Tangazo

September 21, 2016

WATU 283 WAJITOKEZA KUPIMA VVU/UKIMWI KWENYE MKESHA WA MWENGE WILAYANI IKUNGI

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu akikimbia na baadhi ya watumishi wa Wilaya yake ishara ya kuukabidhi Mwenge wa uhuru Manispaa ya singida mara baada ya kumaliza mbio zake Wilayani Ikungi
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Ikungi Hassan Tati akizungumza wakati wa kuwashukuru wananchi kwa kujitokeza kupima Virusi Vya Ukimwi
Wananchi wa Manispaa ya Singida wakiusubiri Mwenge wa Uhuru kwa shauku kubwa muda mchache kabla ya kuwasili katika eneo lao ukitokea Wilaya ya Ikungi

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ndugu George Jackson Mbijimaakitoa salamu za shukrani kwa wakazi wa Ikungi
 Watumishi wa Wilaya ya Ikungi katika ubora wao
 Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu akizungumza muda mchache kabla ya kuukabidhi Mwenge wa Uhuru kwa Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhe Elias Tarimo
Askari Polisi wakiulaki Mwenge wa Uhuru 
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ally J. Mwanga akisisitiza jambo wakati wa Mkutano wa Shukrani kwa wananchi wa Wilaya ya Ikungi kwa kushiriki kukimbiza Mwenge wa Uhuru

Na Mathias Canal, Singida

Jumla ya wakazi 283 wa Wilaya ya Ikungi, Mkoani Singida wakiwemo wanaume 71 na wanawake 83 sawa na asilimia 29% wamejitokeza kupima Virusi vya Ukimwi VVU ambapo wananchi wanne sawa na asilimia 1.4% kati yao ndio waliokutwa na maambukizi hayo ambapo wanaume ni wawili na wanawake ni wawili.

Mbio za Mwenge wa Uhuru kwenye mapambano dhidi ya UKIMWI zina ujumbe usemao Tanzania Bila Maamubukizi Mapya chini ya kauli mbiu ya "Unyanyapaa na vifo vitokanavyo na Ukimwi inawezekana" imekuwa ikiwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya zao ili kurahisishia serikali kujua hali ilivyo ya maambukizi kama inapungua ama inaongezeka ili kufahamu namna bora ya kuisaidia jamii kupunguza maambukizi hayo yasiyo kuwa na lazima.

Akitoa taarifa hiyo wakati akiwashukuru wananchi kwa kushiriki kwenye mkesha na shughuli nzima za Mwenge wa Uhuru tangu ulipowasili Wilayani hapo jana asubuhi Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu amesema kuwa Watanzania wanaweza kuepuka vifo visivyo kuwa vya lazima pamoja kwa kupima na kuzifahamu afya zao kwa itakuwa rahisi kwa wao kupatiwa dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi jambo ambalo litawafanya kuishi muda mrefu kuliko kuishi na Virusi vya Ukimwi kwa kificho kwani ni hatari kwa mustakabali wa Maisha yao na kusababisha vifo vya haraka mara baada ya kuathirika.

Hata hivyo Dc Mtaturu ameutaja ugonjwa wa Maralia kuwa ni miongoni mwa magonjwa yanayowasumbua watu wengi katika Wilaya hiyo ambapo mwaka 2015/2016 ugonjwa huo uliongoza katika magonjwa kumi ndani ya Wilaya.

Alisema kuwa wastani wa vifo katika Wilaya ya Ikungi vilivyotokana na Maralia kwa Mwaka 2015/2016 ni watu 6 kwa upande wa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, wenye umri zaidi ya miaka mitano ni wawili huku kwa upande wa wanawake kukiwa hakuna kifo kilichoripotiwa.

Sambamba na hayo pia alisema kuwa jumla ya wagonjwa 35,408 waliugua Malaria, kati yao watoto wenye umri chini ya miaka mitano ni 15,788 na wenye umri zaidi ya miaka mitano ni 19,620.

Naye Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ndugu George Jackson Mbijima amewashukuru wananchi kwa umoja wao kwa kujitokeza kwa wingi kwenye shughuli za Kukimbiza Mwenge huo kwani wameonyesha imani kubwa tena kwa vitendo na serikali ya awamu ya Tano yenye kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu.

Mbijima alisema kuwa ni jambo la nadra sana kwa baadhi ya wananchi kujitokeza kupima kutokana na Jografia pamoja na dhana ya kuamini kuwa kujitokeza kupima ni kujiaibisha ama kurahisisha vifo kutokana na mawazo mara baada ya kifahamu afya zao.

Sambamba na hayo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Singida Hassan Tati akitoa salamu za Shukrani kwa niaba ya CCM amewapongeza wananchi kujitokeza kwa wingi kuunga mkono Mwenge wa uhuru kwani ni dhahiri kuwa wameonyesha kukiamini Chama Cha Mapinduzi CCM na serikali ya awamu ya tano kwa kuenzi Nembo ya Taifa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ally J. Mwanga alisema kuwa baraza la madiwani ambalo analisimamia litatekeleza maagizo yote muhimu yaliyotolewa na kiongozi wa Mbio za Mwemge kitaifa kwa manufaa ya wananchi.

Ukiwa Wilayani Ikungi Mwenge wa Uhuru umetoa hamasa na Ari kwa vijana na wananchi wa Wilaya ya Ikungi ambapo pia umetembea umbali wa Kilomita 141.5 na kutembelea miradi 9 yenye jumla ya Shulingi Milioni 975,991,180.44.

Tayari Mwenge wa uhuru umekabidhiwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhe Elias Cholo Tarimo ambapo hii leo utakimbizwa katika Manispaa ya Singida na kuzuru takribani Kilomita 96 na kuzindua Miradi pamoja na kuweka mawe ya msingi 8 yenye thamani ya jumla ya shilingi Bilioni 7,402,091,775.

No comments: