Tangazo

April 30, 2015

WANAZUONI WAJADILI MUSTAKABALI WA TANZANIA DEMOKRASIA YA VYAMA VINGI

Jaji Francis Mtungi akifunguja mkutano wa wadau wa siasa  wa uimatishaji demokrasia ya vyama vingi
Jaji Francis Mtungi akifungua mkutano wa wadau wa siasa wa uimarishaji demokrasia ya vyama vingi.


Dk. Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dare s salaam ambaye amebobea katika masuala ya siasa amewataka wadau wa siasa na wananchi kwa ujumla kuzuia uvunjifu wa amani kuelekea uchaguzi mkuu kwa kufuata Sheria na kutobeza mamlaka.

Dk Bana alisema hayo jana akijibu swali la msimamizi wa mdahalo wenye lengo la kuimarisha demokrasia ya vyama vingi ulioandaliwa na Msajili wa Vyama vya siasa kwa ufadhili wa UNDP, Profesa Bernadetta Killian.

Profesa Killian alitaka kujua baada ya maelezo ya awali ya Dk Bana juu ya mtazamo wake kuhusu ukuaji wa demokrasia ya vyama vingi nchini Tanzania , nini kinastahili kufanya kuepuka uvunjifu wa amani hasa katika muda huu ambapo viashiria vipo.

Dk Bana alisema kama watu hawatafuata utamaduni wa vyama vingi, utamaduni wa kufuata sheria na kutobeza mamlaka, taifa litaingia katika machafuko.

Alisema watu kama wanaona wanaonewa wanatakiwa kufuata taratibu na kama taratibu hizo zinaonekana ni tatizo bado wanatakiwa kuwa na subira na kuondoa taratibu hizo zenye matatizo kwa kufuata utaratibu.

Katika shauri hilo la viashiria vya mizozo Profesa Rugumamu, aliyebobea katika masuala ya kutanzua mizozo aliihimiza Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa kutengeneza mfumo wa utambuzi wa viashiria vya hatari (early warning) ili iweze kukabiliana navyo mapema.

Akizungumzia kama Tanzania ni nchi ya demokrasia Dk. Bana alisema kwamba kuna maendeleo makubwa yamepatikana tangu mtindo wa vyama vingi kuingia nchini miaka 23 iliyopita.

Alisema demokrasia haijengwi kwa siku moja, ina safari ndefu yenye milima na mabonde na wakati mwingine watu wasifike.
Mkurugenzi UNDP Philippe Poinsot  akizungumza katika mdahalo
Mkurugenzi wa Mkazi wa Shirika Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP, Philippe Poinsot akizungumza na wawakilishi wa vyama mbalimbali vya siasa na kiraia katika mkutano huo.

Aidha alisisitiza kwamba demokrasia sio suala jepesi, lakini watanzania wanastahili kujivuna kwa hatuha waliyofikia katika mambo mbalimbali ambayo hata mataifa mengine ya Ulaya hayajafikia.
Alisema mwaka 1994 wakati taifa linaingia katika vyama vingi taifa lilikuwa na vyama 13 kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 1995 lakini sasa tunapozungumza kuna vyama 22 vyenye usajili wa kudumu, wigo wa kuwania dola ukiwa umetanuka zaidi.

Pia alisema mafanikio mengine ni namna ambavyo vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuandika inavyoona sawa, japo kumekuwa na tukio la kufungiwa kwa gazeti la Mwanahalisi, Mtanzania na Mwananchi, lakini kadhia hizo haziondoi ukweli kuwa kumekuwepo na uhuru mkubwa wa vyombo vya habari.
Dk bana akizungumza katika mdahalo
Dk Benson Bana akizungumzia demokrasia ya vyama vingi.

Alisema taifa hili halina sababu ya kuomba radhi kwa mafanikio yaliyopo na changamoto zake katika siasa kwani uelewa katika masuala ya siasa unazidi kutanuka.

Alisema pamoja na mafanikio hayo bado kuna mapungufu mengi hasa ya kutokuwa na utamaduni wa vyama vingi, utamaduni unaoambatana na vyama kuwa na aidolojia (itikadi), kukosekana kwa lugha za kistaarabu katika majukwaa ya siasa na hata mitafaruku ya ndani ya kivyama.

Alisema kutanuka kwa wigo wa ushiriki wa kuwania dola (vyama vingi vya siasa) kunatakiwa kwenda sanjari na kujenga utamaduni huo wa kuimarisha ustawi wa utamaduni wa vyama vingi.

Alisema pia kuna haja ya kuimarishwa kwa taasisi zinazosaidia utamaduni huo kama Tume huru ya Uchaguzi, Bunge na hata mfumo wa utawala ambapo wakuu wa mikoa na wilaya wasiwe katika hali ya kikada bali wale wanaoweza kutekeleza majukumu yanayostahili katika maeneo yao.
jaji Mutungi akiwa na Mkurugenzi UNDP Poinsot
Jaji Mutungi akiteta jambo na Mkurugenzi UNDP, Bw. Poinsot.

Aidha alisema kwamba vyama vingi vya siasa vinafanyakazi ya uanaharakati badala ya kuwa na itikadi ya kuifuata .

Alizungumzia pia haja ya vyama vya upinzani kujivunja na kuanzisha chama kimoja na kutengeneza mkakati wa kutwaa dola huku akisema muungano wa Ukawa kwa sasa una mushkeri zaidi badala ya kusaidia kujiandaa kutwaa dola.

Katika mdahalo huo ambao ulielezwa na Msajili wa vyama vya Siasa jaji Francis Mutungi, si mkusanyiko wa kufanya kampeni ya uchaguzi bali jukumu la ofisi ya msajili hasa kuelekea uchaguzi mkuu, washiriki wake pia walielezwa changamoto za siasa za vyama vingi.

Profesa Rugumamu alisema kwamba katika tafiti aliyoifanya yeye na wenzake katika nchi 15 za bara la Afrika wamekumbana na changamoto takribani saba ambazo ni kikwazo katika kupata na kukuza utamaduni wa demokrasia ya vyama vingi.
IMG_4917
Jopo la wanazuoni kuanzia kulia Dk Bana, Profesa Meena, Profesa Rugumamu na mwishoni ni msimamizi wa mdahalo Prof Bernadetta Killian.

Miongoni mwa changamoto hizo ni vyama vikongwe na utamaduni wake kushindwa kuainisha kati ya mamlaka ya dola na vyama vyenyewe, kuwepo kwa vyama vya kikanda na kidini katika kipindi cha mpito katika demokrasia ya vyama vingi, wanasiasa kubadili katiba waendelee kutawala, vyama na wanachama kutojua haki na wajibu wao kutokana na kutofundishwa uraia tangu awali.

Pia alizungumza uadui unaojijenga kwa nchi ambazo zimetoka vitani na uanzishaji wa makundi ya ulinzi ya vyama ambavyo husababisha mitafaruku wakati wa uchaguzi au kwenye uchaguzi na matumizi ya fedha yasiyojulikana kwa ama kukosa sheria au sheria kuwapo na watu kutoizingatia.
Alisema dosari zote hizo zinatikisa ujenzi wa utamaduni wa demokrasia ya vyama vingi.

Awali akimkaribisha Jaji Mutungi kufungua mkutano huo Mkurugenzi wa UNDP nchini, Philippe Poinsot alisema Umoja wa mataifa umefurahishwa kwa wadau wa siasa nchini Tanzania kuwa na mazungumzo yenye lengo la kustawisha amani kuelekea uchaguzi na kutengeneza mfumo wa majadiliano kama kukiwepo na kutokuelewana.

Alisema mkutano huo walioufadhili ni sehemu ya makubaliano ya Ofisi ya Msajili na UNDP kupitia mradi wake wa kuimarisha demokrasia (DEP) yenye kulenga kujenga uwezo na kuimarisha demokrasia ya vyama vingi na kuleta maelewano ndani ya vyama na kitaifa wakati nchi inaelekea katika uchaguzi mkuu.
IMsimamizi wa mdahalo Prof Bernadetta Killian
Msimamizi wa mdahalo Prof Bernadetta Killian.

Alisema ni matumaini yake kwamba mkutano huo utatengeneza mustakabari bora wa Tanzania kuwa na uchaguzi huru na wa amani.

Alisema kutokana na ushindani, uchaguzi unaweza kuleta matata kwa hiyo ni vyema kama wadau wataliangalia hilo na kuona namna ya kutanzua matata ili taifa libaki na amani na kusonga mbele katika maeneo yote ya jamii.

Naye Jaji Mutungi aliwaasa washiriki kutambua kwamba hakuna sababu ya kukamiana na kukomoana miongoni mwa vyama vya siasa kwani wote wanajenga nyumba moja na kimsingi hawana sababu ya kugombania fito.

Alitaka wadau kucheza mchezo wa siasa kwa maridhiano ili wasibomoe misingi ya amani ya taifa na mafanikio yake.

Alisema lengo la mkutano huo ni kuweka sawa dhana ya demokrasia ya vyama vingi na kutafuta majibu ya changamoto zinazokabili pasipo kuvunja amani ya nchi.
Profesa Ruth Meena akizungumzia ushiriki wa kijinsia katika demokrasia ya vyama vingi
Profesa Ruth Meena akizungumzia ushiriki wa kijinsia katika demokrasia ya vyama vingi.
Profesa Rugumamu akizungumza
Profesa Rugumamu akizungumza.
IMG_4861
Baadhi ya washiriki wakijadiliana.
IMG_4879
Washiriki wa mkutano wakijadiliana.
wanamdahalo wakiwa makini
Wanamdahalo wakiwa makini.

No comments: