WIZARA
YA KATIBA NA SHERIA
TAASISI
YA MAFUNZO YA UANASHERIA KWA VITENDO TANZANIA
TAARIFA KWA UMMA
UFAFANUZI KUHUSU TUHUMA ZA UBADILISHAJI WA
MATOKEO YA MITIHANI
Utangulizi:
Hivi karibuni kumekuwepo na taarifa zilizoenea katika mitandao ya
kijamii hususan Facebook na WhatsApp zilizoainishwa kama “Tuhuma
Nzito katika Tasnia ya Sheria”. Kwa ufupi, tuhuma hizo zinadai kuwa baadhi ya Wahadhiri
na Watumishi wa Taasisi hii wanafanya “biashara haramu” ya kufelisha wanafunzi kwa makusudi sambamba
na ubadilishaji wa matokeo ya mitihani, hususan Somo la Mirathi (Probate, Administration of Estates and
Trusts).
Ufafanuzi:
Tunapenda kuufahamisha Umma kuwa tuhuma
hizo si za kweli. Kumbukumbu zetu zinaonyesha kuwa wanafunzi wote waliofanya
mitihani wametendewa haki. Wale waliofaulu wamefaulu kihalali na hakuna
aliyefelishwa kwa makusudi. Katika utendaji kazi wa Taasisi watumishi wote
wanafanya kazi kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.
Kwa nafasi hii, tunapenda kueleza juu ya utaratibu wa utayarishaji na utoaji
wa matokeo ya mitihani kama ifuatavyo:-
1. Baada ya mtihani kusahihishwa na jopo la Wahadhiri wa somo husika (Internal Examiners), majibu ya wanafunzi
(answer books) hupelekwa kwa Mtahini
wa Nje ya Taasisi (External Examiner)
kwa ajili ya uhakiki wa usahihishaji na alama za ufaulu zilizowekwa.
2. Baada ya kupokewa kutoka kwa Watahini wa Nje na kuandaliwa, matokeo
huwasilishwa katika kikao cha ndani cha Wahadhiri/Watahini wa Ndani (Panel of Internal Examiners) kwa ajili
kujadiliwa na kutolewa mapendekezo ya kuwasilishwa katika Kamati ya Mafunzo kwa
Vitendo na Mitihani (Practical Legal
Training and Examinations Committee).
3. Baada ya kupokelewa, kujadiliwa na kupitishwa na Kamati ya Mafunzo kwa
Vitendo na Mitihani, Taasisi hutangaza Matokeo ya Awali (Provisional Results) kupitia Tovuti ya Taasisi ambayo inaruhusu
mwanafunzi husika kuona matokeo yake baada ya kuingiza nambari yake ya usajili.
4. Katika hatua ya mwisho, Matokeo ya Awali huwasilishwa kwenye Bodi ya
Uendeshaji wa Taasisi (Governing Board)
kwa ajili ya kujadiliwa na kuthibitishwa kuwa matokeo rasmi (Final Results).
Baada ya matokeo ya awali kutangazwa, mwanafunzi ambaye hajaridhika na matokeo
yake ana haki na fursa ya kuomba uhakiki wa matokeo yake (verification) au kukata rufaa (appeal) au vyote kwa pamoja. Uhakiki
humwezesha mwanafunzi husika kuthibitisha usahihi wa matokeo yake.
Hivyo, Taasisi inatoa rai kwa mwanafunzi ye yote ambaye ana shaka na
matokeo yake kuwa afuate taratibu zilizoelezwa hapo juu.
Mwisho, Taasisi inatoa rai kwa wahusika waliotoa taarifa hizo za uzushi
kuepuka tabia ya kutoa tuhuma bila ushahidi. Tuhuma zilizotolewa zimeleta
usumbufu mkubwa sio tu kwa wahadhiri, wafanyakazi na wanafunzi wa Taasisi bali
pia kwa wazazi/walezi wa wanafunzi na wadau wengine katika tasnia ya Sheria.
IMETOLEWA
NA:
MKUU WA
TAASISI TAASISI YA MAFUNZO YA UANASHERIA KWA VITENDO TANZANIA
(THE LAW SCHOOL OF TANZANIA)
5 Mei, 2015
No comments:
Post a Comment