Tangazo

August 14, 2015

HAKUNA UGONJWA WA EBOLA NCHINI YASEMA WIZARA YA AFYA

Na Magreth Kinabo – Maelezo
 
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imesema kwamba  uchunguzi wa sampuli  ya mgonjwa mwenye umri wa miaka 39 kutoka katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu, iliyopo mkoani  Kigoma, iliyopelekwa  kwenye Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii,ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iliyopo Dar es Salaam,  vipimo havijaonyesha kuwa ni ebola, wala  dengue, chikungunya na RVF.
 
Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu Mkuu wa wizara hiyo,Dkt. Donald Mmbando (pichani) wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mgonjwa huyo aliyehisiwa kuwa na ugonjwa wa kutoka damu mkoani Kigoma,ambaye sampuli yake ilichukuliwa Agosti 11, mwaka huu na   kupelekwa  kwenye maabara hiyo.  
 
Mgonjwa huyo aliyepokelewa katika hospitali ya Mkoa wa Kigoma Maweni Agosti 9, mwaka huu  akiwa na dalili za kutokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili hasusan kwenye fizi, macho na masikio  na kufarikia dunia Agosti 10, mwaka huu.
 
“Maabara hii imepima uwepo wa virusi vinavyoweza kusabbaisha ktokwa na damu , vipimo hivyo havijaonyesha maambukizi yoyote ya virusi hivyo. Kesi ya Kigoma haikuwa ni ebola, lakini tunaendelea kufuatilia kwa karibu kujua tatizo tutatoa taaarifa, alisema Dkt.Mmbando.

 Aliongeza kuwa Tanzania imejipanga kwa  vifaa tiba na wataalamu ili kama tatizo hilo litajitokeza watalidhibiti, hivyo imewataka wananchi kutokuwa na hofu.Wizara  yake imejiandaa vyema kudhibiti ugonjwa huu iwapo utaingia nchini ikiwa ni pamoja na kutengeneza mpango kazi wa udhibiti wa ugonjwa huu wa miaka mitatu kuanzia 2015 hadi 2017.

 Dkt. Mmbando aliongeza kwamba   sampuli hizo zimepelekwa  katika maabara ya KEMRI Nairobi  kwa ajili ya uhakiki kulinganisha ubora wa kimaabara, ambapo ni taratibu za upimaji  wa sampuli ambazo Shirika la Afya la Dunia(WHO) imeweka kama mwongozo na kutoa maabara ambazo zinaweza kutumika kuhakiki ikiwemo ya KEMRI.

 Aidha  imesema kwamba  damu. itapeleka  sampuli kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kubaini chanzo cha kifo chake.

 “Maabara ya Mkemia Mkuu  wa Serikali  ndiyo ya mwisho ya kutupatia majibu sahihi ya kitu au dawa gani iliyomdhuru,” alisisitiza.

 Ugonjwa wa ebola umeendelea kuenea katika nchi za Afrika ya Magharibi ambapo hadi sasa nchi tatu ambazo ni Guinea, Liberia na Siera Leone, zimeendelea kutoa taarifa za wagonjwa wapya.

 Aidha, mpaka kufikia  Agosti 9, mwaka huu, idadi ya wagonjwa waliothibitishwa kuwa na ugonjwa huu ni 27,965 na vifo 11,298.

 Dkt. Mmbando alisema  kuna sababu mbalimbali zinazosababisha kutokwa na damu,ikiwemo maambukizi ya virusi na bacteria, ini kutofanya kazi vizuri kama kemikali mbalimbali. Virusi hivyo ni kama Ebola, Marburg, Dengue, Rift Valley, Chikungunya, Lassa na Crimean –Congo.

 Mgonjwa huyu alikuwa ni mkimbizi wa kutoka nchi ya Burundi ambaye ameishi katika kambi ya Nyarugusu kwa miaka mitatu. Mgonjwa huyu alikuwa mmojawapo wa wakimbizi waliokuwa wasafirishwe katika mpango wa kawaida chini ya Shirika la Kimataifa linalohudumia wakimbizi kwenda Marekani. Safari hiyo ilikuwa ianze tarehe 9 Agosti 2015.
 

No comments: