukuru viongozi waliokuja kuwakilisha vyama mbalimbali kuungana na Watanzania kumuenzi Brig. Gen. Hashim Mbita.  Wanafalsafa wanatuambia ushindi wa kumbukumbu za wale tutakaowakumbuka zitadumu katika mioyo ya watu na katika historia ya Taifa walilolitumikia. Sihitaji kuwashawishi Ndugu waombolezaji wenzangu kukiri kuwa Brig. Gen Mbita atabaki kwenye mioyo yetu na kuendelea kukumbukwa na wananchi wengi wa Bara la Afrika alioshirikiana nao kuwarudishia Uhuru wao na heshima yao.

Kwa kumalizia, kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi natoa pole kwa Mama Mjane, Watoto, Ndugu na Jamaa, Marafiki na kwa Jeshi la Wananchi Tanzania.

Mwenyezi Mungu amfungulie milango ya Pepo.

Imetolewa na:

Idara ya Itikadi na Uenezi
Chama Cha Mapinduzi
30/04/2015

1 comment:

Vimax Asli said...

nice blog and article